NYOTA wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa la Ivory Coast, Didier Drogba, ameweka wazi dhamira yake ya kusaidia maendeleo ya michezo nchini baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nchi kuhusu maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027 na ukuaji wa sekta hiyo.
Drogba amesema anajivunia kupata nafasi ya kutembelea Tanzania na kushirikiana na Serikali katika kuona namna bora ya kuinua kiwango cha michezo na kuifanya kuwa chachu ya maendeleo ya vijana na jamii.
Akizungumza kuhusu mkutano wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Drogba amesema: “Nina furaha sana kuwa hapa Tanzania na kupata heshima ya kukutana na Rais. Nimealikwa kuona namna ninavyoweza kusaidia maandalizi ya AFCON.”
Drogba amesema anaiona Tanzania kama nchi inayopiga hatua kubwa katika michezo, hasa kutokana na ongezeko la uwekezaji wa Serikali katika sekta hiyo muhimu.
Amefafanua hilo kwa kusema: “Nilitembelea Bunge na kuona bajeti ya michezo imeongezeka. Hili ni jambo kubwa kwa sababu michezo ni chombo muhimu cha maendeleo.”
Akitoa ushauri kwa vijana wa Kitanzania, Drogba ameweka msisitizo mkubwa juu ya elimu kama msingi wa mafanikio.
Amesema: “Wengi wanataka kucheza mpira, lakini jambo muhimu zaidi ni elimu. Elimu inakusaidia kuwa mtu bora na mwenye maadili na inaweza kukufanya udumu kwenye mafanikio.”
Ameendelea kueleza umuhimu wa kujiamini na kujifunza kila siku, akisema: “Unapaswa kujiamini kama nilivyojiamini mimi. Kilichonisaidia kufikia mafanikio ni elimu na kujifunza kila siku.”
Katika kuelezea maisha yake binafsi, Drogba amefichua kuwa safari yake haikuwa rahisi, hasa kutokana na upinzani kutoka kwa familia yake mwanzoni.
“Baba yangu hakutaka nicheze mpira… lakini nilihakikisha nafanya vizuri shuleni. Elimu ilikuwa sehemu yangu ya usalama,” amesema.
Ameongeza kuwa mafanikio yake hayakuwa ya kumpinga mzazi wake bali kujithibitisha yeye mwenyewe: “Haikuwa vita dhidi ya baba yangu, ilikuwa ni vita ndani yangu kujithibitisha kwamba ninaweza.”
Katika maisha yake ya soka, Drogba alijijengea jina kubwa akiwa na klabu ya Chelsea ambapo alifunga mabao 164 katika mashindano yote na kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi wa Kiafrika kuwahi kucheza Ligi Kuu England.
Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kuisaidia Chelsea kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya 2012, ambapo alifunga bao muhimu na pia penalti ya ushindi, pamoja na kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu England na kushinda tuzo ya mfungaji bora mara mbili.
Pia Drogba ameweka historia akiwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ivory Coast, akifunga mabao 65.
Drogba ambaye alitua nchini Mei 3, 2026, alikuwa nchini kufuatia mwaliko wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ambapo Mei 4, 2026 alipata fursa ya kuhudhuria uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026-2027, kisha Mei 5, 2026 akaondoka.