Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema leo Alhamisi kuwa hatari ya kiafya kwa umma duniani kutokana na mlipuko wa virusi vya Hanta unaohusishwa na meli ya kifahari ya kitalii bado ni ndogo, huku shirika hilo likiendelea na harakati za uchunguzi wa chanzo cha mlipuko huo sambamba na kufuatilia abiria na watu waliokutana nao katika nchi mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi leo tarehe 7 Mei 2026,  Dkt. Tedros amesema bado maambukizi yaliyothibitishwa ni watu wanane katika meli ya kitalii yenye bendera ya Uholanzi, MV Hondius, na vito ni vitatu, wawili kati yao wanandoa.

Meli hiyo iliondoka Argentina kupitia baharí ya Atlantiki ambako Jumamosi baada ya ripoti za kuwemo kwa wagonjwa ndani yake, ilitia nanga nchini Cabo Verde, magharibi mwa Afrika.

Dkt. Tedros amesema kuwa  “kabla ya kupanda meli, wagonjwa wawili wa mwanzo walikuwa wamesafiri kupitia Argentina, Chile, na Uruguay katika safari ya kutazama ndege warukao. Safari hiyo ilijumuisha kutembelea maeneo ambayo yalikuwa na aina ya panya waonaojulikana kubeba virusi vya Andes. WHO inafanya kazi pamoja na mamlaka za afya nchini Argentina ili kuelewa mienendo ya wanandoa hao, na ninaishukuru serikali ya Argentina kwa ushirikiano wake, kutokana na uzoefu na utaalamu wake kuhusu virusi vya Andes.”

Argentina pia imetuma vifaa 2,500 vya uchunguzi wa maabara katika nchi tano kusaidia juhudi za upimaji wa haraka.

Virusi vya Andes vimetambuliwa kuwa chanzo

Maafisa wa WHO wamesema mlipuko huo unahusisha virusi vya Andes, aina ya virusi vya Hanta inayopatikana Amerika Kusini na ndiyo aina pekee inayojulikana kuweza kuambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa kiwango kidogo.

Dkt. Tedros amesema muundo wa maambukizi katika tukio la sasa unaonekana kufanana na milipuko ya awali.

Mlolongo wa matukio ya mlipuko wa sasa

Dkt.Tedros amesema mgonjwa wa kwanza aliyefahamika alianza kuugua tarehe 6 Aprili na alifariki akiwa ndani ya meli tarehe 11 Aprili. Kwa sababu dalili zake zilifanana na magonjwa mengine ya mfumo wa upumuaji, sampuli hazikuchukuliwa na mwanzoni virusi vya Hanta havikushukiwa kuwa chanzo.

Baadaye mke wa mwanaume huyo alishuka katika kisiwa cha Saint Helena akiwa tayari ana dalili za ugonjwa. Hali yake ilizidi kuwa mbaya akiwa kwenye ndege kuelekea Johannesburg, Afrika Kusini tarehe 25 Aprili na alifariki siku iliyofuata.

Vipimo vilivyofanywa vilithibitisha maambukizi ya virusi vya Hanta.

Abiria wa tatu alifariki tarehe 2 Mei baada ya kupata dalili siku kadhaa kabla.

Abiria mwingine aliyeambukizwa alihamishwa kutoka Kisiwa cha Ascension kwenda Afrika Kusini ambako bado amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum.

Abiria wengine watatu waliokuwa na dalili walipatiwa matibabu baada ya madaktari kutoka Cabo Verde kupanda meli hiyo. WHO iliratibu kuhamishwa kwao kwenda Uholanzi kwa matibabu.

Wawili bado wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali nzuri, huku abiria mwingine ambaye hana dalili akisafiri kwenda Ujerumani.

Mgonjwa wa nane ni abiria aliyeshuka katika kisiwa cha Saint Helena na baadaye kupatikana na maambukizi mjini Zürich nchini Uswisi. Uchunguzi wa vinasaba uliofanywa na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Geneva, ulithibitisha kuwa virusi hivyo ni aina ya Andes.

© WHO Wagonjwa watatu walioshukiwa kuwa na hantavirus wamehamishwa kutoka kwenye meli na wako njiani kwenda kupata matibabu nchini Uholanzi.

Hatua za WHO kuzuia maambukizi zaidi

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema tayari wameanzisha mwitikio wa kimataifa wenye lengo la kudhibiti mlipuko huo na kuzuia maambukizi zaidi.

Shirika hilo limewaagiza abiria wote waliomo ndani ya MV Hondius kubaki ndani ya vyumba vyao. Vyumba vinaendelea kusafishwa kwa dawa maalum za kuua vijidudu, na abiria yeyote anayeonesha dalili anatengwa.

Mapema Mwakilishi Mkazi wa WHO nchini Cabo Verde Ann Lindstrand amesema hivi sasa meli hiyo Hondius iko njiani kuelekea visiwa vya Canary nchini Hispania, “na kwenye meli tuna daktari wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna madaktari wawili wa Kiholanzi ambao wameimarisha timu, na kuna mtaalamu mmoja wa magonjwa ya mlipuko ambaye atasafiri na meli hadi bandari inayofuata ambayo ni visiwa vya Canary. Kwa sasa hakuna mtu mgonjwa kwenye meli, lakini iwapo mtu ataugua, basi kutakuwa na madaktari na vifaa vya matibabu vya kuwahudumia wakati wa safari.”

WHO pia inaandaa mwongozo wa namna ya kuwashusha salama abiria na wafanyakazi pamoja na kuratibu safari zao baada ya meli kufika katika visiwa vya Canary.

Dkt. Tedros amemshukuru Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sánchez kwa kukubali kuipokea meli hiyo na kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko huo.

“Hispania ina uwezo kamili wa kudhibiti hatari hii,” amesema Tedros, akiongeza kuwa WHO bado inaona hatari kwa wakazi wa visiwa vya Canary kuwa ndogo.

Uchunguzi wa watu waliokutana na wagonjwa unaendelea

WHO imezijulisha nchi 12 ambazo raia wake walishuka katika kisiwa cha Saint Helena wakati wa safari hiyo. Nchi hizo ni pamoja na Canada, Denmark, Ujerumani, Uholanzi, New Zealand, Singapore, Sweden, Uswisi, Uturuki, Uingereza na Marekani.

Nazo mamlaka za afya nchini Afrika Kusini pia zinaendelea kuwafuatilia abiria waliokuwa kwenye ndege kutoka Saint Helena kwenda Johannesburg pamoja na mwanamke aliyefariki dunia.

Dkt. Tedros ameonya kuwa wagonjwa wengine wanaweza kujitokeza kwani kipindi cha kujificha kwa virusi vya Andes hadi kubainika au kutokeza ni hadi wiki sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *