USHINDI wa bao 1-0 uliyoipata Dodoma Jiji dhidi ya Mtibwa Sugar Mei 6, 2026, umemfanya kocha wa timu hiyo, Aman Josiah kusema umewaongezea morali ya kupambana zaidi na kuendelea kujiondoa katika presha ya kushika nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Alisema ili Dodoma Jiji iaanze kucheza mechi bila presha kubwa, inahitaji kufikisha alama 35 sawa na kushinda mechi mbili na kutoka sare moja kuanzia sasa, hivyo jambo la msingi ni kuhakikisha wanalinda kiwango chao ili kuyatafsiri malengo kuwa katika uhalisia.

“Mechi dhidi ya Mtibwa wachezaji walicheza kitimu, kiukomavu, kujituma na walionyesha pafomansi ya juu, kama kocha nitaendelea na kurekebisha baadhi ya vitu, mfano kuongeza nguvu katika kujilinda na kuimarika kila mechi,” alisema Josiah na kuongeza;

“Mfano tukifikisha alama 35 angalau tutakuwa eneo salama, hivyo Dodoma tunaweza kucheza bila presha na mpira ambao mashabiki watafurahia kuona burudani.”

Kocha huyo alisema viongozi wa timu hiyo wapo muda wote wanawaunga mkono na kila timu inaposhinda kuna pesa wanatoa kama motisha kwa wachezaji kuendelea kujituma na kuhakikisha wanashinda.

“Kusema ukweli hilo limesaidia sana wachezaji kupambana wakijua wanaposhinda kuna kifuta jasho,” alisema.

Katika mechi 21 ilizocheza Dodoma Jiji, imeshinda saba sawa na sare na ilizopoteza, inamiliki mabao 19, imeruhusu mabao 21 ikikusanya pointi 28.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *