Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema katika mandalizi ya kuelekea mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, Serikali itajenga viwanja vya mazoezi ndani ya mbuga zenye wanyama wapole.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza Simba SC kwa ushindi ilioupata dhidi ya Yanga katika fainali ya Kombe la Muungano, huku akisema Simba ni timu yake ya kazini.

“Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza timu yangu ya kazini Simba kwa ushindi walioupata jana, hii ni baada ya mechi nane mfululizo hatimaye jana wakashinda kwa taabu sana,” amesema Waziri Mkuu.

Simba ilishinda mechi hiyo iliyochezwa Aprili 29, 2026 kwenye Uwanja wa New Aman Complex baada ya kupata penalti dakika za mwisho wa mchezo uliodumu kwa dakika 120 mfungaji akiwa Seleman Mwalimu.

Kuhusu viwanja vya mazoezi AFCON 2027, Dk Nchemba amesema lengo la kuvijenga maeneo ya mbuga za wanyama ni kuendelea kuvutia watalii na kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Aman (CCM), Abdul Yusus Maalim ambaye ameuliza Serikali imejiandaa vipi kuyatumia mashindano hayo kwa ajili ya kutangaza utalii na kuongeza pato la nchini.

Waziri Mkuu amesema, Serikali imefanya maandalizi kwa hatua kubwa ikiwemo kuandaa miundombinu ambapo kwa sasa imeunda kamati ambayo inatafuta namna ya kukamilisha mkakati wa kuhakikisha nchi inanufaika na mashindano hayo.

“Lakini miongoni mwa maandalizi hayo, Serikali itaandaa viwanja vya mazoezi katika mbunga za wanyama ambako hakuna wanyama wakali ili wakati wachezaji wanafanya mazoezi wawe wanaona wanyama pia,” amesema Dk Nchemba.

Amesema kila uwanja utakaotumika kwenye mashindano hayo kutakuwa na uwekezaji wa kibiashara ili kuhakikisha vijana wananufaika na fursa hizo ambapo barabara zote zitakazoelekea kwenye viwanja zitafungwa taa ili kuruhusu biashara wakati wote.

Kuhusu mkakati wa utalii, amesema tayari wameshaelekeza Wizara husika watengeneze bango ambalo litatoa mwongozo kwa wageni kujua mahali walipo hadi kuelekea kwenye mbunga au hifadhi yoyote itawachukua muda gani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *