Dar es Salaam. Jukwaa la AfroExchange Aprili 30,2026 liliwakutanisha wadau mbalimbali wa tasnia ya muziki jijini Dar es Salaam, katika mjadala uliolenga kutafuta njia za kuufikisha muziki wa Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.
Mjadala huo uliwakutanisha wasanii, watayarishaji wa muziki, DJs na wadau wengine wa sekta ya burudani. Kujadili nafasi ya Tanzania katika ramani ya muziki wa kimataifa.
Katika hatua ya kwanza ya majadiliano hayo, nafasi ya DJs iliwekwa mbele, ikitambuliwa kama moja ya nguzo muhimu katika kueneza muziki. Kuunganisha masoko na kuifikisha sauti ya Afrika kwa watu wengi zaidi duniani.
Baadhi ya hoja zilizojadiliwa ni umuhimu wa ushirikiano ndani ya tasnia, matumizi ya majukwaa ya kimataifa pamoja na nafasi ya DJs katika kusambaza muziki kwenye masoko mbalimbali.
Mbali na majadiliano, AfroExchange pia ilitangaza hatua za utekelezaji wa baadhi ya mawazo yaliyoibuliwa. Kupitia mpango huo, baadhi ya DJs wa Tanzania watapata ufadhili wa kushiriki katika tukio la DJ Consequence litakalofanyika nchini Nigeria, hatua inayolenga kuwapa fursa ya kupata uzoefu wa kimataifa.