“Uhamiaji sio mgogoro,” amesema. “Mgogoro ni kushindwa kwa dunia kushirikiana katika kuusimamia.”

© UNICEF/Juan Haro Safari ya msichana mvenezuela na baba yake kupitia mojawapo ya njia hatari zaidi za uhamiaji ulimwenguni.

Maelfu wamekufa na kusafirishwa kiharamu 

Katibu Mkuu huyo ameelezea hali mbaya inayowakabili wahamiaji duniani, akitaja takwimu kutoka ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa kwa ajili ya jukwaa hilo. 

Kwa mujibu wa Guterres, zaidi ya watu 200,000 wengi wao wanawake na wasichana walisafirishwa kiharamu katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku zaidi ya wahamiaji 15,000 wakifariki dunia au kutoweka katika njia za uhamiaji ndani ya miaka miwili pekee.

“Hakuna nchi inayoweza kusimamia uhamiaji peke yake,” amesisitiza, akitaka ushirikiano mkubwa wa kimataifa kulinda haki za wahamiaji na kuvunja mitandao ya kihalifu ya usafirishaji haramu wa binadamu ambayo “inanufaika na vifo na kugeuza mateso kuwa biashara.”

Wito wa njia salama na halali za uhamiaji

Guterres pia amezitaka serikali kupanua wigo wa njia salama na halali za uhamiaji kwa wafanyakazi, wanafunzi, familia na watu wanaotafuta hifadhi na ulinzi. Amesema mifumo ya haki ya uhamiaji inaweza kupunguza uhamiaji usio rasmi, kudhibiti unyonyaji na kusaidia kukidhi mahitaji ya soko la ajira. 

“Njia za uhamiaji zinapokuwa wazi, za haki na zinazofikika kwa wote, kila mmoja hunufaika,” amesema. 

© SOS Méditerranée/Fabian Mondi Wahamiaji waliokuwa wakijaribu kuingia Ulaya kupitia bahari ya Mediterania wakiokolewa baharini

Katibu Mkuu Guterres amezitaka nchi kuondoa ada za ajira kwa wafanyakazi wahamiaji, kutambua taaluma na vyeti vyao pamoja na kupunguza gharama za kutuma fedha kwa familia zao.

Uwekezaji na ushirikiano vyatajwa kuwa suluhisho

Katibu Mkuu huyo pia ametoa wito wa kuongeza uwekezaji katika elimu, ajira na fursa kwa vijana katika nchi za asili ili kupunguza shinikizo la watu kulazimika kufanya safari hatari za uhamiaji. 

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, ukusanyaji bora wa takwimu za uhamiaji na kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Uhamiaji Salama, wa Utaratibu na Halali. 

“Uhamiaji unapaswa kuwa chaguo halisi,” amesema Guterres, akizitaka nchi kubadilisha ahadi kuwa hatua za vitendo “katika maisha ya wahamiaji na jamii wanazozijenga.”

Mkuu wa IOM aitaka  dunia kurejesha imani katika ushirikiano wa uhamiaji

Katika hotuba yake kwenye jukwaa hilo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, na Mratibu wa Mtandao wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhamiaji, Amy Pope, ametoa wito kwa viongozi wa dunia kurejesha imani na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu uhamiaji, akionya kuwa maelfu ya maisha yanaendelea kupotea kutokana na mifumo isiyo salama ya uhamiaji.

Akizungumza katika Jukwaa hilo Bi.Pope amesimulia kisa cha fundi muwashi kijana kutoka Bangladesh aliyekutana naye Libya, aliyenusurika katika ajali ya boti katika Bahari ya Mediterania baada ya wasafirishaji haramu kumwahidi kumfikisha Ulaya.

“Fundi muwashi kijana mwenye ujuzi unaohitajika na dunia hapaswi kuhatarisha maisha yake baharini kutafuta ajira yenye hadhi,” amesema. “Uhamiaji ni suala la kibinadamu sana. Ni watu, vipaji, mnepo na matarajio.”

© IOM/Alexander Bee Kundi la wahamiaji likipita Djibouti

Wito wa njia salama na hatua kali dhidi ya wasafirishaji haramu

Pope amesema zaidi ya watu 82,000 wamefariki dunia au kupotea katika njia za uhamiaji katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, akisisitiza kuwa vifo vingi vinaweza kuzuilika. 

Almezitaka serikali kuanzisha njia salama na za kawaida za uhamiaji, kuimarisha mifumo ya ajira na kuongeza juhudi za kupambana na mitandao ya usafirishaji haramu na ulanguzi wa binadamu inayowakatili wahamiaji wanaokata tamaa.

“Hakuna nchi inayoweza kusimamia uhamiaji peke yake na hakuna anayenufaika pale uhamiaji unapodhibitiwa vibaya,” amesema Pope. 

Ameongeza kuwa kizazi kijacho cha wahamiaji kinapaswa kusafiri kupitia “njia salama na za kawaida kuelekea ajira yenye heshima si kushikamana na maisha hatari katikati ya bahari,” akitoa wito kwa serikali, waajiri na jamii kubadilisha ahadi za uhamiaji kuwa hatua halisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *