Akizungumza mjini Geneva Uswisi hii leo, msemaji wa UNHCR Carlotta Wolf amesema hali ya ukosefu wa usalama katika njia muhimu za Ghuba ya Uajemi, ikiwemo Mlango Bahari wa Hormuz, imevuruga usafiri wa meli na kuongeza gharama za kusafirisha bidhaa muhimu za kibinadamu.

“Mamilioni ya wakimbizi na watu waliofurushwa kutoka kwenye makazi yao wanakabiliwa na kuchelewa au kupunguzwa kwa misaada ya kuokoa maisha kutokana na ongezeko kubwa la gharama za usafirishaji na mafuta,” amesema Wolf.

© UNOCHA/Adedeji Ademigbuji Mwanamke ameketi na mtoto wake ndani ya makazi ya dharura ya muda huko Malakal, Sudan Kusini. (Picha ya maktaba)

Gharama za misaada Sudan na Chad zaongezeka mara mbili

UNHCR imesema baadhi ya gharama za kusafirisha misaada zimeongezeka zaidi ya mara mbili tangu kuanza kwa mapigano katika eneo hilo.

Shirika hilo limeeleza kuwa gharama za kupeleka vifaa vya misaada kutoka ghala lake la kimataifa mjini Dubai kwenda operesheni zake nchini Sudan na Chad zimepanda kutoka dola 927,000 hadi dola milioni 1.87.

Aidha, viwango vya usafirishaji kutoka nchi muhimu za ununuzi wa misaada vimeongezeka kwa karibu asilimia 18 tangu kuanza kwa mapigano, huku uwezo wa kampuni za usafirishaji duniani ukishuka kutoka asilimia 97 hadi 77 tangu mwanzo wa mwaka 2026.

Wolf amesema UNHCR imelazimika kubadili njia za usafirishaji kwa kutumia bandari mbadala kama Aqaba pamoja na kuongeza matumizi ya usafiri wa barabarani kupitia Rasi ya Arabia na Uturuki.

Afrika yaathirika zaidi kutokana na migogoro mingi

UNHCR imeeleza kuwa hali ni ya kutia wasiwasi zaidi barani Afrika ambako migogoro mingi ya wakimbizi inaendelea kwa wakati mmoja.

Nchini Kenya, ongezeko la bei ya mafuta kwa takribani asilimia 15 limepunguza upatikanaji wa malori na kuchelewesha usafirishaji wa misaada kwenda Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Sudan Kusini.

Katika Sudan, ambako vita sasa vinaingia mwaka wa nne, gharama za kupeleka misaada zimeongezeka maradufu katika miezi ya karibuni, huku meli zikilazimika kuzunguka Rasi ya Cape of Good Hope, jambo linaloongeza hadi siku 25 za kuchelewa kwa usafirishaji.

© UNHCR/Magnum Photos/Emin Ozme Watu nchini Lebanon wanafungua vifaa vya misaada vilivyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

UNHCR yajivunia mifumo ya dharura kuendelea kufanya kazi

Pamoja na changamoto hizo, UNHCR imesema bado imefanikiwa kuendelea kutoa misaada ya dharura kutokana na mtandao wake wa kimataifa wa maghala ya misaada na mifumo ya maandalizi ya haraka.

Shirika hilo lina maghala saba ya kimataifa katika miji ya Dubai, Termez, Copenhagen, Accra, Douala, Nairobi na Panama City, yenye uwezo wa kusaidia hadi watu milioni moja waliokimbia makazi yao wakati wowote.

Kwa mujibu wa UNHCR, tangu kuanza kwa mgogoro huo, shirika hilo pamoja na washirika wake wamefikisha misaada kwa zaidi ya watu 200,000 waliokimbia makazi yao nchini Lebanon, kwa kiasi kikubwa wakitumia vifaa vilivyokuwa tayari vimehifadhiwa.

“Msaada huu umewezeshwa pia na safari tatu za ndege za misaada zilizotolewa na Umoja wa Ulaya pamoja na nchi za Ufaransa, Ireland na Italia,” amesema Wolf.

Onyo kuhusu athari kubwa zaidi endapo mgogoro utaendelea

UNHCR imeonya kuwa iwapo hali ya ukosefu wa utulivu Mashariki ya Kati itaendelea, gharama za usafirishaji, ucheleweshaji wa mizigo na upungufu wa uwezo wa usafiri vitaendelea kudhoofisha operesheni za kibinadamu duniani.

Wolf amesema, “Iwapo usumbufu huu utaendelea kwa muda mrefu, uwezo wa misaada kuwafikia watu wanaohitaji kwa haraka na kwa kiwango kinachohitajika utaathirika vibaya, na hilo linaweza kuwa na madhara makubwa kwa mamilioni ya wakimbizi na watu waliolazimika kukimbia makazi yao duniani kote.”

OHCHR: Uhaba wa mafuta waathiri vibaya jamii maskini duniani

Kwa upende wake msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, (OHCHR), Jeremy Laurence, ameonya kuwa uhaba wa mafuta duniani uliochochewa na vita inayoendeea Mashariki ya Kati unaendelea kusababisha madhara makubwa ya kibinadamu, hasa kwa jamii maskini na zilizo katika mazingira hatarishi.

Akizungumza kuhusu athari za kupungua kwa upatikanaji wa mafuta, Laurence amesema wakulima wadogo katika nchi za Afrika, Asia na Amerika Kusini wanashindwa kuendesha mashine zao za kilimo kutokana na ukosefu wa mafuta.

“Mkulima mdogo barani Afrika au Asia au Amerika Kusini hawezi kuendesha mashine zake kwenye kipande chake kidogo cha ardhi kinachotegemewa kuhudumia familia yake kubwa,” amesema Laurence.

© Unsplash/Zach Theo Kiwanda cha mafuta cha ufukweni iko pwani katika maji ya wazi.

Shule, hospitali na huduma muhimu zaporomoka

Kwa mujibu wa OHCHR, athari hizo zinaenda mbali zaidi ya sekta ya kilimo, huku jenereta zinazotumia dizeli zikisimama kufanya kazi na kusababisha huduma muhimu kuvurugika.

Laurence amesema mabasi ya shule pia hayawezi kufanya kazi kutokana na uhaba wa mafuta, hali inayowanyima watoto haki yao ya kupata elimu.

“Jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli haziwezi tena kufanya kazi, huku mabasi ya shule yakishindwa kuendelea na safari zake na watoto kunyimwa elimu,” amesema.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara UNCTAD limeandaa dashibidi ya kufuatilia athari za kimataifa za usafirishaji wa bahari za nishati, chakula, za kiuchumi na ufadhili fuatilia hapa

Maskini waathirika wa kwanza

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imeonya kuwa jamii maskini ndizo zinazoathirika kwanza kila mara kunapotokea mizozo ya kiuchumi au usumbufu wa usambazaji wa mafuta duniani.

“Inaathiri kwanza wale walio katika mazingira magumu zaidi,” amesema Laurence, akisisitiza umuhimu wa hatua za haraka za kimataifa kulinda maisha na haki za msingi za watu walio hatarini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *