Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijiandaa kuanza utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 unaoweka teknolojia, ubunifu na uchumi wa kidigitali kama msingi wa taifa la baadaye, dalili za mafanikio ya matumizi ya teknolojia tayari zimeanza kuonekana katika huduma muhimu za jamii.
Tofauti na miongo iliyopita ambapo mifumo ya karatasi ilisababisha ucheleweshaji wa huduma na kuwanyima wakulima pamoja na jamii za vijijini taarifa muhimu kwa wakati, sasa mifumo ya kidigitali imeanza kuunganisha jamii na kupunguza pengo kati ya vijijini na mijini.
Akizungumzia mwelekeo huo mpya, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na China umegeuka chachu ya mabadiliko hayo ya kidigitali.
Kairuki alitoa kauli hiyo Ijumaa, Mei 1, 2026, katika ukumbi wa Kituo cha East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC), Ubungo, alipotembelea maonyesho ya Teknolojia za juu za China.
Waziri Kairuki alisisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na China umevuka diplomasia ya kawaida na sasa unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi kupitia teknolojia.
“Uhusiano wetu na China umebadilika sana na kuwa chachu ya mapinduzi ya kidigitali nchini, hatua inayochochea fursa za ajira na ujasiriamali kwa vijana,” amesema.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, akizungumza katika Warsha ya Maonesho ya Teknolojia za China jijini Dar es Salaam, Ijumaa Mei 1, 2026.
Amefafanua kuwa ujio wa teknolojia za kisasa, ikiwemo akili unde (AI), nishati safi ya jua na mifumo ya Tehama, umeanza kutoa majibu kwa changamoto za muda mrefu katika sekta muhimu.
Katika sekta ya kilimo, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitegemea mbinu za jadi, amesema teknolojia hizo zimewawezesha wakulima kupata taarifa sahihi za uzalishaji na masoko kwa wakati, pamoja na kutumia zana za kisasa zinazoongeza tija na kipato.
Kwa upande wa huduma za kifedha, mifumo ya kidigitali imepanua upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi, hususan vijijini na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na kufungua fursa mpya kwa wajasiriamali.
Aidha, sekta ya elimu imeanza kunufaika kupitia matumizi ya Tehama, ambapo huduma za elimu mtandaoni zinapunguza pengo la maarifa kati ya mijini na vijijini.
Akizungumzia hatua za mbele, Kairuki amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa kuwakaribisha wawekezaji wa China kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa kidigitali wa Tanzania.
“Ninawaalika wajasiriamali wa China kuja kuwekeza nchini kwetu ili kuchochea maendeleo ya pamoja katika uchumi wa kidigitali,” amesema.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema nchi yake inaendelea kuwa kinara wa ubunifu wa teknolojia duniani, hususan katika eneo la akili unde.
“China iko mstari wa mbele katika ubunifu na matumizi ya teknolojia ya AI duniani, hatua inayochochea maendeleo ya huduma za kidigitali Tanzania na kwingineko,” amesema.
Ameeleza kuwa kwa Tanzania, teknolojia hizo zimechangia kuboresha mifumo ya Serikali, ikiwemo utoaji wa huduma mtandaoni, usajili wa vitambulisho vya taifa, mifumo ya utoaji taarifa na huduma za kijamii.
Aidha, amesema mchango wa China katika nishati safi umeongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo muhimu kama hospitali na shule.
“Ushirikiano huu pia unaenda sambamba na ujenzi wa uwezo kwa Watanzania kupitia mafunzo na ufadhili wa masomo, ili kuhakikisha teknolojia hizi zinakuza ujuzi kwa vijana,” ameongeza.