Dar es Salaam. Njombe imeendelea kuthibitisha ubora wake katika masuala ya usafi wa mazingira baada ya kuibuka kinara kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo, matokeo yanayoakisi uwekezaji wa muda mrefu katika mifumo ya usimamizi wa taka na uhamasishaji wa jamii.

Katika matokeo ya Mashindano ya Kitaifa ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2026 yaliyotangazwa jana Jumatano, Aprili 29, 2026 mafanikio ya Njombe yameonekana katika ngazi mbalimbali, kuanzia wilaya, miji, vijiji hadi taasisi za elimu na vituo vya afya, hali inayothibitisha juhudi za pamoja za wakazi na viongozi wake.

Wakati Njombe ikiendelea kung’ara, vyuo vikuu vitatu Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) navyo vimeibuka vinara wa usafi katika kundi la taasisi za elimu ya juu.

Katika kundi hilo, NM-AIST cha Arusha imechukua nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na UDSM huku Sua ikishika nafasi ya tatu. Mashindano hayo, yanayoratibiwa na Wizara ya Afya, yanalenga kuhamasisha jamii kulinda afya kupitia mazingira safi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hizo, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema ushindi huo ni matokeo ya juhudi za pamoja katika kuimarisha afya ya jamii.

“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunadhibiti utupaji holela wa taka, kutumia vyoo bora, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, pamoja na kutumia maji safi na salama ya kunywa,” amesema.

Ameongeza hatua hizo zina mchango mkubwa katika kupunguza mzigo wa magonjwa kwa familia, ikiwa ni pamoja na gharama za matibabu na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema juhudi za usafi wa mazingira nchini zimeanza tangu mwaka 1987, zikiwa na lengo la kuimarisha afua za kinga dhidi ya magonjwa.

Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)

Amesisitiza magonjwa mengi yanaweza kuzuilika kwa kuzingatia usafi wa mazingira na usafi binafsi, akitaja magonjwa kama kipindupindu, kuhara, kuhara damu na homa ya matumbo kuwa yanahusiana moja kwa moja na tabia duni za usafi.

“Tunapaswa kuimarisha kinga kwa kuzingatia usafi wa mazingira na usafi binafsi. Hii ni silaha muhimu ya kupunguza mzigo wa magonjwa katika jamii,” amesema Dk Magembe.

Ameongeza falsafa ya usafi inapaswa kuonekana kama nidhamu ya pamoja, si jukumu la mtu mmoja au familia moja pekee.

“Nyumba moja inapokuwa safi lakini mtaa mzima ukawa mchafu, afya ya nyumba hiyo bado iko hatarini. Kama kijiji kimoja kinatunza kisima lakini kingine kikachafua chanzo cha maji, ugonjwa hausimami kwenye mipaka ya kitongoji,” amefafanua.

Kwa mujibu wake, usafi ni mkataba wa kijamii unaohitaji ushiriki wa kila mmoja ili kuwa na matokeo chanya kwa taifa zima.

Matokeo kwa ujumla

Mbali na vyuo vikuu kuongoza katika usafi wa mazingira, matokeo ya mashindano ya mwaka 2026 pia yameonyesha ushindani mkubwa katika ngazi za halmashauri, shule na vituo vya huduma za afya, huku maeneo ya Nyanda za Juu Kusini yakijitokeza kwa nguvu.

Katika kundi la halmashauri za majiji, Jiji la Arusha limeibuka mshindi wa kwanza, likifuatiwa na Jiji la Mwanza katika nafasi ya pili na Jiji la Tanga likishika nafasi ya tatu. Ushindi huo unaonyesha juhudi za majiji hayo katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji taka na kuhamasisha usafi wa mazingira kwa wakazi wake.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa upande wa halmashauri za manispaa, Manispaa ya Shinyanga imeongoza, ikifuatiwa na Manispaa ya Iringa huku Manispaa ya Moshi ikichukua nafasi ya tatu. Katika kundi la miji, Mji wa Njombe umeibuka kinara, ukifuatiwa na Mji wa Mafinga na Mji wa Babati.

Ngazi ya wilaya pia ilishuhudia ushindani mkali ambapo Wilaya ya Njombe imechukua nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Wilaya ya Makete na Wilaya ya Mufindi. Mafanikio ya Njombe katika ngazi tofauti yanaonyesha uwekezaji mkubwa katika usafi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii.

Katika kundi la mitaa, Mtaa wa Kwivaha uliopo Mji wa Njombe umeongoza, ukifuatiwa na Mwereni wa Manispaa ya Moshi na Miti Mirefu wa Manispaa ya Shinyanga. Kwa upande wa vijiji, Ihang’ana na Ukalawa vyote vya Wilaya ya Njombe vimechukua nafasi ya kwanza na pili mtawalia, huku Utanziwa cha Wilaya ya Makete kikishika nafasi ya tatu.

Sekta ya elimu nayo haikubaki nyuma. Katika shule za msingi za serikali, Shule ya Msingi Ihang’ana na Ukalawa za Wilaya ya Njombe zimeongoza, huku Azimio ya Jiji la Mbeya ikishika nafasi ya tatu. Kwa shule za sekondari za bweni, Ahmes Mbweni ya Dar es Salaam imeibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Nyangao ya Wilaya ya Mtama na St. Francis Girls ya Mbeya.

Katika sekta ya afya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha – Mount Meru imeongoza kwa hospitali za rufaa za mikoa, ikifuatiwa na Manyara na Amana ya Dar es Salaam. Kwa hospitali za halmashauri, Hospitali ya Mji wa Njombe imeibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Chunya ya Mbeya na Mafinga.

Kwa ujumla, matokeo hayo yanaonyesha kuwa usafi wa mazingira si tu ushindani bali ni utamaduni unaojengwa, huku Njombe ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa maeneo mengine nchini katika kulinda afya na mazingira.

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST)

Baadhi ya vigezo vilivyotumika katika mashindano hayo ni pamoja na uwepo wa mifumo bora ya ukusanyaji na utupaji wa taka, hali ya vyoo na miundombinu ya maji, pamoja na ushiriki wa wanafunzi na watumishi katika shughuli za usafi.

Washindi hao wametajwa kuwa mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za elimu ya juu na jamii kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki ambapo serikali inaendelea kusisitiza kinga dhidi ya magonjwa kupitia usafi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *