WAKATI Yanga ikikaribia kusherehekea ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’ amewataka wachezaji wa kikosi hicho kutambua bado wana kazi moja kubwa iliyobakia.
Kauli ya kocha huyo inakuja baada ya Yanga kuifunga TRA United mabao 3-0, Juni 27, 2026 na kubakisha mechi moja ya ugenini dhidi ya JKT Tanzania, ambapo endapo itashinda itatangazwa bingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2025-2026.
Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa nyota wa Yanga, Allan Okello akifunga mabao yote matatu (Hat-Trick), imeifanya timu hiyo kufikisha pointi 72, ambapo ikiifunga JKT Tanzania kesho Jumanne itakuwa na 75 ambazo haziwezi kufikiwa na wengine msimu huu ndani ya ligi hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Moallin amesema wachezaji hawapaswi kuendelea kufurahia kutokana na kile walichokifanya dhidi ya TRA United, kwani bado wana kazi kubwa iliyo mbele yao ya kutimiza malengo ya kutetea taji hilo.
“Baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la CRDB, kwa sasa malengo yetu tumehamishia Ligi Kuu Bara, TRA United ilitupa mechi nzuri na ya ushindani ila tunashukuru tumepata matokeo mazuri ya ushindi tuliyoyahitaji,” amesema Moallin.
Aidha, Moallin amesema gepu la pointi mbili lililopo na wapinzani wao wakubwa Simba ndilo linalowapa hamasa zaidi ya kuendelea kupambana ili kutetea taji hilo, huku akiwataka wachezaji kutambua bado wana kazi kubwa ya kuwapa furaha mashabiki zao.
“Kombe la Ligi Kuu ndilo pekee lililokuwa mikononi mwetu na kuanzia kwetu benchi la ufundi, viongozi, mashabiki na wachezaji tunalitambua hilo, hii ni ishara inayoonyesha tunapaswa kupambana ili kutimiza malengo yetu,” amesema Moallin.
Katika mechi 29 za Ligi Kuu Bara ilizocheza Yanga msimu huu wa 2025-2026, imeshinda 22, sare sita na kupoteza moja, ikifunga mabao 68 na kuruhusu tisa, ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 72, nyuma yake kuna watani wao wa jadi, Simba iliyopo ya pili na pointi 70.
Moja ya faida kubwa inayoipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu ni tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya wapinzani zao wa jadi Simba, kwa sababu hata ikitoka sare dhidi ya JKT Tanzania ina uwezekano pia mkubwa wa kuwa bingwa.
Simba inayomaliza msimu kwa kucheza dhidi ya KMC iliyoshuka daraja, katika mechi 29 ilizocheza, imeshinda 21, sare saba na kupoteza moja, ikifunga mabao 53 na kuruhusu 11, ambayo ni sawa na tofauti ya mabao 42, huku washindani zake Yanga ikiwa na tofauti ya mabao 59.
Moallin anainoa Yanga akirejea kikosini hapo baada ya kuondoka Julai 27, 2025, alipohudumu akiwa ni Mkurugenzi wa Ufundi. Hivi sasa anakaimu nafasi hiyo kufuatia aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, raia wa Ureno Pedro Goncalves kusitishiwa mkataba wake, Mei 6, 2026.