Upofu na matatizo ya kuona kwa watoto ni miongoni mwa changamoto kubwa za afya ya umma duniani.

Licha ya maendeleo ya kitabibu na kiteknolojia yaliyosaidia kupunguza baadhi ya visababishi vya upofu, bado mamilioni ya watoto wanaishi na hali hii, hususan katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani watoto milioni 1.4 duniani wanaishi na upofu, huku makumi ya mamilioni wakikabiliwa na matatizo mbalimbali ya kuona.

Hali hii haiathiri tu afya ya mtoto, bali pia huathiri elimu yake, ustawi wa kijamii, na hata uwezo wa kiuchumi wa jamii kwa ujumla.

Barani Afrika, hali ni mbaya zaidi ukilinganisha na wastani wa dunia. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 75 ya watoto vipofu duniani wanaishi Afrika na Asia.

Nchini Tanzania, ingawa takwimu kamili za kitaifa ni chache, utafiti unaonyesha kuwa kiwango cha upofu kwa watoto ni takribani 0.17 kwa kila watoto 1,000, hali inayoakisi mwenendo wa nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Magonjwa ya macho duniani yameongezeka kwa kasi, watoto wapatao milioni 1.4 wanakabiliwa na ulemavu wa kutoona, zaidi ya asilimia 50 kati ya hao wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania”anasema Mkurugenzi wa huduma za uuguzi na ukunga Tanzania, Ziada Sellah.

Karne ya 21 na athari kwa afya

Katika karne ya 21, matumizi ya vifaa vya kidijitali kama simu, kompyuta na televisheni yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watoto.

Tofauti na zamani ambapo watoto walitulizwa kwa nyimbo na michezo ya asili, siku hizi mara nyingi hutulizwa kwa kupewa simu au kuangalia vipindi mbalimbali.

Aidha, tafiti kubwa zilizohusisha zaidi ya watoto 335,000 zimeongeza uzito wa hoja hii kwa kubainisha kuwa kila saa moja ya ziada ya matumizi ya skrini huongeza hatari ya kutoona vitu vya mbali (myopia) kwa takribani asilimia 21. Takwimu hizi zina uzito mkubwa na zinatoa ujumbe wa wazi kuhusu umuhimu wa kudhibiti matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto, hasa katika umri wa ukuaji wa macho na ubongo.

Wataalamu wa afya ya macho wanaeleza kuwa athari za vioo vya vifaa hivi kwa macho ya watoto hutokea kupitia njia kadhaa zinazohusiana. Kwanza, matumizi ya yake husababisha hali inayojulikana kama “near work”, ambapo macho hulazimika kutazama vitu vilivyo karibu kwa muda mrefu, kama vile simu au kompyuta.

Hali hii husababisha macho kuzoea kuona vitu vya karibu, na hatimaye hubadilika kimfumo, jambo linaloweza kusababisha mtoto kushindwa kuona vitu vya mbali kwa uwazi.

Pili, matumizi ya muda mrefu ya vioo hupunguza kwa kiasi kikubwa muda ambao watoto hutumia nje ya nyumba. Tafiti zinaonyesha kuwa mwanga wa asili wa jua una mchango muhimu katika ukuaji bora wa macho ya mtoto na husaidia kupunguza hatari ya myopia. Watoto wanaokaa ndani kwa muda mrefu bila kupata mwanga wa asili, huwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata matatizo ya kuona.

Tatu, matumizi ya vioo huathiri tabia ya kufumba macho (blinking). Kwa kawaida, mtoto mwenye afya hufumba macho kati ya mara 15 hadi 20 kwa dakika anapokuwa akicheza au kuzungumza. Hata hivyo, anapotumia skrini, kiwango hiki hupungua hadi mara tano hadi saba kwa dakika au hata chini zaidi.

Kupungua huku kwa kufumba macho husababisha macho kukosa unyevunyevu wa kutosha, hali inayoweza kusababisha ukavu wa macho, maumivu, kuwashwa, kuona kwa ukungu, na wakati mwingine maumivu ya kichwa yanayoendelea.

Athari kwa macho

Wataalamu wa afya ya macho wanaendelea kufafanua kuwa matumizi ya muda mrefu ya vioo huathiri macho ya watoto kwa namna mbalimbali.

Mosi, husababisha kile kinachoitwa “near work”, yaani kulenga vitu vilivyo karibu kwa muda mrefu. Hali hii huifanya macho kuzoea mazingira ya karibu na hatimaye mtoto hushindwa kuona vitu vya mbali kwa ufasaha.

Aderick Venance, mtaalamu wa afya ya macho Mkoa wa Tabora, anaeleza kuwa hata muundo wa macho ya mtoto unaweza kubadilika kutokana na matumizi hayo.

“Hali hii husababisha mabadiliko ya muundo wa jicho, ambapo jicho hujirekebisha kuona vitu vya karibu zaidi, na hatimaye mtoto hushindwa kuona vitu vya mbali vizuri,” anasema.

Pili, matumizi ya vifaa hupunguza muda wa watoto kukaa nje, jambo linalowanyima fursa ya kupata mwanga wa asili wa jua ambao una mchango mkubwa katika kulinda macho dhidi ya tatizo la kutoona mbali.

Tatu, hupunguza kiwango cha kufumba macho. Kwa kawaida mtoto hufumba macho kati ya mara 15 hadi 20 kwa dakika, lakini anapotumia vioo hivyo kiwango hiki hushuka hadi mara tano hadi Sana au hata chini ya hapo. Hali hii husababisha macho kukauka, maumivu ya macho, kuona kwa ukungu na hata maumivu ya kichwa.

Kwa kuzingatia hatari hizi, wataalamu wanatoa mapendekezo kuhusu matumizi sahihi kwa watoto kulingana na umri. Kwa watoto wachanga walio chini ya mwaka mmoja, matumizi hayapendekezwi kabisa, kwani ubongo wao unahitaji mwingiliano wa moja kwa moja na watu pamoja na mazingira.

Kwa watoto wa mwaka mmoja hadi mwili, matumizi ya yanapaswa kuwa machache sana na yafanyike chini ya uangalizi wa karibu, hasa kwa mawasiliano ya video.

Kwa watoto wa miaka miwili hadi minne muda usizidi saa moja kwa siku, na uwe wa maudhui yenye kujenga maarifa. Kwa watoto wa miaka mitano hadi 17, ingawa hakuna kikomo rasmi cha muda, inasisitizwa kuwepo kwa uwiano kati ya matumizi ya vifaa, shughuli za kimwili, usingizi na masomo.

Wazazi wafanye haya

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa skrini si mbaya kwa ujumla. Zinapotumiwa kwa usahihi, zinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujifunza na kukuza ujuzi wa mtoto.

Changamoto kubwa ipo katika matumizi kupita kiasi pamoja na ukosefu wa usimamizi sahihi.

Ili kulinda afya ya macho ya watoto, wazazi na walezi wanapaswa kuweka mipaka ya muda wa vifaa hivi, kuhakikisha watoto wanapata muda wa kucheza nje angalau saa moja hadi mbili kwa siku, na kuepuka matumizi yake kabla ya kulala.

Aidha, kuwafundisha watoto tabia bora za matumizi ya vifaa ni hatua muhimu katika kulinda afya yao ya macho na maendeleo yao kwa ujumla.

Moja ya mbinu rahisi na yenye ufanisi inayopendekezwa na wataalamu ni kanuni ya 20-20-20, ambapo baada ya kila dakika 20 za kutumia kifaa, mtoto anatakiwa kuacha kuangalia kifaa na kutazama kitu kilicho umbali wa takribani mita 20 kwa sekunde 20.

Zoezi hili husaidia kupumzisha misuli ya macho, kupunguza uchovu na kudumisha afya bora ya mfumo wa kuona kwa muda mrefu.

Ni muhimu pia kuwafundisha watoto umuhimu wa mkao sahihi wanapotumia vifaa vya kidijitali, kuhakikisha wanakaa kwa umbali unaofaa kutoka kwenye kill na kuepuka matumizi ya vifaa hivyo katika mazingira yenye mwanga hafifu au usiku wa manane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *