Ngara. Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka pamoja na Kituo cha Kupoza Umeme cha Benaco, hatua inayotarajiwa kuiunganisha Mkoa wa Kagera katika Gridi ya Taifa.

Jiwe la msingi la mradi huo limewekwa leo Mei 9, 2026 katika eneo la Benaco wilayani Ngara na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ndejembi amesema Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh270 bilioni na utakamilika ndani ya miezi 24.

“Leo tupo hapa kudhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika. Ili huduma ya umeme iwafikie wananchi hadi vitongojini ni lazima kuwe na miundombinu imara ya kusafirisha na kupooza umeme,” amesema Ndejembi.

Ameeleza kuwa njia hiyo mpya ya umeme yenye msongo wa kilovolti 220 ina uwezo mkubwa zaidi ikilinganishwa na laini ya sasa ya kilovolti 132 inayopokea umeme kutoka nchini Uganda, hatua itakayosaidia Mkoa wa Kagera kuingia rasmi katika Gridi ya Taifa.

“Tunatarajia ndani ya miezi 24 Mkoa wa Kagera uwe umeunganishwa katika Gridi ya Taifa na changamoto za umeme kwa wananchi ziwe historia,” amesema.

Waziri huyo pia ameuagiza uongozi wa Tanesco kuhakikisha wananchi hawaendelei kusubiri huduma ya umeme kwa muda mrefu kwa kutafuta transfoma kubwa zitakazosaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea.

Aidha, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati huku wakitoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika pamoja na kulipa fidia stahiki kwa waliopisha utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema mradi huo umetengewa dola za Marekani milioni 105.6 sawa na zaidi ya Sh279 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo miwili.

Amesema tayari wakandarasi wote wamelipwa malipo ya awali ili kuanza kazi huku zaidi ya Sh1.7 bilioni zikiwa tayari zimetolewa katika awamu ya kwanza ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi.

Twange amesema maeneo ya Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini pamoja na Manispaa ya Bukoba kwa sasa yanapata umeme kutoka Uganda kupitia laini ya kilovolti 132 kutoka Masaka hadi Kituo cha Kupooza Umeme cha Kyaka.

“Mradi huu utaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kusaidia kukuza shughuli za kiuchumi na uzalishaji katika Mkoa wa Kagera,” amesema.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Zuhura Bundala amesema mradi huo utafungua fursa mbalimbali za maendeleo kwa wananchi wa Kagera kupitia ongezeko la shughuli za uzalishaji mali, ajira kwa vijana pamoja na kuinua kipato cha wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Mathias Kahabi amesema vijiji vyote 75 vya Jimbo la Ngara tayari vimefikiwa na huduma ya umeme huku vitongoji 219 kati ya 389 vikiwa tayari vimeunganishiwa umeme.

Akihitimisha hafla hiyo, Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya nishati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na ya uhakika pamoja na mazingira mazuri ya kufanya shughuli za maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *