Sasa, wakati mahitaji ya kibinadamu yakiongezeka, ufadhili ukipungua na athari za ukame zikiendelea kuikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, mashirika ya misaada yanakimbizana na muda kuzuia janga jingine kubwa la njaa.

Akiwa amesimama juu ya kichuguu kikubwa katika maeneo makavu ya kaskazini mashariki mwa Somalia, mvulana mwenye umri wa miaka 10, Farah, pamoja na mama yake Safiya Maxamed, wanajikinga dhidi ya jua kali huku wakichunga mbuzi wachache waliobaki wakila matawi yenye miiba.

“Nilikuwana mbuzi 100,” anasema Maxamed. “Hawa watano unaowaona ndio wote waliobaki.”

Mabwawa yaliyokauka, mazao yaliyoharibika, mizoga ya wanyama na vyungu vya zamani vilivyojaa majivu sasa ni sehemu ya mandhari mpya katika kijiji cha Diilin, eneo la Puntland. Mifugo, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa uti wa mgongo wa maisha ya kiuchumi na kitamaduni eneo hilo, imeangamizwa na misimu mitatu mfululizo ya mvua hafifu.

Sasa, kama mamilioni ya Wasomali wengine wanaokabiliwa na njaa, Maxamed na familia yake ya watu sita wameishiwa matumaini, huku msaada wa kibinadamu kutoka WFP na mashirika mengine ukitoweka kutokana na ukosefu wa fedha. 

Njaa imetamalaki kila kona

Kadri akiba ya chakula na fedha inavyopungua, familia hiyo inalazimika kupunguza kiwango cha chakula na kufikiria kukimbia kwenda maeneo wanayotarajia kupata msaada wa dharura.

“Tumekuwa tayari kuokoa maisha, lakini bila msaada endelevu jamii zinaweza kurejea katika njaa ya dharura au hali mbaya zaidi,” amesema Mkurugenzi wa WFP nchini Somalia, Hameed Nuru.

Somalia inakabiliwa na moja ya majanga magumu zaidi ya njaa katika miaka ya hivi karibuni, yanayosababishwa na ukame mkali, migogoro, watu wengi kukimbia  makazi yao na upungufu mkubwa wa misaada ya kibinadamu. Pia, athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati zimeongeza bei za chakula na mafuta na kuvuruga minyororo ya usambazaji, hali inayotishia utoaji wa misaada ya kuokoa maisha, hasa kwa watoto.

Licha ya mvua zilizonyesha hivi karibuni, tathmini za wataalamu zinaonesha kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa ya kiwango cha mgogoro au zaidi karibu imeongezeka maradufu ndani ya mwaka mmoja na kufikia milioni 6.5. Kati yao, milioni 2 wako katika hali ya njaa ya dharura, kiwango cha pili kwa ukali wa uhaba wa chakula, huku idadi hiyo ikiongezeka mara tatu ndani ya miezi minane pekee. Zaidi ya watoto milioni 1.8 wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu.

“Familia nyingi zimelazimika tena kufanya maamuzi magumu zaidi,” amesema Nuru. “Wameuza mali zao chache walizokuwa nazo, wamepunguza au kusitisha kabisa milo, na wameacha kila kitu nyuma kutafuta msaada lakini safari hii hakuna msaada unaopatikana.”

Hali ya sasa inafanana kwa kiasi kikubwa na ile ya mwaka 2022, ambapo ukame mkubwa uliisukuma Somalia karibu na baa la njaa. Wakati huo, janga hilo liliepukwa kwa shida baada ya WFP kuongeza misaada ya chakula na lishe kwa kiwango kikubwa na kuwafikia watu milioni 8, mafanikio yaliyowezekana kutokana na msaada mkubwa wa wahisani, washirika wa kibinadamu na Serikali ya Shirikisho ya Somalia.

Leo, Somalia ipo katika nafasi bora zaidi ya kuongeza hatua za misaada, jambo linaloipa uwezo mkubwa wa kuzuia majanga na kusaidia jamii kuanza kujijenga upya. Ongezeko la misaada linaweza kubadili hali ya sasa, na WFP ipo tayari kuongeza shughuli zake mara moja.

Kwa sasa, WFP ndiyo nguzo kuu ya mwitikio wa kibinadamu nchini Somalia, ikitoa karibu asilimia 90 ya misaada ya chakula na kusaidia washirika kote nchini. Ukame ulipoanza kuwa mbaya zaidi, shirika hilo lilitoa misaada ya fedha taslimu ya dharura kwa watu 380,000 walioathirika kupitia mifumo ya serikali ya ulinzi wa kijamii.

Hata hivyo, kutokana na upungufu wa fedha, WFP sasa inaweza kuwafikia mtu 1 tu kati ya 10 wanaohitaji msaada wa haraka, na kuna hatari ya kusitisha kabisa misaada ya dharura ifikapo Julai mwaka huu.

Kukesha na njaa

Kijiji cha Maxamed ni miongoni mwa wilaya 30 ambako WFP imesitisha utoaji wa msaada wa chakula wa dharura kutokana na ukosefu wa fedha. Kitaifa, hali hiyo pia imelazimisha shirika hilo kupunguza msaada wa lishe kwa watoto pekee, huku wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wakikosa huduma. Aidha, idadi ya vituo vya afya vinavyoungwa mkono na WFP imepungua kutoka zaidi ya 600 mwaka 2025 hadi 120 pekee sasa.

“Katika mji huu tunaoishi, kila mtu yuko katika hali ngumu sana. Mamia ya familia hulala njaa usiku, na watoto hawaendi shule,” amesema Maxamed. “Baadhi ya watu hukaa wiki mbili mfululizo bila chakula, wala hata maziwa hawapati.”

Awali familia ya Maxamed ilikuwa ikijitegemea kupitia mifugo yao. Watoto wake walikuwa wakisoma mjini, na yeye mwenyewe alikuwa akiwasaidia wanafunzi wengine kufundisha. Lakini baada ya mbuzi wake kuanza kufa taratibu kutokana na miaka miwili ya karibu kutokuwepo kwa mvua, familia ilipoteza chanzo chake cha kipato na chakula.

“Hakuna siku ya kawaida tena,” amesema. “Katika wiki moja, tunaweza kula usiku nne tu, huku usiku mwingine mitatu tukikesha na njaa.”

Kadri mateso yanavyozidi kuongezeka, familia hiyo inaweza kulazimika kuelekea kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani, kujiunga na watu milioni 4 wanaotarajiwa kukimbia makazi yao kutokana na ukame mwaka huu.

Fadumo Abdikarim tayari amepitia safari hiyo baada ya kukimbia migogoro na njaa. Sasa anaishi na familia yake katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Mogadishu. Hata huko, upungufu wa fedha umelazimisha WFP kupunguza misaada yake.

“Kuna shida kubwa na mahitaji makubwa,” amesema Abdikarim akielezea hali katika kambi hiyo yenye msongamano. “Baadhi ya watoto hawana baba, wengine hawana mama, na watu wengi hawana kazi.”

Tayari kuokoa maisha

Uhamasishaji mkubwa wa misaada ulioshuhudiwa wakati wa janga la mwisho la njaa Somalia unaweza pia kusaidia kubadili hali ya sasa. Kwa ufadhili wa kutosha, WFP na washirika wake wanaweza kuongeza haraka misaada ya chakula na lishe inayohitajika kuokoa watoto dhidi ya utapiamlo na kusaidia familia kurejesha maisha yao.

“Tumekuwa tayari kuokoa maisha, lakini bila msaada endelevu jamii zinaweza kurejea katika njaa ya dharura au hata hali mbaya zaidi,” amesema Nuru. “Kupungua zaidi kwa misaada kutasababisha athari kubwa za kibinadamu, kiusalama na kiuchumi ambazo zinaweza kuvuka mipaka ya Somalia.”

Kwa familia kama ya Maxamed, ambayo tayari imepoteza karibu kila kitu, kila siku huanza kwa swali lilelile; watawezaje kutumia kwa uangalifu kile kidogo kilichobaki, na wataendelea kuvumilia kwa muda gani kabla nao hawajalazimika kuondoka nyumbani kwao?

Jua linapotua, yeye na mwanawe wanarejea nyumbani wakiwa wamebeba chombo kidogo cha plastiki chenye kiasi kidogo cha maji kwa ajili ya familia yao.

“Wanyama wamekwisha, na maisha ya watu yako hatarini,” amesema Maxamed. “Ikiwa hali hii ngumu itaendelea, bila maji na bila chakula, watu watakufa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *