Mradi wa ujenzi wa bandari kavu ya Katosho uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma, umeendelea kubaki kuwa kitendawili kwa wananchi na wadau wa maendeleo, huku ukitajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyokusudiwa kuimarisha sekta ya usafirishaji na biashara nchini.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2019, unalenga kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari za Dar es Salaam na Kigoma, sambamba na kuboresha ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi, hasa kwa nchi za ukanda wa Maziwa Makuu zinazotegemea Ziwa Tanganyika, zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Tanzania.

Kupitia mradi huo, huduma za upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa mizigo zilitarajiwa kurahisishwa kwa kiasi kikubwa, hatua ambayo ingeleta nafuu ya muda na gharama kwa wafanyabiashara, huku ikiimarisha ushindani wa kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hata hivyo, zaidi ya miaka mitano tangu kuanza kwake, utekelezaji wa mradi huo unaonekana kusuasua, hali inayozua maswali mengi kuhusu hatima yake, huku wananchi waliopisha mradi huo wakieleza wasiwasi wao.

Wananchi wa Kata ya Kibirizi, eneo ambalo mradi huo unatekelezwa, wanasema licha ya kuhamishwa tangu mwaka 2015 kupisha ujenzi huo, hakuna maendeleo ya kuridhisha yaliyofanyika hadi sasa.

Badala ya kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi, eneo hilo limegeuka kuwa maegesho ya malori yanayofanya safari zake kuelekea Rwanda, jambo linaloongeza sintofahamu kuhusu dhamira ya mradi huo.

Mkazi wa Soweto, Malik Bocho, anasema wananchi hawajui kinachoendelea na wanahisi huenda kuna changamoto kubwa ambayo haijawekwa wazi kwa umma.

“Hadi sasa sisi kama wananchi hatujui kinachoendelea kuhusiana na mradi huu, kwani bandari hii ingekuwa imekamilika sisi kama vijana tungeweza kupata ajira na kupata maendeleo katika mji wetu,” anasema Bocho.

Anaongeza: “Vijana wengi hatuna kazi tunazunguka mtaani bila uelekeo hivyo tunaiomba serikali iweze kulifikiria hili kwa nini bandari imeendelea kukaa bila kufanya kilichokusudiwa na badala yake imekuwa kama maegesho ya magari, ni muhimu serikali ikafanya lengo la awali la kuwapo kwa bandari hiyo.”

Kwa upande wake, Buchumi Ali anasema ukosefu wa taarifa rasmi umeacha mianya ya uvumi, huku baadhi ya wananchi wakiamini huenda mradi huo umehamishwa.

“Kama serikali imeshindwa kuendeleza mradi huu basi ni bora wananchi wakarudishiwa maeneo yao ili waweze kuishi na kuyaendeleza kama awali kwani kuna baadhi ya wananchi hadi sasa bado wanahangaika na hawana makazi maalumu ya kuishi,” anasema Ali.

Fidia na malalamiko

Mmoja wa wananchi waliolipwa fidia, Rugegwa Juma, anasema kuchelewa kwa mradi huo kumeongeza mateso kwa baadhi ya wakazi waliopisha eneo hilo.

Anasema kama serikali haina mpango wa kuendeleza mradi huo kwa sasa, ni vyema ikaangalia uwezekano wa kuanzisha mradi mwingine utakaoweza kuchochea uchumi wa eneo hilo.

“Maeneo haya usalama wake ni mdogo hususani nyakati za usiku watu wanatekwa, wakina dada wanafanyiwa vitu ambavyo havifai na hali hii inatokana na eneo hili kuwa na uwazi mkubwa kutoka eneo la mradi hadi kufika kwenye makazi ya watu,” anasema Juma.

Anaongeza kuwa, kutokana na kuwa sehemu ya ulinzi shirikishi, amewahi kushuhudia na hata kuokoa baadhi ya wanawake waliokuwa wakikumbwa na vitendo vya uhalifu.

“Niliwahi kuwaokoa wanawake waliokuwa wamezingirwa na vijana watano ambao awali waliwaibia simu na kisha kutaka kuwabaka,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Butunga, Hamisi Yasini, anasema tathmini ya awali ya eneo hilo ilifanyika mwaka 2012, huku malipo ya fidia yakianza mwaka 2015 ili wananchi waweze kupisha mradi huo.

Hata hivyo, anasema hadi sasa hakuna maelezo ya kuridhisha kuhusu hatima ya mradi huo, huku akibainisha kuwa matukio ya kihalifu yameongezeka katika maeneo yanayozunguka mradi.

“Matukio hayo ya kihalifu yalikuwa yanatokea na tumeendelea kupambana nayo kwani kuna baadhi ya watu tuliwafikisha polisi na wengine mahakamani lakini bado matukio hayo yanaendelea na kwa siku za hivi karibuni nimepokea taarifa ya kina mama kubakwa na watoto kulawitiwa,” anasema Yasini.

Anaongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2025, amepokea matukio saba hadi nane ya aina hiyo, hali inayoongeza umuhimu wa serikali kuchukua hatua za haraka.

Kuhusu fidia, anasema baadhi ya wananchi walilipwa fedha zote, wengine walilipwa kiasi kidogo kisicholingana na thamani ya mali zao, huku wengine wakikosa kabisa fidia na kulazimika kufungua kesi mahakamani kudai haki zao.

Kuhusu utekelezaji wake

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti dada la The Citizen ya Aprili 16, 2026, mwaka 2021 Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilitoa Sh12 bilioni kwa ajili ya fidia kwa wananchi 1,228 wa Katosho na Kigoma waliopisha mradi huo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa wananchi 1,196 walikubali fidia hiyo, huku 31 wakikataa kuipokea wakidai viwango vilivyotolewa havikulingana na thamani halisi ya mali zao.

Mradi huo umetajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa TPA, ukitarajiwa kuhudumia si Tanzania pekee bali pia nchi za Afrika Mashariki na ukanda wa Maziwa Makuu.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Rashidi Chuachua, anasema utekelezaji wake ulianza rasmi mwaka 2019 katika eneo la hekta 67.

Anabainisha kuwa kati ya eneo hilo, hekta 10 zilitengwa kwa ajili ya Burundi na hekta 15 kwa ajili ya DRC, huku zaidi ya Sh2.4 bilioni zikitengwa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mradi.

“Katika mchakato wa kuufungua mkoa wa Kigoma kumekuwa na mipango ya kuimarisha miundombinu ya reli na barabara, pia kusogeza huduma karibu kwa nchi tunazozihudumia za Burundi na DRC Congo ikiwa nia ni kuwezesha mizigo kuchukuliwa hapa Kigoma badala ya Dar es Salaam,” anasema Chuachua.

Anaeleza kuwa awamu ya kwanza ya mradi ilihusisha ujenzi wa uzio na ilikamilika kwa asilimia 100 ndani ya kipindi cha miezi tisa kuanzia Machi hadi Desemba 2019, ikitekelezwa na kampuni ya Josam JV Satellite Construction Ltd.

Kwa mujibu wa Chuachua, hatua inayofuata ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupata mkandarasi wa kufanya upembuzi yakinifu utakaoongoza uwekaji wa miundombinu muhimu kama maji, umeme na sakafu ngumu.

Hoja ya uhitaji wa mradi

Katika mjadala wa Bunge mwaka 2022, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda, alihoji kuhusu mpango wa serikali kukamilisha mradi huo.

Akijibu swali hilo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, alisema kuwa kiwango cha mizigo kinachopitishwa katika bandari ya Kigoma bado hakijafikia uwezo wake kamili.

Alieleza kuwa bandari hiyo hupitisha wastani wa tani 180,000 hadi 200,000 kwa mwaka, wakati uwezo wake ni tani 700,000 kwa mwaka, sawa na chini ya asilimia 50 ya uwezo wake.

Kauli hiyo inaashiria kuwa, kwa wakati huo, kulikuwa na hoja ya kiuchumi kuhusu uharaka wa kuendeleza bandari kavu ya Katosho, kutokana na bandari ya Kigoma kutokuwa imelemewa.

Wataalamu wa uchumi wanaona kuchelewa kwa mradi huo kunaibua maswali kuhusu utekelezaji wa sheria na sera za uwekezaji nchini.

Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022, iliyofuta ile ya mwaka 1997, inalenga kuweka mfumo madhubuti wa kuratibu, kuvutia na kulinda uwekezaji nchini.

Aidha, mwaka 2025 Tanzania ilipitisha sheria mpya inayounganisha maeneo ya uwekezaji na kanda maalum za kiuchumi, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na ufanisi wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa mantiki hiyo, kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi wa bandari kavu ya Katosho kunaonekana kwenda kinyume na dhamira ya kuharakisha uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *