Hata watu wasio na uelewa au wasiovutiwa na habari za biashara huenda wamewahi kusikia kuhusu neno GDP, ambalo hutajwa mara kwa mara katika vyombo vya habari kama kiashiria cha maendeleo.

GDP kwa lugha rahisi ni nini?

Kwa lugha rahisi, GDP ni jumla ya kila kitu ambacho nchi huzalisha na kuuza, lakini wachumi wamejua kwa miaka mingi kuwa kipimo hicho hakitoi picha kamili.

Maeneo yasiyojumuishwa kwenye GDP

  • Kazi zisizolipwa kama kulea watoto au kuwahudumia wanafamilia wenye ulemavu hazihesabiwi kama mchango chanya.
  • Vipimo vya ukosefu wa usawa havijumuishwi,.
  • Wala gharama za uchafuzi wa mazingira au matumizi ya mabaya ya rasilimali za watu, (unyonyaji wa rasilimali)

Hili ni tatizo kwa sababu huunda motisha na malengo yasiyo sahihi katika utungaji wa sera. Kwa kufuatilia ukuaji wa GDP pekee, watunga sera wanaweza kuwa hawalengi yale yaliyo muhimu zaidi kwa watu na sayari.

Kuhesabu yale yenye umuhimu

Ukosefu wa vipimo vya kina zaidi vya kunasa maendeleo umekuwa ukitambuliwa kwa muda mrefu na jumuiya ya kimataifa, na suala hilo lilichukuliwa mwaka mmoja uliopita wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipoanzisha Jopo la UN la Wataalamu wa Ngazi ya Juu likimulika kile kilichoitwa Zaidi ya GDP.

Baada ya mwaka mmoja wa mashauriano, jopo hilo leo Alhamisi limetoa matokeo yake kupitia ripoti iliyopatiwa jina “Kuhesabu Yenye Umuhimu”, iliyofafanuliwa kama “Dira kwa watu na sayari.”

Ripoti hiyo inatoa mwongozo wa kwanza wa kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa wa kuondoka kwenye utegemezi wa kipimo finyu cha GDP, na inatoa hoja yenye nguvu ya kutumia vigezo vipana zaidi ya vipimo ili kuongoza sera na maamuzi.

Ripoti haipingi matumizi ya GDP bali inataka wigo upanuliwe

Haipingi matumizi ya GDP katika kupima uzalishaji wa kiuchumi, lakini inanukuu onyo kutoka kwa mchumi aliyebuni kipimo hicho — mshindi wa Tuzo ya Nobel Simon Kuznets — kwamba GDP pekee haitoshi kupima ustawi wa taifa.

© ADB/DERAriel Javellana “Zaidi ya GDP” ni mbinu au njia mpya ya kupima maendeleo.

Kwa kutumia utafiti wa miongo kadhaa pamoja na majaribio mengi ya kitaifa na kimataifa ya kutafuta njia bora za kupima maendeleo, kikundi hicho kinatoa ajenda ya vitendo itakayowezesha serikali na mfumo wa kimataifa kupunguza utegemezi mkubwa wa GDP pale ambapo si kipimo sahihi.

Kiini cha ripoti ya kikundi hicho ni jedwali la viashiria vinavyojengwa juu ya nguzo nne: kanuni za msingi (ikiwemo amani, haki za binadamu na heshima kwa sayari), ustawi wa sasa, usawa na ujumuishaji, pamoja na uendelevu na ustahimilivu.

Hatua zinazofuata: Wajibu wa kila mtu vikiwemo vyombo vya habari

Ingawa jopo hilo la wataalamu halipendekezi mbadala wa GDP unaozipanga nchi kwa viwango, linapendekeza kuundwa kwa seti ndogo ya viashiria vikuu vya kuelezea kwa watunga será na umma maendeleo kwa uwazi zaidi.

Hatua za vitendo za kuendeleza ajenda ya “Zaidi ya GDP” zimejumuishwa katika ripoti hiyo, kama vile kupitishwa kwa haraka kwa “dashibodi za maendeleo” za kitaifa, zinazolingana na vipaumbele vya kila taifa na kuingizwa katika michakato ya utungaji sera.

Pia inapendekezwa kuanzishwa kwa mfumo wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa utoaji taarifa, ukiwemo ripoti ya kila mwaka ya maendeleo inayolingana na ufuatiliaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Aidha, Vyuo Vikuu, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na vyombo vya habari vinahimizwa kuchangia kupitia utafiti, utoaji taarifa, na ushiriki wa maana ili kubadilisha mjadala na kuwawajibisha viongozi kuhusu vipimo vya maendeleo vinavyokwenda zaidi ya GDP.

Nchi wanachama pitisheni njia mpya za kupima maendeleo- Guterres

Akizungumza baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu António Guterres amezitaka nchi kupitisha njia mpya za kupima maendeleo zaidi ya Pato la Taifa (GDP), akisema kuwa ukuaji wa uchumi pekee hauakisi tena ustawi halisi wa watu na sayari.

Guterres amesema mfumo unaopendekezwa unajumuisha dashibodi ya viashiria vinavyolenga maeneo manne muhimu: ustawi, usawa na ujumuishaji, uendelevu na ustahimilivu, pamoja na misingi ya amani, haki za binadamu na ulinzi wa mazingira.

“Vipimo hivyo vipya vitatathmini masuala kama afya, elimu, ajira, taasisi za kiraia, miundombinu na hali ya mazingira, ikiwemo hewa safi, maji salama na usalama wa chakula,” amesema Guterres.

Amesisitiza kuwa ukosefu wa usawa na umaskini haviwezi tena kukubalika kama hali zisizoepukika, akieleza usawa kuwa “msingi wa mshikamano wa kijamii na nguzo ya amani.”

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa pia ameonya kuwa kuangazia mapato ya sasa na uzalishaji wa kiuchumi pekee kunapuuza umuhimu wa kulinda rasilimali za asili, maarifa na mali nyingine muhimu kwa maendeleo ya baadaye, hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Jukumu la serikali na asasi za kiraia, wataalamu wa takwimu na wengineo

Akiitaja ripoti hiyo kuwa ni “mwito wa kuchukua hatua,” Guterres amesema serikali, asasi za kiraia, biashara, wataalamu wa takwimu na mashirika ya kimataifa lazima washirikiane kutekeleza viashiria hivyo vipya, huku taasisi za kifedha za kimataifa zikihimizwa kuvijumuisha katika maamuzi yao.

Mchakato wa majadiliano kati ya serikali unaanza sasa,” amesema, akizihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuboresha na kuhalalisha matumizi ya dashibodi hiyo inayopendekezwa.

“GDP haitoshi,” Guterres amesema. “Ukuaji kwa gharama yoyote unatufanya sote kuwa maskini zaidi, si matajiri zaidi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *