KUPANDA kwa kiwango cha Neo Maema Simba, unaambiwa hakujatokea kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya mambo matatu ambayo ni mabadiliko ya kiufundi, kimfumo na kiakili katika uchezaji wake.
Kutoka kuwa mchezaji wa kuingia na kutoka kikosini, sasa ameanza kujitengenezea utawala wake kwenye eneo la kiungo cha Simba, hasa kwenye mechi zenye uzito.
Ishara kubwa ya mabadiliko hayo imeonekana kwenye dabi mbili mfululizo dhidi ya Yanga. Kwanza ilikuwa fainali ya Muungano iliyopigwa Zanzibar ambapo Simba ilishinda kwa bao 1-0, kisha Ligi Kuu Bara iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katika michezo hiyo miwili, Maema alionyesha kwa nini kocha Fadlu Davids aliamua kumsajili kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mwanzoni mwa msimu huu akitua sambamba na Rushine De Reuck.
Tofauti na mwanzo wa msimu ambapo alionekana kukosa muendelezo, sasa Maema anaaminiwa akipata nafasi katika michezo minane mfululizo ya Ligi Kuu Bara akicheza kwa jumla ya dakika 436, huku jukumu lake likiwa ni kucheza kama kiungo huru anayehusika katika awamu zote za mchezo kuanzia ujenzi wa mashambulizi hadi kusaidia kujilinda.
Katika soka la kisasa, kiungo anayetawala kasi ya mchezo huwa na thamani kubwa uwanjani, Maema ameanza kuonyesha sifa hii, anapokea mpira akiwa na utulivu, akichagua aina ya pasi kulingana na presha ya mpinzani badala ya kucheza kwa pupa.
Kwenye fainali ya Muungano, alionyesha uwezo wa kupunguza kasi ya mchezo. Hakuwa na haraka ya kupeleka mpira mbele bila mpangilio, bali alihakikisha timu inabaki na umiliki wa mpira, jambo lililosaidia kuvunja kasi ya wapinzani.
Katika dabi ya ligi, aliongeza kasi ya mchezo pale nafasi zilipokuwa wazi. Hapa ndipo tunaona tofauti ya kiungo wa kawaida na yule mwenye uwezo wa kuifanya timu icheze yani mwenye uwezo wa kubadilisha mdundo wa mchezo ndani ya sekunde chache kulingana na mazingira ya uwanjani.
Kwa ujumla, Maema anakuwa kiungo anayefanya maamuzi ya kimkakati badala ya kiufundi tu. Hii inaifanya Simba iwe na ubora zaidi zaidi katikati, kwani kila shambulio au mzunguko wa mpira unapitia kwake kwa namna iliyopangiliwa.
Moja ya sifa muhimu za Maema kwa sasa ni uwezo wake wa kukaa katika maeneo magumu ya ulinzi wa mpinzani hasa kati ya kiungo na mabeki. Haya ndiyo maeneo yanayojulikana kama ‘half-spaces’ na kuyatumia vizuri kunahitaji akili ya juu ya mchezo.
Katika dabi ya sare ya 2-2, alionekana mara nyingi akipokea mpira akiwa amejitenga kidogo na walinzi wa moja kwa moja. Hii ilimpa muda wa kuamua kama apige pasi ya mbele au abebe mpira, jambo lililosaidia Simba kuendelea kushambulia kwa utulivu.
Kwenye fainali ya Muungano, alitumia nafasi hizi kuwavuta walinzi wa Yanga kutoka kwenye maeneo yao, hali iliyofungua nafasi kwa washambuliaji wa Simba kufanya majaribio ya kushambulia. Hii ni kazi isiyoonekana sana kwenye takwimu lakini ina athari kubwa kwenye mchezo.
Kwa tafsiri ya kiufundi, Maema anaonyesha uwezo wa kusoma nafasi kabla hata mpira haujafika kwake. Hii ndiyo inamfanya awe kiungo hatari kimkakati, hata kama hafungi au kutoa pasi ya mwisho.
Tofauti na awali ambapo alionekana zaidi upande wa ushambuliaji, sasa Maema ameongeza uwiano kwenye mchezo wake kwa kuchangia pia upande wa kulinda. Hii ndiyo dhana ya kiungo wa kisasa kuwa na mchango katika pande zote mbili za uwanja.
Katika mechi zote mbili dhidi ya Yanga, alionekana akiwapa presha wapinzani baada ya kupoteza mpira. Hii ilisaidia Simba kurejesha umiliki wa mpira haraka na kuzuia mashambulizi ya kushtukiza kutoka kwa wapinzani.
Pia alionyesha nidhamu ya kurudi nyuma kulinda eneo la kati, akisaidia kudumisha umbo la timu. Hii ni muhimu sana hasa kwenye mechi za dabi ambapo makosa madogo yanaweza kugharimu matokeo.
Kwa mtazamo wa kiufundi, Maema sio mchezaji wa kutegemea takwimu za mabao au pasi za mwisho pekee, bali ana athari kubwa kwenye hatua za mwanzo na za kati za mashambulizi.
Akimzungumzia kiungo huyo, kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids ambaye alimsajili nyota huyo kabla ya yeye kutimkia Raja Casablanca, anafichua kwa kusema:
“Najua ni mchezaji wa daraja gani na niliamini anaweza kuwa msaada, ilikuwa ni suala la muda tu kwa sababu unapojiunga na timu mpya tena nchi nyingine kila kitu huwa kipya, ninafurahi kusikia anaendelea vizuri.”
Akizungumzia kiwango chake kwa sasa, Maema anasema: “Niwe mkweli, ninafurahia kuwa hapa, naamini naweza kufanya zaidi kwa ajili ya Wanasimba, kuhusu mkataba tusubiri tuone nini kitatokea mwisho wa msimu, kwa sasa mwazo yangu ni kuipambania timu.”