Songwe. Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba, mkoani Songwe kwa gharama ya Sh1.8 bilioni.

Jengo la Mahakama hiyo litajengwa Kata ya Chapwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Scorpion Limited.

Akizungumza eneo la ujenzi alilomkabidhi mkandarasi huyo, leo Jumatatu, Machi 4, 2026, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe, Gabriel Malata amesema ujenzi huo utasaidia kusogeza huduma kwa wananchi na kuboresha mazingira ya utoaji haki.

Malata amesema kwa sasa Momba haina jengo la Mahakama ya wilaya, wanalotumia sasa wamepanga, hivyo kutumia gharama kubwa kulipa kodi ya pango kila mwezi.

Amesema licha ya Momba kuwa na halmashauri mbili, hakuna hata yenye jengo la Mahakama, kitendo ambacho Serikali imeona ni vyema kutoa fedha hizo kujenga  katika eneo la Kata ya Chapwa lililotolewa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

“Jengo litakalojengwa litakuwa na sehemu tofauti tofauti likiwamo jengo la Mahakama ya wilaya, Mahakama ya mwanzo, mahabusu ya kike na kiume pamoja na vyoo, ambalo ni tofauti na jengo linalotumika sasa,” amesema Jaji Malata.

Amesema ujenzi wa mradi huo utasaidia wananchi kupata haki za kimahakama kwa kuwa, muda mrefu wilaya hiyo haikuwa na jengo la Mahakama ya Wilaya, walikuwa wanapanga nyumba na kutumika kama mahakama.

“Sisi kama Mahakama tunatarajia kuanza kutoa huduma za kimahakama Januari 2027 hivyo mkandarasi ufanye kazi usiku na mchana na kuzingatia masharti ya kimkataba ndani ya miezi minane iwe imekamilika,” amesema Jaji Malata.

Aidha amesisitiza halmashauri kutenga maeneo ya kujenga Mahakama za mwanzo katika kata za Mpemba na Kamsamba ambazo zimekuwa na wingi wa wananchi wanaohitaji huduma za kimahakama.

“Naishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuidhinisha Sh1.8 bilioni kujengea Mahakama hiyo, ilikuwa hitaji la wananchi wa Momba kwa muda mrefu,” amesema Jaji Malata.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elius Mwandobo amesema licha ya ukubwa wa wilaya hiyo haikuwa na jengo la Mahakama, linalotumika sasa ni finyu na halina hadhi ya kimahakama kwa ajili ya kuhudumia wananchi kupata haki za kisheria.

Mwandobo amesema ujenzi huo pindi utakapokamilika utasaidia kuondokana na adha ya kukodi jengo lisilo na sifa za kimahakama kutoa huduma kwa wananchi.

Mkandarasi kutoka Kampuni ya Scorpion Limited, Wilson Ezekiel amesema atahakikisha anajenga jengo hilo kwa viwango kulingana na mahitaji yaliyopo kwenye makubaliano ya kimkataba.

Akizungumzia ujenzi wa Mahakama hiyo, Christopher Simbeye mkazi wa Kata ya Chapwa amesema Serikali imefanya jambo la maana katika ujenzi wa Mahakama, kwani awali walipanga jengo ambalo halikidhi kutoa huduma.

“Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za kimahakama, hivyo kama wananchi tunaomuomba mkandarasi ajenge haraka kulingana na mkataba na sisi tutashirikiana kulinda vifaa vya ujenzi,” amesema Simbeye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *