Mbeya. Wakati Serikali ikiendelea kuyatambua na kuyapa kipaumbele makundi mbalimbali ya kijamii katika nyanja za kiuchumi na kijamii, kundi la wahudumu wa nyumba za kulala wageni limeendelea kubaki pembezoni, huku likikabiliwa na changamoto nyingi zinazohatarisha afya, usalama na ustawi wao kwa ujumla.

Makundi kama mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wadogo yamekuwa yakitajwa mara kwa mara katika mipango ya uwezeshaji, lakini wahudumu wa nyumba hizo, ambao ni sehemu muhimu ya sekta ya huduma, wanaonekana kusahaulika licha ya mchango wao mkubwa katika kuhudumia maelfu ya watu wanaotumia huduma za malazi kila siku.

Nyumba za kulala wageni zimekuwa sehemu ya muhimu kwa watu wa kada mbalimbali wakiwamo viongozi, wafanyabiashara, watumishi wa umma na wananchi wa kawaida. Watu hao hutegemea maeneo hayo kwa mapumziko, starehe au shughuli nyingine binafsi.

Nyuma ya pazia la huduma hizo, kuna kundi la wafanyakazi wanaofanya kazi katika mazingira magumu, wakihakikisha kila kitu kinakuwa safi na salama kwa wateja, huku wao wenyewe wakibeba hatari kubwa kiafya.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Mkoa wa Mbeya umebaini kuwa wahudumu hao, wengi wao wakiwa wanawake na wasichana, wanakabiliwa na ukosefu wa mikataba rasmi ya ajira, wanapata malipo duni, wana mazingira hatarishi ya kazi pamoja na vishawishi vya kingono vinavyoweza kuhatarisha afya zao, ikiwamo hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wahudumu katika ‘loji’ moja jijini Mbeya, Riziki Daniel anasema mazingira ya kazi yao ni magumu na hayazingatii usalama wa afya za wafanyakazi.

Anasema licha ya kazi wanazofanya kuwa nzito na za hatari, hawapati vifaa kinga wala teknolojia ya kisasa inayoweza kurahisisha kazi hiyo.

“Tunafanya kazi nyingi kwa mikono. Mashuka na nguo za wateja tunafua wenyewe bila mashine. Wakati mwingine unakuta zimechafuka sana, lakini huna namna, lazima ufanye kazi,” anasema.

Riziki anaeleza kuwa changamoto kubwa zaidi ni kushughulika na uchafu hatarishi, ikiwamo damu za hedhi au majimaji mengine ya mwili, hali inayowaweka katika hatari ya kupata maambukizi.

“Kuna wateja wanaacha vyumba katika hali mbaya sana. Unakuta kuna damu za hedhi zimeachwa wazi, na sisi tunalazimika kufua kwa mikono. Kama una jeraha mkononi, ni rahisi sana kuambukizwa magonjwa,” anasema.

Anaongeza kuwa katika baadhi ya nyumba za wageni, hakuna hata glovu wala vifaa vingine vya kujikinga, hali inayowalazimu kufanya kazi bila kinga yoyote.

“Wengine hatuna hata glovu. Unafanya kazi kwa mikono mitupu. Ukipata maambukizi, hakuna anayejali,” anasema.

Mbali na hatari ya maambukizi, Riziki anasema kazi hiyo imemletea matatizo ya kiafya, ikiwamo maumivu makali ya mgongo kutokana na kubeba mizigo na kufanya kazi nzito kwa muda mrefu bila msaada wa vifaa vya kisasa.

“Kwa sasa siwezi kusafiri bila kuwa na mto wangu maalumu kwa sababu ya maumivu ya mgongo. Hii kazi imeathiri afya yangu,” anasema.

Vishawishi na hatari

Mbali na mazingira hatarishi ya kazi, wahudumu hao pia wanakumbana na vishawishi kutoka kwa baadhi ya wateja, hali inayoweza kuhatarisha afya na usalama wao.

Mhudumu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema baadhi ya wateja, hasa wanaume, hujaribu kuwashawishi wahudumu hao kuingia katika mahusiano ya kimwili kwa malipo.

“Mteja anaweza kukuambia akulipe Sh30,000 ili ulale naye. Kwa mtu mwenye matatizo ya kifedha, ni vigumu kukataa,” anasema.

Anaeleza kuwa licha ya baadhi ya wahudumu kujitambua na kukataa vishawishi hivyo, ugumu wa maisha huwafanya wengine kushindwa kujizuia.

“Hii inawaweka wengi katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza. Ni changamoto kubwa sana,” anasema.

Aidha, anabainisha kuwa kazi hiyo imekuwa ikitazamwa kwa mtazamo hasi katika jamii, hali inayowafanya baadhi ya wahudumu kuficha kazi zao hata kwa familia zao.

“Wengi wetu hatuwaambii ndugu zetu kazi tunazofanya. Wanajua mazingira si salama, lakini tunalazimika kuzifanya kwa sababu ya maisha,” anasema.

Mikataba na malipo duni

Changamoto nyingine kubwa inayowakabili wahudumu hao ni ukosefu wa mikataba rasmi ya ajira, hali inayowanyima haki zao za msingi kama wafanyakazi.

Huruma Mbezi, mhudumu katika ‘loji’ iliyopo mtaa wa Isanga jijini Mbeya, anasema kwa zaidi ya miaka 18 aliyofanya kazi hiyo, hajawahi kupewa mkataba wa maandishi.

“Tunafanya kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Hakuna mkataba. Hii inafanya iwe rahisi kunyimwa haki zako bila hatua zozote kuchukuliwa,” anasema.

Anasimulia kuwa aliwahi kufanya kazi katika nyumba nyingine ambapo hakulipwa mshahara kwa miezi saba, lakini hakuweza kudai haki yake kutokana na kukosa mkataba.

“Niliondoka bila kulipwa kwa sababu sikuwa na ushahidi wa ajira. Hii ni changamoto kubwa sana kwetu,” anasema.

Huruma anaongeza kuwa malipo wanayopata ni kidogo sana, yakianzia Sh60,000 hadi Sh100,000 kwa mwezi, kiwango ambacho hakikidhi mahitaji ya maisha ya kila siku.

“Tunafanya kazi hizi kwa sababu hatuna chaguo. Wengine hatuna elimu, na hata wenye elimu hawapati kazi. Tunaishia hapa ili kujikimu,” anasema.

Kuhusu changamoto zao kazini, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mlezi Foundation, George Mackona amesema ni wakati mwafaka kwa jamii na Serikali kulitambua kundi hilo na kulipatia msaada unaostahili.

“Tumeliona kundi hili sasa na tutalifanyia kazi. Tutahakikisha wanapata elimu ya kujikinga na tunahamasisha kuanzishwa kwa umoja wao,” anasema.

Anaongeza kuwa umoja huo utawasaidia kudai haki zao na kuboresha mazingira yao ya kazi.

Wamiliki wazungumza

Baadhi ya wamiliki wa nyumba za kulala wageni wamekiri kuwepo kwa changamoto hizo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi.

Timoth Yohana, mmiliki wa nyumba moja jijini Mbeya, anasema anajitahidi kuwajali wafanyakazi wake licha ya kutokuwa na mfumo rasmi wa mikataba.

“Natoa posho ya chakula na fedha ya chai kila siku, pamoja na mshahara wa mwezi. Pia nikiona mfanyakazi ana shida, namsaidia,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kuwa bado kuna haja ya kuboresha zaidi mazingira ya kazi ili kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.

“Tunapaswa kuweka mbele ubinadamu. Afya ya mfanyakazi ni muhimu kuliko faida,” anasisitiza.

Kwa upande wake, Jason Temba anasema waajiri wanaokiuka haki za wafanyakazi wanapaswa kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

“Kila kazi ina sheria zake. Waajiri wanapaswa kuzifuata ili kulinda haki za wafanyakazi,” anasema.

Kauli ya Serikali

Kaimu Meneja wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Danford Kafumu amesema mamlaka hiyo inaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo ya kazi ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi.

“Tunabaini maeneo yasiyokidhi vigezo na kuchukua hatua, ikiwamo kutoa faini au kufunga biashara. Lakini pia tunatoa elimu kwa waajiri,” anasema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeti Nyema amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha wahudumu hao wanapatiwa elimu ya afya na vifaa kinga.

“Tutashirikiana na mamlaka nyingine kuwafikia na kuwapa elimu pamoja na kuboresha mazingira yao ya kazi,” anasema.

Anaongeza kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa umoja miongoni mwa wahudumu hao, hali inayowafanya kushindwa kuibua matatizo yao kwa uwazi.

“Tunalifanyia kazi suala hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanapata msaada unaostahili,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *