Dar es Salaam. Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, Mei mosi kesho, yanatarajiwa kuambatana na hisia mseto miongoni mwa wafanyakazi, kufuatia kupanda kwa nauli za mabasi ya mikoani na daladala.

Wengi wao wanatega masikio kusikia iwapo kutatangazwa ongezeko la mishahara litakaloendana na hali halisi ya maisha inayozidi kuwa ngumu, hasa katika kipindi hiki kutokana na kupanda kwa bei za mafuta.

Mbali na suala la mishahara, wafanyakazi wamesema wanatarajia Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti bei za biadhaa zinazoendelea kuathiri uwezo wao wa kumudu gharama za maisha, hasa baada ya kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali.

Hata hivyo, wapo wanaoona kuwa kupanda kwa gharama za maisha kumetokana na hali ya dharura isiyotabirika, hivyo hawana sababu ya kuishinikiza Serikali moja kwa moja.

Badala yake, wanasisitiza umuhimu wa kuongeza bidii kazini ili kukuza uchumi na kukabiliana na changamoto hizo.

Maadhimisho ya Mei mosi mwaka huu yakayofanyika mkoani Njombe, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi, yanafanyika katika kipindi ambacho bei ya mafuta imeongezeka nchini na duniani kote, hali inayochangiwa na athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati unaohusisha Marekani, Israel na Iran.

Mgogoro huo umeathiri usafirishaji wa mafuta duniani, hususan baada ya kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, unaopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa kimataifa.

Kupanda kwa bei ya mafuta kumesababisha ongezeko la gharama za uzalishaji, usafirishaji na hatimaye bei za bidhaa na huduma, zikiwemo nauli za usafiri wa umma.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilitangaza viwango vipya vya nauli za daladala na mabasi ya mikoani vitakavyoanza kutumika kesho.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, nauli za mabasi ya mijini (daladala) zimeongezeka kwa Sh100 kwa kila safari, ambapo kiwango cha chini sasa ni Sh700 kutoka Sh600 kwa umbali usiozidi kilometa 10.

Aidha, nauli za safari za masafa marefu zimepanda kulingana na umbali, huku baadhi ya mikoa ikishuhudia ongezeko kubwa zaidi, ikiwemo Mwanza (Sh9, 000), Morogoro (Sh2, 000), Dodoma (Sh4,000) na Arusha (Sh5, 000).

Akizungumzia sherehe za Mei mosi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema zitafanyika katika kiwanja kipya kilichopo katika eneo la Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”

Matarajio, kilio cha wafanyakazi

Kutokana na mazingira ya maadhimisho ya Mei mosi mwaka huu, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu na Wafanyakazi wa Shule Zisizo za Serikali Tanzania (TPTU), Julius Nkoba amesema wanatarajia Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti mfumuko wa bei unaoathiri moja kwa moja kipato cha wafanyakazi.

Sambamba na hilo, amesema ni matarajio yao kuiona Serikali ikifanya marekebisho ya mishahara kwa kuwaongezea wafanyakazi wa umma na binafsi kwa viwango vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya sasa.

Kuhusu nauli mpya zinazotarajiwa kuanza kutumika Ijumaa, Mei mosi 2026, Nkoba amesema wanatarajia kuwepo kwa uwazi katika upangaji wake, pamoja na kuhakikisha zinaendana na uwezo wa wananchi.
“Nauli mpya zitakazotangazwa ziwe na uwiano wa haki na uwezo wa wananchi, zikitokana na tafiti huru na shirikishi,” amesema.

Kutokana na mabadiliko hayo ya nauli, ameongeza kuwa wanatarajia Serikali kuboresha usafiri wa umma ili wananchi wapate huduma inayolingana na thamani ya fedha wanazolipa.

Aidha, amesema matarajio yao ni kuona Serikali inalinda ajira na haki za wafanyakazi kwa kusimamia kikamilifu sheria za kazi, ili kuzuia vitendo vya unyonyaji na ajira zisizo na staha.

Pia amesisitiza umuhimu wa kukuza ajira mpya kwa vijana kwa kuongeza uwekezaji katika sekta zenye uwezo wa kuajiri watu wengi.

Vilevile, Nkoba amesema wanatarajia Serikali kusikiliza sauti za vyama vya wafanyakazi na kuhakikisha maamuzi yote ya kiuchumi yanashirikisha wadau muhimu, ikiwemo vyama hivyo.

Mbali na matarajio hayo, ametaja matamanio yao kuwa ni kuona ukuaji wa uchumi unaoakisiwa moja kwa moja katika maisha ya kila Mtanzania, pamoja na kuwepo mifumo imara ya kulinda wafanyakazi wakati wa dharura na hata baada ya kustaafu.
“Kuimarishwa kwa sekta ya elimu ili kuzalisha rasilimali watu yenye ushindani na wananchi wapate huduma bora za afya bila mzigo mkubwa wa kifedha,” amesema.

Ameongeza kuwa wanatamani kuona mfumo wa usafiri unaowahudumia wananchi kwa ufanisi na kwa gharama nafuu, pamoja na kuimarishwa kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na haki katika utoaji wa huduma za umma.
“Tunatamani jamii yenye usawa, haki na mshikamano bila ubaguzi wa aina yoyote. Tunaamini utekelezaji wa matarajio na matamanio haya utasaidia kujenga Taifa lenye ustawi, haki na maendeleo kwa wote,” amesema.

Wakati TPTU ikitoa matarajio hayo, Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari, Ufundi Stadi na Utafiti (Raawu) kimesema kinaamini ukimya wa Serikali una maana ndani yake.

Mwenyekiti wa chama hicho, Jane Mihanji amesema wanatarajia kuona Serikali ikichukua hatua zitakazosaidia kupunguza makali ya maisha kufuatia kupanda kwa gharama zinazosababishwa na ongezeko la bei ya mafuta.
“Tunajua kwa kupanda kwa bei ya mafuta na gharama za maisha zitapanda, lakini tunaamini Serikali ni sikivu na itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kunakuwa na unafuu,” amesema.

Amewahimiza wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na tija kwa Taifa, akibainisha kuwa wao ndiyo kundi muhimu katika kukuza uchumi wa nchi.

Hata hivyo, amesema mwaka jana ulikuwa na mafanikio kwa wafanyakazi, baada ya Serikali kutekeleza baadhi ya madai yao, ikiwemo kuongeza kima cha chini cha mshahara. Ameongeza kuwa watumishi wa umma walipandishwa madaraja kwa wingi, huku wajawazito waliojifungua kabla ya muda wakiongezewa siku za likizo, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Vitu vingi wafanyakazi tulivyokuwa tunadai Serikali imevitimiza, hivyo mwaka huu tunatarajia mazuri zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (Tughe), Henry Mkunda amesema matarajio yao ni kuona wafanyakazi wanashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Tunatarajia wafanyakazi wanakuwa sehemu ya utekelezaji wa dira kwa sababu hatuwezi kujitenganisha na suala hilo muhimu kwa Taifa letu,” amesema.

Akizungumzia gharama za maisha na nauli mpya, Mkunda amesema ni wazi kuwa changamoto hizo zimesababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani, jambo ambalo halikutarajiwa.

Amesema tayari wamewasiliana na Serikali ili kutafuta suluhisho, lakini si kwa shinikizo bali kwa ushauri.
“Tumeshazungumza na Serikali kuwaambia wazingatie namna ya kutusaidia. Sio suala la kuomba kwa nguvu, tunajua ni kushauri hivyo tunatarajia Serikali itakuja na jambo lolote kuhusu hilo,” amesema.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema jukumu la shirikisho hilo ni kuwahimiza wafanyakazi kuongeza bidii kazini ili kukuza uzalishaji, kwani hapo ndipo msingi wa kudai haki unapoanzia.

Ameongeza kuwa katika miaka mitatu iliyopita, wafanyakazi wameshirikiana vizuri na Serikali na kushuhudia ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma, jambo ambalo halikuwa la kawaida hapo awali.
“Lakini kwa mwaka huu nini kitatokea tusubiri kuona Rais atasema nini, tunatarajia majibu yatapatikana Mei mosi,” amesema Nyamhokya.

Daladala na nauli mpya

Kwa upande wa wadau wa usafiri, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwanya Lema, amesema katika mazungumzo yao na Latra walikubaliana kuongeza Sh100 kwa kila safari na kwa wanafunzi zimebaki vilevile Sh200 kwa kila safari.
“Tulifanya mazungumzo na mamlaka husika na makubaliano tukakubaliana ongezeko la Sh100 kwa kila safari na Sh200 ilrile kwa wanafunzi, na hili lipo wazi,” amesema Lema, akisisitiza kuwa lengo si kuwaumiza abiria bali kuhakikisha huduma inaendelea bila kukwama.

Naye Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John amesema abiria wanapaswa kuelewa mfumo wa nauli mpya kwa kuzingatia umbali wa safari.
“Hapa ni kuzidisha tu kiwango kilichowekwa kwa kila kilometa ya safari. Kwa mfano, wanaokwenda Mwanza wameongezewa Sh9, 000 kwa magari ya kawaida, Dodoma Sh4, 000, Morogoro Sh2,000 na Arusha Sh5,000,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *