
Rais wa DRC alifungua mlango mnamo Mei 6, 2026, kwa muhula wa tatu unaowezekana kufuatia kura ya maoni ya kikatiba, na kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwaka 2028 ikiwa mzozo mashariki mwa DRC utaendelea.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Akiwa madarakani tangu mwaka 2019, Félix Tshisekedi, 62, atafikia mwisho wa muhula wake wa pili mnamo mwaka 2028. Katiba ya nchi hiyo inaweka kikomo cha mihula miwili ya rais. Matangazo haya yamesababisha hasira kutoka kwa vyama kadhaa vya upinzani, ambavyo vimesema ni hali isiyowezekana.
Siku ya Jumatano jioni, Félix Tshisekedi alisema kwamba yuko tayari kwa muhula wa tatu, ikiwa raia wa Kongo watampa nafasi hiyo. Vyama vya upinzani, nchini DRC na nje ya nchi, havikuchelewa kutoa maoni yao.
Hervé Diakiesé, msemaji wa chama cha Ensemble pour la République, aliyewasiliana na Patient Ligodi, alilaani: “Anadhai atasalia madarakani bila kuandaa uchaguzi [ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa rais, uliopangwa kufanyika mwaka 2028] kwa sababu Kivu Kaskazini na Kivu Kusini haziko tena chini ya udhibiti wa usalama wa serikali kuu. Lakini wakati huo huo, anasema bado anaweza kusalia madarakani kwa kubadilisha Katiba ili kupata muhula wa tatu usioeleweka, kulingana na kura ya maoni ambayo itaandaliwa kwa kuitenga mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini [mikoa ambayo sehemu zake zinadhibitiwa na kundi la kisiasa-kijeshi la AFC/M23]. Kwa hivyo, nia inaonesha imani mbaya na asili isiyo ya kikatiba ya mbinu yake.”
“Yuko njia panda”
Mwanasiasa huyo wa upinzani, kutoka chama cha Moïse Katumbi, ameongeza: “Vivyo hivyo, anadai kwamba Katiba inapaswa kubadilishwa kwa sababu ya mkataba na Marekani, ambao anasema unamlazimisha kufanya hivyo, na huo ni uongo mtupu. Amejikuta katika yuko njia panda: serikali inayodai kuwa huru, ikisema kwamba Katiba yetu ya sasa ni katiba ya kigeni, sasa itakubali kubadilisha Katiba kwa sababu tulisaini mkataba na wageni. Hakuna kifungu cha Katiba kinachoweza kubadilishwa kwa sababu tu tunasaini mikataba ya biashara.”
Rais wa muungano wa Lamuka, Martin Fayulu, akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa siku ya Alhamisi, alionya dhidi ya changamoto yoyote dhidi ya mchakato wa kidemokrasia: “Hana uwezo wa kuwapinga raia wa Kongo mwaka wa 2028. Ikiwa hakutakuwa na uchaguzi mwezi Januari 2029, ataondoka mamlakani,” alitangaza kwa mwandishi wetu huko Kinshasa, Pascal Mulegwa. “Tutafanya kinachowezekana. Tulimzuia Kabila kuwaia muhula wa tatu, na pia tutamzuia Félix Tshisekedi kuwania muhula wa tatu […]. Anataka kusalia madarakani kwa gharama ya raia wa Kongo.” »
Kiongozi huyo wa upinzani sasa anamshutumu Félix Tshisekedi kwa kuchochea vita hivi na anakataa wazo lolote la kuongeza muhula wake: “Masuala ya usalama mashariki yalikuwepo mwaka wa 2023, na aliandaa uchaguzi. Ikiwa kuna vita mashariki, anafanya nini kuimaliza? Ni kana kwamba alifanya makubaliano na Bw. Kagame ili kuigawanya Kongo kati yao. Anamwachia Kagame mashariki na kuchukua sehemu zingine za jamhuri.”
Francine Muyumba Nkanga, seneta wa zamani na mwanachama wa chama cha PPRD – chama cha rais wa zamani Joseph Kabila, aliyewekewa vikwazo na Marekani mwishoni mwa mwezi Aprili na kuhukumiwa kifo bila kuwepo na serikali ya Kinshasa mnamo mwezi Septemba 2025 – pia anabainisha kwamba kauli za Félix Tshisekedi zimejaa vitendawili na kinzani. “Katiba ya DRC iliwasilishwa na UDPS, chama cha Félix Tshiseked, kama katiba ya kigeni ambayo, kulingana na chama hicho, ilihitaji kubadilishwa kuwa ya Kikongo. Leo, Rais Tshisekedi anazungumzia mchakato wa kikatiba unaoendeshwa na nchi za nje. Kwa hivyo utata huu unaonyesha kashfa halisi ya kisiasa, kwa maoni yangu ya mazuri,” alibainisha katika mahojiano na Alexandra Brangeon.
“Kuhusu uchaguzi wa mwaka 2028, tunaambiwa leo kwamba haitawezekana kufanyika kwa sababu nchi iko vitani. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba muhula wa pili wa rais Tshisekedi ulipatikana haswa katika muktadha huu wa vita mnamo mwaka 2023. Bila kusahau kwamba pia alitaja uwezekano wa kufanyika kwa kura ya maoni ya kikatiba. Lakini mchakato kama huo unawezaje kufanyika huku ukitenga sehemu ya raia wa Kongo? Ikiwa kura ya maoni kuhusu Katiba inaweza kufanyika wakati wa vita, kwa nini uchaguzi unaokusudiwa kuruhusu kukabidhiana madaraka kidemokrasia utakuwa mgumu?” anauliza.
DRC na Rwanda zilitia saini makubaliano dhaifu ya amani huko Washington mapema mwezi Desemba chini ya usimamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambayo hayajamaliza mapigano mashariki ambapo makundi mengi yenye silaha wakati mwingine hutumiwa kama wasaidizi na pande zinazopigana. Mkataba huu unajumuisha sehemu ya kiuchumi inayolenga kuhakikisha kwamba tasnia ya teknolojia ya hali ya juu ya Marekani ina usambazaji wa madini ya kimkakati, ambayo yanapatikana nchini DRC.