Katika ujumbe wake wa siku ya Kimataifa ya Vesak, ambayo huadhimishwa wakati wa mwezi mpevu mwezi Mei, ambayo ni siku takatifu kwa mamilioni ya Wabuddha duniani kote Guterres amesema kuwa mwaka huu maadhimisho hayo yanafanyika wakati ambapo dunia inakabiliwa na mivutano ya kisiasa, mgawanyiko na migogoro.

Amekumbuka mwaka 2023 ambapo alipata fursa ya kutembelea Lumbini, Nepal mahali alikozaliwa Buddha jambo lililomkumbusha kuwa suluhisho la changamoto za dunia ya sasa linaweza kupatikana katika mafundisho ya kudumu ya kutokutumia vurugu, huruma na kujitolea kwa ajili ya wengine.

“Kwa kuongozwa na mfano wa Buddha, na tuinue ubinadamu wetu wa pamoja na kujenga dunia yenye amani na endelevu ambayo watu wote wanaihitaji na kustahili. Heri ya Siku ya Vesak kwa wote,” amesema Guterres.

Kauli mbiu ya Vesak inaendana kwa karibu na misingi ya Umoja wa Mataifa, ambayo inalenga kudumisha amani na usalama wa kimataifa pamoja na kukuza maendeleo endelevu kwa wote.

Kuhusu siku ya Vesak

Siku ya Vesak, ni siku takatifu kwa mamilioni ya Wabuddha duniani kote. Inaadhimisha matukio matatu muhimu katika maisha ya Buddha kuzaliwa kwake mwaka 623 kabla ya Kristo, kupata mwanga, na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Mwaka 1999, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 54/115 kutambua rasmi Siku ya Vesak kimataifa. Hatua hiyo ililenga kuthamini mchango mkubwa wa Ubuddha mojawapo ya dini za kale zaidi duniani katika kuimarisha hali ya kiroho ya binadamu kwa zaidi ya miaka elfu mbili na nusu.

Kila mwaka, maadhimisho haya hufanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa na katika ofisi zake mbalimbali duniani, kwa kushirikiana na nchi wanachama na wadau wengine.

Mafundisho ya Buddha yanasisitiza huruma, amani na nia njema maadili ambayo yameendelea kugusa maisha ya mamilioni ya watu duniani. 

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Javier Pérez de Cuéllar, aliwahi kusema katika ujumbe wake mwaka 1986 kuwa maadhimisho ya Vesak ni fursa muhimu kwa Wabuddha kote duniani kusherehekea ujumbe wa huruma na kujitoa kwa ajili ya ubinadamu.

Alisisitiza kuwa ujumbe huo una umuhimu mkubwa zaidi katika dunia ya sasa, akibainisha kuwa amani, uelewano na mtazamo wa ubinadamu unaovuka mipaka ya kitaifa ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za dunia ya kisasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *