
Kumekuwa na mabadiliko na maendeleo makubwa katika soka la Tanzania hivi sasa kulinganisha na miaka ya nyuma.
Kupiga hatua kwa soka letu, kumechangia kuvutia kampuni na taasisi mbalimbali kubwa na ndogo, kuwekeza fedha zao kupitia udhamini wa mashindano mbalimbali, timu na wachezaji zikiamini zitapata fursa ya kujitangaza zenyewe na bidhaa au huduma zao.
Kitendo cha soka letu kuingiza fedha, kimezidi kuboresha maisha ya timu na wachezaji,maofisa wa benchi la ufundi pamoja na waajiriwa wa nafasi tofauti za kiutawala katika klabu tofauti hapa nchini.
Uboreshwaji huo wa hali za kiuchumi umetokana na uhakika wa malipo ya mishahara, posho na stahiki nyingine ambao klabu zimekuwa nao kutokana na mafungu ambayo zinakusanya kupitia udhamini pamoja na vyanzo vingine vya mapato.
Na ndio maana tunaona kwa sasa, sio jambo la ajabu kwa wachezaji hata wa timu za kawaida kumiliki magari, nyumba au miradi tofauti ambayo ni zao la matumizi mazuri ya fedha wanazolipwa kutokana na jasho wanalovuja ndani ya uwanja.
Ni tofauti na maisha ya wachezaji wengi wa zamani ambao walicheza soka katika kipindi ambacho hakukuwa na fedha nyingi ambayo mengi ni ya kubangaiza na kundi kubwa wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na hali nzuri kiuchumi.
Kufanikiwa kimaisha kwa wachezaji wa kizazi cha sasa kumesaidia kutunza familia, ndugu, jamaa na marafiki zao jambo ambalo miaka mingi ya nyuma lilionekana kuwa gumu na kuchangia wazazi wengi wasione haja ya kuruhusu watoto wao wenye vipaji kujikita zaidi na soka kwa vile walikuwa hawaoni mwanga chanya wa mchezo huo mbele ya safari.
Hivyo kufanikiwa kwa wachezaji hivi sasa hakuna faida tu katika suala la hali za kiuchumi lakini pia kunasaidia kubadilisha mitazamo ya wazazo kuhusu mchezo wa mpira wa miguu na kupelekea hivi sasa wengi wao kuruhusu vijana wao kujihusisha na soka.
Kwa vile watoto wengi kwa nyakati hizi wamekuwa na hamu na tamaa ya kucheza soka ni vyema kaka zao ambao wamewatangulia, wakazidi kuwaongezea ari ya kuendelea kuwepo katika mchezo huo kwa kuwapa sapoti ya vifaa muhimu vinavyohitajika katika malezi na makuzi yao kimpira ili nao baadaye waje kusaidia wengine.
Katika kile wanachokivuna katika timu wanazochezea iwe kwa Ligi Kuu au Ligi za chini yake, wajenge utamaduni wa kutoa kidogo kwa ajili ya kurudisha katika timu zao za mitaani ambazo zilichangia kwa namna moja au nyingine wao kufika mahali walipo.
Wanapaswa kukumbuka kuwa hizo timu zimechangia kwa kiasi kikubwa kwa wao kufika walipo sasa kupitia mafunzo na malezi ambayo kama wasingeyapata, pengine wasingeweza kufikia ubora na nafasi waliyopo kwa sasa.
Na kwa vile timu hizo nyingine ni za mitaani na hazijasajiliwa wala kutambulika kisheria ingawa zinafahamika tu kwa namna zinavyosaka na kuendelea vipaji vya vijana wadogo kisoka, huwa zinakosa haki muhimu za kisheria za mchezaji ikiwa anauzwa kwenda timu fulani kama muongozo wa sheria na hadhi za wachezaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (Fifa) unavyofafanua.
Mahitaji makubwa ya timu hizo ambazo wachezaji wetu wanaweza kuyamudu kutokana na kile wanachokiingiza ni jezi, mipira, koni za mazoezi pamoja na vizibao ambavyo haviuzwi kwa gharama kubwa au inayoweza kuwa kiwazo kwao kununua.
Kufanya hivyo mbali na kwamba itasaidia kuandaa mazingira mazuri ya wenzao kuandaliwa kama ambavyo ilikuwa kwao lakini pia ina mchango katika kutengeneza ushawishi na hamasa kwa vijana wadogo kucheza soka ili wafikie pale walipo wao.
Wapo wachezaji wachache ambao tumeshuhudia wakifanya hivyo katika timu zilizowakuza wakati walipokuwa wadogo lakini haipaswi kuishia kwao tu bali na wengine wanapaswa kuiga pia na kufanya jambo hilo.
Mfano wa nyota ambao mara kwa mara wamekuwa wakikumbuka walikotoka na kupeleka msaada wa vifaa vya michezo ni Dickson Job, Hussein Kazi, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto, Aishi Manula, Mohamed Hussein, Masoud Abdallah na Feisal Salum.
Kwa upande mwingine vitendo kama hivyo vinasaidia kupandisha hadhi na tahamni ya mchezaji mbele ya jamii na hilo linaweza kuwa chachu ya ushawishi na mvuto wa kibiashara kutoka kwa taasisi na kampuni mbalimbali.
Kampuni na taasisi nyingi zimekuwa zikipendelea kuwatumia wachezaji ambao wanarudisha kwa jamii kwa vile wanakuwa na haiba na taswira nzuri kwa umma tofauti na wale ambao hawafanyi wala hawajishughulishi na hayo.