Kupitia taarifa iliyotolewa na Radio Okapi ya Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana Mei 6 katika mtaa wa Plateau 1 baada ya mvua kubwa kunyesha katika jiji hilo. 

Vyanzo vya eneo hilo vimesema maporomoko hayo yalitokea karibu na Kanisa Katoliki la Sainte Honorine, ambapo nyumba moja ilifunikwa na udongo ulioporomoka.

Mbali na kupoteza maisha, uharibifu mkubwa wa mali pia umeripotiwa katika eneo hilo huku barabara na njia za mawasiliano zikiharibiwa vibaya.

Wakazi waomba msaada wa dharura

Wakizungumza na Radio Okapi wakazi wa eneo hilo wameelezea hali kuwa mbaya zaidi huku baadhi ya maeneo ya mtaa huo yakikaribia kutofikika kutokana na madhara ya mvua hizo na mafuriko.

“Sisi wakazi wa mtaa wa Plateau 1 tunatoa tahadhari. Mvua ya usiku wa Mei 5 hadi 6 imesababisha uharibifu mkubwa kiasi kwamba tayari tumepoteza mtu mmoja katika mtaa huu. Maeneo ya Mambila na Marsavco karibu yamekatika kabisa. Tunaziomba mamlaka zitusaidie,” amesema mkazi mmoja.

Mvua hizo kubwa zimeonesha tena hatari inayowakabili wakazi wa baadhi ya maeneo ya Kinshasa kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi, hasa katika maeneo yenye makazi mengi yaliyo kwenye vilima.

Mamlaka zataka usafi wa mazingira

Meya wa Mont Ngafula, Séverin Lumbu, amethibitisha tukio hilo na kuwataka wananchi kubaki watulivu huku wakichukua hatua za kujikinga dhidi ya majanga mengine.

“Tuungane pamoja kufanya mitaa na barabara zetu kuwa safi, tusafishe mifereji ya maji na kutupa taka katika maeneo yanayofaa,” amesema Lumbu.

Mamlaka zimeonya kuwa msimu huu wa mvua unaendelea kuwa tishio kubwa kwa wakazi wa Kinshasa, ambapo mifumo mibovu ya maji taka, ujenzi holela na mrundikano wa taka huchangia kuongezeka kwa mafuriko na mmomonyoko wa udongo.

Viongozi wa serikali na jamii sasa wanatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kuzuia kupotea kwa maisha zaidi wakati mvua kubwa zikiendelea kunyesha katika mji huo mkuu wa Congo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *