
Tabora. Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tabora kimepitisha majina ya wagombea udiwani watakaokiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika kufuatia vifo vya madiwani wawili wa kata mkoani humo.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi uliopo Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Manispaa ya Tabora.
Akizungumza leo Mei 2, 2026, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba, amemtaja Termistoles Nobert kuwa mgombea wa udiwani katika Kata ya Ziba wilayani Igunga, huku Michael Kaswiza akiteuliwa kugombea katika Kata ya Itilo wilayani Nzega.
Nkumba amesema wagombea hao wamechaguliwa kwa kuzingatia sifa mbalimbali zikiwemo ukaribu wao na chama pamoja na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
“Tayari chama kimetimiza wajibu wake, kinachosubiriwa sasa ni Tume kutoa mwongozo wa michakato mingine hadi uchaguzi utakapokamilika,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa umoja ndani ya chama hicho, akiwataka wanachama kuachana na makundi na kuunga mkono wagombea walioteuliwa.
“Hawa si wagombea wa kura za maoni tena, bali ni wagombea wa CCM, hivyo kila mmoja anapaswa kushirikiana kuhakikisha ushindi,” amesema.
Aidha, ameonya wanachama watakaovujisha siri za vikao au kuchochea migogoro mitaani kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Kuhusu uimarishaji wa chama, Nkumba amesema makatibu wa uenezi katika kata wamepewa pikipiki ili kurahisisha kazi ya kukisemea chama na kuimarisha matawi na mashina.
“Pikipiki hizi si mapambo, ziletwe tija kwa kufanya kazi na kuhakikisha vikao vinafanyika kwa wakati kulingana na kalenda ya chama,” amesisitiza.
Pia alihimiza wanachama kulipa ada kwa wakati ili kukiwezesha chama kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka mkoa huo, Mohamed Nassoro, amesisitiza kuwa umoja ni nguzo muhimu katika kuhakikisha chama kinapata ushindi kwenye uchaguzi huo wa marudio.
“Tushirikiane sote, matunda ya ushirikiano ni mazuri kwa kila mmoja,” amesema.
Katika kikao hicho, tuzo za utendaji bora zilitolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba, kwa mchango wao katika kuimarisha chama.