
Angalau watu 18 wamefariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa katika sehemu nyingi za Kenya.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mvua zinazoendelea zinasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Siku ya Jumapili polisi ilisema kwamba maporomoko ya ardhi yaliripotiwa katika kaunti za Tharaka Nithi, Elgeyo-Marakwet, na Kiambu katika mikoa ya kati na mashariki mwa nchi hiyo. Polisi ilithibitisha kwamba watu 18 walifariki kutokana na matukio haya na wakatoa wito wa tahadhari kutokana na hali ya hewa mbaya.
Maporomoko ya ardhi yanaathiri “familia nyingi, yanahamisha kaya, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu”, polisi ilisema, ikiwaonya wakazi wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi au yaliyoathiriwa na mafuriko kuwa waangalifu.
Haijulikani ni watu wangapi wamehamishwa makazi kutoka makazi yao.
Ripoti kutoka kwa vyombo vya habari vya ndani zinaonyesha mitaa katika mji mkuu, Nairobi, ikijaa maji kutokana na mafuriko huku magari na watembea kwa miguu wakipita kwenye barabara zilizojaa maji.
Wafanyabiashara katika vitongoji vya Makongeni na Ruai jijini hmo walifanya maandamano siku ya Jumapili kuhusu hali mbaya ya barabara kutokana na mvua, wakisema hali hio inaathiri biashara zao.
Mamlaka ya hali ya hewa ilionya mapema Ijumaa kwamba mvua hiyo inahatarisha afya kwa njia ya magonjwa yanayosababishwa na maji na kwamba uharibifu wa mazao na mashamba huenda ukawa kote nchini.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha chini ya miezi miwili ambapo badhi ya maeneo ya Kenya yanakumbwa na mafuriko mabaya. Mnamo mwezi Machi, maji yalifikia kiwango cha juu kabisa katika baadhi ya maeneo ya Nairobi, na kuua watu wasiopungua 37.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa sasa inakabiliwa na msimu wake wa mvua wa mwezi Machi hadi Mei, ambao kwa kawaida humalizika katika katikati ya mwezi Mei. Hata hivyo, wataalamu wameonya kwa muda mrefu kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu yanazidisha hali ya hewa kuwa mbaya nchini Kenya na nchi zingine za Afrika Mashariki.