Dar es Salaam. Mkali wa Afrobeats kutoka Nigeria, David Adedeji Adeleke maarufu Davido amejizolea umaarufu Afrika kutokana na nyimbo zake nzuri, mtindo wake wa maisha akiwa kama mtoto wa kishua na uhusiano wake na Chioma Ikokwu unaendelea kulipaisha jina lake.
Davido, mkali wa kibao cha Fall (2017), uhusiano hadi ndoa na Chioma ni upande mwingine wa maisha yake ambao umekuwa ukiangaziwa sana na vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
Mbali na familia, Chioma amekuwa bega kwa bega na Davido katika kazi yake ya muziki akiambatana naye katika matukio mbalimbali makubwa kama shoo na hata kushiriki kwenye video za nyimbo zake hatua ambayo pia huwa na matokeo mazuri.
Chioma alikuwepo Qatar wakati Davido alipopata nafasi ya kutumbuiza katika michuano ya Kombe la Dunia 2022, na hivi karibuni alikuwa Marekani ambapo mwanamuziki huyo alitumbuiza katika tamasha kubwa na maarufu la Coachella 2026.
Vilevile, Chioma alionekana katika video ya wimbo wa Davido Assurance (2018), ambayo hadi kufikia sasa imeshatazamwa (views) YouTube zaidi ya mara milioni 111, ikiwa ni video ya sita ya staa huyo kupata namba kubwa katika mtandao huo.
Akizungumza na shoo ya The Breakfast Club, Oktoba 2025, Davido alisema mkewe nyakati zote amekuwa akimuunga mkono tangu walipokuwa vijana wadogo, na hilo limetengeneza jambo la kipekee kwake.
“Kwa kila mara ninapogombana au kutofautiana naye, basi kuna kitu kibaya kitatokea katika biashara yangu ya muziki.”
“Huwa anasema, ‘unapigana na mimi wakati una mpango wa kutoa albamu?, acha tuone!’. Hivyo ana hiyo neema juu yangu,” alisema Davido.
Akikumbushia kuhusu uhusiano wao wa muda mrefu, Davido alifichua kwamba walikutana wakiwa chuo, wakati huo wakiwa na umri wa kati ya miaka 18 na 17, hivyo wamekuwa pamoja kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Ukaribu wao ulibadilika kutoka urafiki hadi kuwa uhusiano wa kimapenzi, na sasa ndoa, huku akigusia jinsi ambavyo Chioma amekuwa akiishi na watoto wake aliowapata katika uhusiano mwingine.
“Watoto wangu wanampenda sana Chioma, hasa binti yangu Hailey. Kuna nyakati niliogopa kuwaleta watoto wangu wakae karibu naye, lakini amekuwa akiishi nao vizuri tu,” alisema Davido aliyetikisa zaidi na wimbo wake If (2017).
Alipoulizwa iwapo kama ana michepuko nje ya ndoa yake, Davido alisema hataki matatizo kwani ameamua kutomsaliti mkewe na hana mpango wa kuoa mke mwingine kama ulivyo utamaduni wa wanaume wengi Nigeria hasa wale wanaojiweza kiuchumi.
Wiki hii, wakati akimtakia Chioma heri ya kuzaliwa, Davido alimtaja kama chanzo cha nguvu huku akishukuru uwepo wake katika maisha yake.
“Heri ya siku yako ya kuzaliwa, mpenzi wangu, amani yangu, nyumba yangu. Umebadilisha kila kitu kwangu. Napenda upendo wako, utulivu wako, namna unavyonisapoti katika kila hali. Wewe ndiye nguvu yangu ya kweli. Mungu kweli alichukua muda wake kukuumba.”
“Asante kwa kuwa mke wa kipekee, mama wa kipekee, na mtu pekee anayenielewa kwa dhati. Nitakuchagua tena na tena, kila siku. Heri ya maisha, baraka nyingi zaidi, na kila kilicho chema kwa sababu unastahili yote na zaidi,” aliandika Davido kwenye Instagram.
Mbali na furaha na mafanikio, ndoa yao imewahi kupitia nyakati kadhaa ngumu, mojawapo ni tukio la kufiwa na mtoto wao wa kwanza, Ifeanyi, ambaye aliaga dunia Oktoba 2022 baada ya kuzama katika bwawa la kuogelea nyumbani kwao.
Davido aliiambia The Breakfast Club kuwa tukio hilo ni moja ya nyakati ngumu zaidi kuwahi kupitia maishani mwake na kuishukuru familia yake kwa kumsaidia kuweza kusonga mbele, na sasa anafurahi kuwa baba wa watoto pacha waliozaliwa na Chioma mnamo Oktoba 2023.
“Kwa sasa tuna watoto pacha, huyo wa kiume amefanana kabisa na binti yangu [Ifeanyi] aliyefariki. Matendo yao yanafana, kila kitu alichokuwa akifanya, naye anafanya,” Davido alieleza.
Davido na Chioma walifunga ndoa ya kitamaduni Juni 25, 2024, jijini Lagos, Nigeria, na baada ya hapo walifanya harusi ya kidini huko Miami, Marekani mnamo Agosti 2025. Ikumbukwe Davido, mwanzilishi wa Davido Music Worldwide (DMW), alipata umaarufu alipoachia wimbo wake Dami Duro (2011), lakini kwa hapa Bongo alivuma zaidi kupitia ngoma yake Aye (2014).