• Chama cha Wamiliki wa Matatu kimezungumzia uvumi unaozidi kuenea kuhusu iwapo huduma za usafiri wa umma zitaathirika wakati wa maandamano ya Juni 25
  • Huku Wakenya wengi wakiwa na wasiwasi kuhusu jinsi maandamano yaliyopangwa yanaweza kuathiri usafiri, waendeshaji wa matatu sasa wametoa msimamo wao rasmi kuhusu utoaji wa huduma kote nchini
  • Taarifa ya sekta hiyo pia iligusia umuhimu wa maadhimisho hayo na haja ya kusawazisha uhuru wa kikatiba na amani pamoja na umoja wa kitaifa

Wakati Kenya ikijiandaa kwa siku ya kumbukumbu na maandamano, waendeshaji wa matatu wamejitokeza kutuliza hofu kuhusu uwezekano wa usumbufu katika huduma za usafiri.

Nairobi matatus
Chama cha Wamiliki wa Matatu kimewataka Wakenya kudumisha amani wakati wa maandamano ya Juni 25. Picha: UGC.
Source: Twitter

Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) kimewahakikishia Wakenya kuwa huduma za usafiri wa umma zitaendelea kama kawaida kote nchini mnamo Juni 25, licha ya wasiwasi unaohusiana na maandamano yaliyopangwa kuadhimisha miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z dhidi ya Mswada wa Fedha.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Juni 24, chama hicho kilikanusha taarifa za uwezekano wa kusimamishwa kwa huduma za usafiri na kuwahimiza abiria kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.

Pia soma

Hatua Kubwa ya Kidijitali: Wakenya Sasa Wapakua Vyeti vya Kuzaliwa Wakiwa Nyumbani

“Ingawa tunafahamu wasiwasi kuhusu uwezekano wa usumbufu, tunawahimiza wamiliki wote wa matatu, madereva, wahudumu na wafanyakazi kubaki watulivu, kujizuia na kuendelea kutoa huduma za usafiri kwa uwajibikaji na weledi,” chama hicho kilisema.

Je, usafiri wa umma utaendelea kama kawaida nchini Kenya mnamo Juni 25?

Mwenyekiti wa MOA, Albert Karakacha, alisema waendeshaji wa matatu wataendelea kuwa barabarani na kuhudumia abiria katika njia zote, akisisitiza kuwa hakuna mipango ya mgomo wa sekta nzima wala kusimamishwa kwa huduma.

“Sekta ya usafiri wa umma inaendelea kujitolea kuwahudumia Wakenya na kuwezesha usafirishaji wa watu na bidhaa. Kwa hivyo, shughuli za matatu zitaendelea kama kawaida huku tukiheshimu haki za kikatiba za wananchi wote na kuweka usalama wa umma mbele ya yote,” Karakacha alisema katika taarifa hiyo.

Wakati huo huo, chama hicho kilitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na wale ambao jamaa zao walijeruhiwa wakati wa maandamano ya Juni 25, 2024, yaliyotokea kote nchini kupinga Mswada wa Fedha.

Wamiliki wa matatu wataka maandamano ya Juni 25 yawe ya amani

Karakacha alibainisha kuwa Wakenya wana haki ya kikatiba ya kuadhimisha siku hiyo huku wakitaka uwajibikaji, lakini akasisitiza umuhimu wa haki, amani na umoja wa kitaifa.

Pia soma

“Acheni Kumshambulia Baba Yangu”: Sky Victor Amtetea Tash Kufuatia Madai ya Pesa

“MOA inalaani vikali aina zote za vurugu, uharibifu wa mali, uchomaji moto, uporaji na uharibifu wa mali za watu. Usalama na ustawi wa abiria, wafanyakazi wa usafiri, magari, biashara na umma kwa ujumla vinaendelea kuwa kipaumbele chetu kikuu,” chama hicho kilisema.

“Tunatoa wito kwa wadau wote, wakiwemo wananchi, viongozi wa jamii, asasi za kiraia, wafanyabiashara na mashirika ya serikali, kudumisha amani, kushiriki mazungumzo yenye tija, kuheshimu sheria na kushirikiana kutafuta suluhisho litakaloimarisha haki, uwajibikaji na umoja wa kitaifa.”

Matatus in Nairobi
Wahudumu wa Matatu wamewahakikishia Wakenya huduma zisizokatizwa mnamo Juni 25. Picha: Simon Maina.
Source: Getty Images

Murkomen alisema nini kuelekea maandamano ya Juni 25?

Uhakikisho huo umetolewa wakati wasiwasi unaongezeka kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na maandamano ya Jumatano kwa usafiri, biashara, shule na shughuli nyingine za kiuchumi.

Wakati huo huo, vyombo vya usalama vimeongeza kiwango cha maandalizi kuelekea maandamano yaliyopangwa kutokana na hofu kwamba wahalifu wanaweza kutumia maandamano ya amani kusababisha fujo na kuvuruga utulivu wa umma.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alitoa wito wa kufanyika kwa maandamano ya amani huku akiwaonya wanasiasa dhidi ya kuwatumia vijana kwa manufaa yao binafsi.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *