
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu madai ya Marekani kwamba iliingia vitani na Iran kwa ajili ya “kujilinda,” akisisitiza kuwa: Hakukuwa na hatua yoyote ya kijeshi kutoka upande wa Iran dhidi ya Marekani, na kwa hivyo shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Iran lilikuwa kitendo cha uchokozi.
Ismail Baqaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X akijibu ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwamba nchi hiyo iliingia vitani na Iran katika hali ya “kujilinda” akisema: “Kujilinda” dhidi ya nini?! Je, kulikuwa na “shambulio la silaha” la Iran ambalo lilihalalisha “kujilinda” huko? La hasha! Kwa hivyo, shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Iran halikuwa “kujilinda” – bali kitendo cha uchokozi dhidi ya taifa la Iran.
Katika siku za hivi karibuni, maafisa wa serikali ya Marekani, wametoa madai kuhusu sababu za kuanzisha vita na Iran, wakijaribu kuhalalisha vitavya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa madai kuwa ni hatua ya “kujilinda”.
Waziri wa Vita wa Marekani pia alidai kwamba uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran ulichochewa na nia ya kukabiliana na mipango ya nyuklia ya Tehran. Madai haya yametajwa kuwa hayana msingi wowote katika sheria za kimataifa na yanatumiwa kuhalalisha uchokozi na mashambulio ya kijeshi dhidi ya watu wa Iran.