Dar es Salaam. Jana Jumatano, Aprili 29, 2026 Wekundu wa Msimbazi, Simba walifanikiwa kuweka historia nyingine baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mechi ya fainali ya Kombe la Muungano iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.

Katika mchezo huo mkali uliowakutanisha watani hao wa jadi, ulishuhudiwa ukimalizika dakika 90 bila mbabe na kuongezwa 30 za ziada ambazo ndizo ziliamua bingwa wa michuano hiyo baada ya mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu kufunga kwa mkwaju wa penalti bao pekee kufuatia faulo aliyochezewa Clatous Chama ndani ya eneo la hatari dakika mbili kabla ya mechi hiyo kumalizika.

Simba imetwaa taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili ambapo mara ya mwisho Wekundu hao wa Msimbazi kutwaa taji ilikuwa 2024 ilipobeba Ubingwa wa kombe hilo Visiwani Zanzibar. Simba imeifunga Yanga kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka mitatu bila ushindi baada ya mara ya mwisho kuifunga kwa mikwaju ya penalti mwaka 2023 na kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii.

Kocha wa Simba, Steve Barker amefanikiwa kubeba taji la kwanza akitumia siku 131 tangu alipotambulishwa klabuni hapo Desemba 19, 2025. Berker ametwaa taji hilo baada ya kupita makocha watatu bila mafanikio ambao ni Abdelhack Benchikha, Fadlu Davids na Dimitar Pantev.

Mara ya mwisho Simba kutwaa taji ilikuwa chini ya nahodha John Bocco ambaye kwa sasa amestaafu kucheza soka akiinoa timu ya vijana ya Simba.

Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe na Chama ni wachezaji pekee ambao walikuwepo mara ya mwisho wakati Simba inanyanyua ubingwa wa Ngao ya Jamii 2023.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amepoteza mechi ya kwanza katika mashindano ya ndani tangu alipotambulishwa Oktoba 25, 2025 alikuwa hajawahi kupoteza mechi yoyote ya mashindano ya ndani huku akifanikiwa kubeba Kombe la Mapinduzi 2026.

Mara ya mwisho Yanga ilifungwa mabao 3-1 na APR katika robo fainali ya Kombe la Mapinduzi 2024, mechi iliyochezwa Januari 7, 2024 kwenye Uwanja wa Amaan Complex. Baada ya hapo, imekuja kufungwa tena jana Jumatano, Aprili 29, 2026 uwanjani hapo.

Watani hao wa jadi watakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ambayo itapigwa Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Meja General Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *