
Katika miaka ya hivi karibuni, dhana ya elimu ya mapenzi imekuwa ikitajwa sana katika magazeti, mitandao ya kijamii na mijadala ya kifamilia.
Wengi wameanza kuamini kuwa matatizo ya uhusiano na ndoa yanatokana na kukosa elimu sahihi ya mapenzi.
Hata hivyo, kadiri dhana hii inavyoenea, ndivyo inavyozidi kuwachenga wengi. Badala ya kuwa chombo cha kuwaweka watu huru kihisia, mara nyingi elimu ya mapenzi imegeuka kuwa mzigo wa matarajio, masharti na nadharia zinazokinzana na uhalisia wa maisha.
Elimu ya mapenzi, kwa mtazamo wa wengi, imejengwa juu ya vitabu, semina na kauli za wataalamu wanaoeleza jinsi ya kupenda kwa “usahihi”.
Tatizo linakuja pale elimu hii inapochukuliwa kama kanuni zisizobadilika, badala ya mwongozo unaopaswa kubadilishwa kulingana na mazingira, utu na tofauti za watu.
Watu wengi wamejikuta wakihukumu
uhusiano wao kwa misingi ya walichosoma au kusikia, badala ya kile wanachoishi.
Hapo ndipo elimu ya mapenzi inaanza kuwachenga, kwa kuwafanya waamini kuwa kuna fomula kamili ya mapenzi ambayo ikifuatwa, matatizo hayatakuwapo.
Mapenzi si darasa la nadharia pekee. Ni uzoefu hai unaohusisha hisia, makosa, maumivu na kujifunza kwa vitendo. Elimu ya mapenzi inapokosa kuzingatia upande huu wa kibinadamu, hujenga picha ya uongo inayowaacha wengi wakiwa wamechanganyikiwa na kukata tamaa wanapokutana na uhalisia usioendana na walichofundishwa.
Onyo kuhusu elimu ya mapenzi
Mwanafalsafa na mwanasaikolojia, Erich Fromm, katika kitabu chake: The Art of Loving, alionya mapema kuhusu hatari ya kuifanya elimu ya mapenzi kuwa nadharia tupu.
Anaandika: “Tatizo kuu la mapenzi si kupendwa, bali ni kupenda.” Fromm hakupinga elimu ya mapenzi, bali alipinga elimu inayomfanya mtu ajikite katika kupokea badala ya kutoa.
Kwa maoni yake, wengi wanachengwa kwa kufundishwa jinsi ya kutafutwa, kuthaminiwa na kupendwa, bila kufundishwa wajibu wa kupenda wengine kwa dhati.
Fromm pia anaongeza kuwa watu wengi wanachukulia mapenzi kama bidhaa sokoni, wakiamini kuwa elimu ya mapenzi itawapa mbinu za kupata “mchumba bora”.
Mtazamo huu huacha nje ukweli kwamba mapenzi ni kazi inayoendelea, si zawadi inayopatikana kwa kutumia mbinu sahihi pekee.
Elimu inaposhindwa kusisitiza hili, huwafanya wengi waamini kuwa tatizo likitokea, basi ama hawakujifunza vya kutosha au wamechagua mtu asiye sahihi.
Mwandishi mwingine aliyegusia kwa kina mtego wa maarifa ya mapenzi ni Alain de Botton. Katika kitabu chake The Course of Love, anaandika: “Hatujifunzi jinsi ya kupenda, na hivyo tunatarajia mapenzi yatukomboe.”
Anaeleza kuwa kile kinachoitwa elimu ya mapenzi mara nyingi ni mkusanyiko wa ndoto na matarajio makubwa, si mafunzo ya kukabiliana na changamoto halisi. Watu wanapokutana na migogoro ya kawaida, hushangaa na kuamini mapenzi yao yamekufa, kumbe walichokosa si hisia bali uelewa wa uhalisia.
Kwa mtazamo wa de Botton, elimu ya mapenzi inawachenga wengi kwa kuwafanya waamini kuwa mapenzi ya kweli hayapaswi kuwa na maumivu, migongano au kuchoka.
Anapinga wazo hilo kwa kusisitiza kuwa mapenzi ya kudumu ni yale yanayokubali dosari na udhaifu wa mwanadamu. Elimu isipoelekeza upande huu, hujenga kizazi kinachokimbia uhusiano pindi tu changamoto zinapojitokeza.
Paulo Coelho naye, katika maandishi yake ya kifalsafa, amegusia mara kadhaa hatari ya kujaribu kufunga mapenzi katika mafundisho magumu. Katika Eleven Minutes, anaandika: “Mapenzi hayapatikani kwa mtu mwingine, bali ndani yetu wenyewe.” Kauli hii inapochunguzwa kwa makini, inaonesha kuwa elimu ya mapenzi inayowafundisha watu kutegemea wengine kwa furaha yao, inawachenga. Badala ya kuwajenga ndani, elimu hiyo huwapeleka nje, wakitafuta majibu kwa wenzi wao.
Coelho anaashiria kuwa mapenzi hayawezi kufundishwa kikamilifu darasani au kwenye vitabu. Kuna sehemu ya mapenzi ambayo ni ya ndani, ya kujitambua na kukubali udhaifu binafsi.
Elimu inapopuuzia safari hii ya ndani, huacha watu wakiwa wamejaa nadharia lakini wakiwa watupu kihisia.
Kwa upande wake, Chimamanda Ngozi Adichie katika hotuba na maandiko yake kuhusu uhusiano na ndoa, amekuwa akionya dhidi ya simulizi moja ya mapenzi.
Ingawa hakuiita moja kwa moja elimu ya mapenzi, katika kitabu; We Should All Be Feminists anadokeza kuwa jamii huwafundisha watu mapenzi kwa njia potofu.
Kauli yake: “Tunawafundisha wasichana wajipunguze, wajifanye wadogo.” kwake elimu hii ya kijamii ya mapenzi huwafanya wengi kuingia kwenye uhusiano wakiwa wamepoteza sauti na utu wao, wakiamini hivyo ndivyo kupenda kunavyotakiwa kuwa.
Kwa kuunganisha mawazo ya waandishi hawa, inabainika kuwa elimu ya mapenzi, inapokosa mizani, hugeuka mtego. Badala ya kuwaelimisha watu kupenda kwa uhalisia, huwafundisha kuigiza mapenzi kwa misingi ya nadharia na matarajio yasiyotekelezeka.
Nini kifanyike?
Katika uhalisia wa maisha ya leo, changamoto si kukosa elimu ya mapenzi, bali ni aina ya elimu tunayopokea.
Wengi wanahoji kama kweli tunahitaji “elimu zaidi” au tunahitaji elimu sahihi. Elimu ya mapenzi inayowachenga wengi ni ile inayotafuta majibu rahisi kwa maswali magumu ya maisha ya kihisia.
Elimu sahihi ya mapenzi inapaswa kuanza kwa kukubali kuwa mapenzi hayana njia moja.
Kila uhusiano una lugha yake, historia yake na maumivu yake. Pale elimu inapoweka viwango vya jumla, watu wanaoishi chini ya viwango hivyo hujiona wameshindwa.
Hapo ndipo kuvunjika kwa uhusiano kunapoanza, si kwa sababu ya kukosa mapenzi, bali kwa sababu ya mzigo wa elimu isiyoendana na uhalisia.
Uzoefu unaonesha kizazi cha sasa kina taarifa nyingi lakini hekima ndogo. Watu wanajua maneno mengi ya mapenzi, lakini hawajui kuyatenda.
Wanajua nukuu nyingi, lakini hawajui kuvumilia. Elimu ya mapenzi imewapa lugha, lakini haijawapa moyo wa kustahimili misukosuko ya uhusiano ya kweli.
Mapenzi hayaishi kwenye vitabu pekee, bali yanaishi kwenye uamuzi wa kila siku wa watu wasio wakamilifu wanaojaribu kuishi pamoja.
Elimu ya mapenzi itakapokubali ukweli huu, itaacha kuwachenga wengi na kuanza kuwajenga kwa uhalisia.