
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema kuwa wizara yake imeanza mchakato wa kuangalia utaratibu wa kumpatia uraia nyota wa Simba SC, Clatous Chama, kufuatia bao lake zuri alilofunga dhidi ya Young Africans SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Major General Isamuhyo.
Makonda alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za wanamichezo bora wa mwaka za National Sports Council (NSC) iliyofanyika leo Mei 9, 2026 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
“Kwa lile goli zuri la Chama, wizara imeanza mchakato wa kuona taratibu za kumpatia uraia kwa lengo la kuongeza tija na nguvu katika timu yetu ya taifa. Chama ameonyesha uwezo mkubwa na ameweza kubadilika kulingana na wakati na mahitaji ya mchezo,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa uwezo wa Chama umeonekana wazi kutokana na kucheza kwa mafanikio katika vilabu vikubwa vya Tanzania.
“Bahati nzuri, Chama amechezea timu hizi mbili kubwa. Amechezea Yanga na kuonyesha uwezo wake, na pia ameichezea Simba na kufanya vizuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimechomekea tu, ukiona dokezo limekuja ofisini kwako, ujue ni sehemu ya uzalendo wa kuijenga Tanzania katika sura mpya ya dunia ya michezo,” aliongeza Makonda.
Hata hivyo Chama ni mchezaji halili wa Timu ya Taifa ya Zambia na kwa mujibu wa taratibu za Fifa hawezi kuchezea Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwasababu tayari amemecheza michezo rasmi ya timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo).