Dar es Salaam. Beatrice Morris. Kwa mabishoo na pisi kali za kipindi hiki, ngumu kulijua. Na ‘wainjilisti’ kama siyo ‘maustaadh’ wa kipindi kile pia ni ngumu kumjua mmliki wa jina hili. Lakini nikitaja jina la Nina ni 7 kwa 10 wanalijua.
Nina? Yes, Nina. Katika nyakati za utawala wa Mkapa. Alikuwa ni sehemu ya viumbe uzao wa Eva, waliovuruga akili za vijana hata washua kibao mjini. Alikamilika kwa sura, umbile, rangi, sauti na hasa macho.
Alama rahisi ya kumtambua Nina ilikuwa macho. Wote wangeigiza kama yeye, kuongea kama yeye na umaarufu kama yeye. Lakini likija suala la macho mazuri kwa maana ya uzuri. Nina alikuwa na dunia yake. Acha kabisa.
Kaole ilikuwa na wasanii wa kike wengi wazuri. Lakini walizidiwa uzuri na macho mazuri ya Nina. Kaole ilikuwa na maigizo mazuri sana, lakini macho yaliongeza ubora wa maigizo yao. Ni ngumu kufafanua zaidi.
Unachopaswa kujua ni kuwa kwa dunia ya sasa hakuna muigizaji au mwanamuziki mwenye macho mazuri kama ya Nina. Nina kama akikutazama kwa zaidi ya dakika tatu lazima upate degedege ama kizungu zungu. Alimiliki macho ya ajabu.
Wengi walimkwepa kuigiza naye wakiogopa kumtazama. Alikuwa na macho elekezi, macho agizo, macho kilainishi. Macho ambayo yangefanya Jaji Othman Chande ashindwe kuwasilisha taarifa ya ile Tume yake. Macho tatanishi.
Macho sampuli ile, ndiyo macho yaliyomtazama Samson usoni. Akashindwa kuvunga mbele ya Delila na kutoa boko kibwege. Ni wazi kwamba maigizo ya Kaole Sanaa Group yalivutia wengi. Na macho ya Nina yalivutia wengi.
Beatrice Morris a.k.a Nina. Kama utani akatoweka kwenye ramani ya sanaa na wasanii. Sebule za watu zilikosa msisimko katika runinga zao. Magazeti ya udaku yakakosa stori na sura ya mauzo. Nina alijiweka kando na sanaa.
Akaamua kuishi maisha yake na kutemana na michorano. Mapipa akatoweka, Kino akaisusa, Keko akapakataa. Tukaanza ‘kummisi’ taratibu, mwisho tukamuondoa akilini na kukubaliana na ukweli. Sanaa ikapoteza kiumbe pendwa rasmi.
Kuuliza. Tukaambiwa kuwa kuna mwamba hajataka ujinga wetu wa kumfanya Nina kivutio kama kivutio cha utalii. Yeye kaamua kuweka ndani jumla jumla bila chenji. Macho ayaone peke yake wakiwa ndani kwao. Aliolewa.
Kuna walioolewa na kuendelea na sanaa. Yeye alipoolewa tu na sanaa akatemana nayo jumla. Ni wazi kwamba aliithamini ndoa na mumewe kuliko sisi waja. Mwaka wa 20 na upuuzi toka atemane na uigizaji na kuishi maisha bora ya ndoani.
Akatuachia Sinta, Nora, Mainda, Mona, Lulu na wengineo. Sanaa ilipoteza siyo tu kipaji bora bali kivutio bora cha sanaa yenyewe. Huwezi kumuona kwenye mishe za wasanii na sanaa hata kwa bahati mbaya. Nina yupo lakini sanaa kwake haipo.
Nina alitupiga talaka ya uigizaji akiwa msichana mdogo. Alitaka tu kukaa mbali na maisha yote ya sanaa na kutulia kifamilia zaidi. Nina alituacha akiwa katika kilele chake cha ubora, jina lake likiwa kubwa, akipendwa na kumiliki mashabiki wengi sana.
Tofauti na Nina kuna waliotupiga talaka za vifo wakiwa bado na umri mdogo. Wakasepa machoni na mitaani kwetu. Hivi leo tukilia kwa kuondokewa na Spack, ndo vilevile tukalia kwa kuondokewa na Ngwair, Kanumba, Langa, Shalomilionea na wengineo.
Spack kaondoka na miaka 41 tu. Kanumba 28, Ngwair 32, Langa, Sajuki, Shalomiolea, Mez B, Steve 2K, YP ndo umri huohuo. Kuna Mandojo, Maunda, Complex na Vivie. Wanasanaa hawa wote waliondoka na umri mdogo.
Ukisikia Mbaraka Mwishehe, unapata picha ya mtu wa aina gani? Vipi na Marijani Fajabu? Bila shaka unapata taswira ya watu wazima, wazee waliondoka duniani kwa wakati sahihi ama kwa makusudi. Ndicho kilichopo kwa wengi.
Nyimbo kama Mtaa wa Saba wa Mabaraka, au Mayasa kama siyo Mwanameka ama Marijani. Kwa uwazi kabisa huwezi kuamini ziliimbwa na vijana wa miaka 20 mpaka 30. Kutokana na namna zilivyo unajijengea picha ya watu wazima.
Mbaraka Mwishehe alifariki na miaka 35 tu. Alifanya mengi sana akiwa na umri mdogo. Dunia hii aliizunguka kwa muziki tu, ndivyo ilivyo kwa Marijani Rajabu, naye alifariki dunia akiwa na miaka 40 pekee. Walikuwa vijana wadogo wakiwa bado wanahitajika.
Leo tunalia kwa kuondokewa na Seleman Ramadhan Mvamba ‘Spack’. Wazee wetu wakiwa nao ni vijana wadogo waliumizwa na kulizwa na vifo vya wanamuziki vijana kama Mbaraka Mwishehe na Marijani Rajabu. Siyo kilio cha leo kipo muda mrefu.
Wasanii wengi wametutoka katika umri mdogo. Mbali na kuacha kazi zao, pia huacha na familia ama watoto wadogo. Wanapoondoka tusiishie kulia na kuzika tu, tutafakari tukitazama kile walichoacha mbali ya kazi zao za sanaa. Tujitafakari!