Chanzo cha picha, Getty Images
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umesema Iran imefanya shambulio la kwanza la makombora na droni dhidi ya taifa hilo tangu kusitishwa kwa mapigano na Marekani kuanza Aprili 8, katika mfululizo wa matukio yanayoashiria kuongezeka tena kwa mvutano wa kijeshi katika Ghuba.
Kwa mujibu wa taarifa za UAE, Iran ilirusha droni mbili dhidi ya meli iliyokuwa inapita katika Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Katika upande mwingine, Jeshi la Marekani limesema limeendesha operesheni kali katika Mlango wa Hormuz, ambapo limeshambulia na kuziharibu boti saba ndogo za kijeshi za Iran zilizodaiwa kujaribu kuingilia usafirishaji wa meli zilizo chini ya ulinzi wa Marekani.
Rais Donald Trump amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mpango unaoitwa “Project Freedom” unaolenga kuhakikisha meli zinapita salama katika eneo hilo.
Aidha, Marekani imeripoti kuwa meli mbili za kibiashara zilifanikiwa kupita salama katika Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu, zikilindwa na jeshi la Marekani, katika juhudi za kupunguza hatari kwa wafanyakazi wa baharini.
Iran kwa upande wake imeendelea kusisitiza kuwa inadhibiti usalama wa Mlango wa Hormuz na imetishia kuzuia au kushambulia majeshi ya kigeni yanayojaribu kuingilia eneo hilo.
Katika upande wa kidiplomasia, Tehran imesema imepokea jibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la amani lenye mambo 14, ambalo inalenga kumaliza vita. Hata hivyo, Trump amesema huenda akalikataa pendekezo hilo, akidai Iran “bado haijalipa gharama ya kutosha,” jambo linaloacha mustakabali wa mazungumzo ukiwa na mashaka makubwa.