Hali hiyo ilidhihirika wakati gwiji wa soka wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Mikaël Silvestre, alipokutana na Baba Mtakatifu Papa Leo XIV katika makao ya Vatican, akiwasilisha mpango wa Umoja wa Mataifa wa mpango wa mpira wa miguu kwa malengo au Football for the Goals (FFTG) unaolenga kuhamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Lengo kuu la kukutana huko ni kuonesha nafasi ya kipekee ya mpira wa miguu katika kukuza uendelevu, usawa na haki za binadamu duniani.

© Vatican Apostolic Archives Mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu wa taifa la Ufaransa Mikaël Silvestre (katikati) anamtolea Papa Leo XIV shati la “UN Football for the Goals” au mpira kwa malengo, pamoja na Papa Paolo Celi.

Silvestre, ambaye aliwahi kuchezea klabu kubwa barani Ulaya zikiwemo Inter Milan,Manchester United na Arsenal, alitumia fursa hiyo kusisitiza namna umaarufu wa soka unavyoweza kutumika kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Katika mkutano huo alimkabidhi Papa zawadi mbalimbali ikiwemo jezi ya FFTG yenye jina lake, skafu ya FFTG pamoja na mpira wa SDG uliobeba alama ya malengo 17 ya maendeleo endelevu.

“Mimi na Baba Mtakatifu tunatoka katika wito tofauti kabisa wa maisha, lakini leo tumeshiriki imani moja kwamba mpira wa miguu una nguvu ya kuhamasisha mabadiliko chanya. Soka lina jukwaa kubwa duniani, na tunapaswa kulitumia kuleta tofauti” Amesema Silvestre

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mheshimiwa wa Kipapa Paolo Celi, ambaye ni mjasiriamali na Rais wa Amitié France Italie.

Papa Leo XIV, anayefahamika kuwa mpenda michezo, alipokea zawadi hizo kwa furaha na kupongeza mpango huo, huku akihamasisha kuendelezwa kwa juhudi za kufanikisha dhamira hiyo. Aidha, alitoa baraka kwa familia za Silvestre na Celi pamoja na washiriki wote wa mpango wa FFTG na Umoja wa Mataifa.

© Vatican Apostolic Archives Mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu wa Ufaransa Mikaël Silvestre (kushoto) anampa Papa Leo XIV shati la “UN Football for the Goals” au mpira kwa malengo, pamoja na Papa Paolo Celi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano na Ushirikishwaji wa Kimataifa katika Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa, Robert Skinner, amesema “Kuwasilisha mpango wa Football for the Goals kwa Baba Mtakatifu kunaonesha jinsi mchezo maarufu zaidi duniani unavyoweza kuwaunganisha watu katika maadili ya pamoja na wajibu wa pamoja. Tunatumaini tukio hili litahamasisha wadau zaidi wa soka kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu.”

Nyuma ya pazia: Safari ya mpira wa SDG hadi Vatican

Licha ya picha nzuri ya tukio hilo, mafanikio yake yalitokana na juhudi kubwa za ushirikiano. Mkutano huo uliandaliwa kupitia uratibu wa karibu kati ya timu ya Football for the Goals katika Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, Silvestre na wawakilishi wa Vatican.

Mpira wa SDG uliotolewa kwa Papa ulikuwa zao la ubunifu na kujituma kutoka Duka la Vitabu la Umoja wa Mataifa pamoja na Kitengo cha Machapisho. Hata hivyo, kuusafirisha mpira huo hadi Roma kwa wakati kulikumbwa na changamoto za usafirishaji, ambapo huduma ya pouch ilifika tu uwanja wa ndege na ratiba hazikuendana.

Katika hatua ya haraka, Mkuu wa Machapisho ya Umoja wa Mataifa, Mary Glenn, alichukua jukumu la kupeleka kifurushi hicho kwa DHL, huku timu ya usambazaji ikihakikisha nyaraka za forodha zinakamilika kwa usahihi. Hatimaye, Silvestre alikamilisha mchakato huo kwa kulipia gharama za forodha katika ofisi ya DHL mjini Roma.

Kuhusu mpango wa Football for the Goals (FFTG)

Mpango wa Football for the Goals ni juhudi ya Umoja wa Mataifa inayolenga kuhamasisha wadau wote wa soka duniani ikiwemo mashirikisho, ligi, vilabu, wachezaji na asasi zisizo za kiserikali kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Umoja wa Mataifa Mpira wa soka wwenye maandishi ya SDG una alama 17 za Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) yaliyoundwa kukuza malengo ya kimataifa, uendelevu, na usawa kupitia michezo.

Kupitia mpango huu, wadau wa soka wanahimizwa kuoanisha mikakati na shughuli zao na malengo ya SDGs, huku wakitumia umaarufu wa mchezo huo kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii. 

Wanachama wa mpango huo hutumia majukwaa yao, kama mashindano, vyombo vya habari na mashabiki, kuongeza uelewa na kuhimiza hatua za vitendo katika kufanikisha maendeleo endelevu.

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu yalipitishwa mwaka 2015 na viongozi wa dunia, yakilenga kushughulikia changamoto mbalimbali zikiwemo umaskini, afya, elimu, usawa wa kijinsia na mazingira. Malengo haya yanaendelea kuhamasisha juhudi za kimataifa katika kujenga dunia yenye usawa na maendeleo jumuishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *