Mbeya. Baada ya kimya cha zaidi ya mwaka mmoja, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa kinatarajia kufanya mkutano wake wa hadhara huku mwenyekiti wa kanda hiyo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akitaja mambo manne yatakayojadiliwa.

Mkutano huo unatarajia kufanyika kesho Jumapili Mei 10, 2026 katika soko la Igawilo lililopo katika Jimbo la Uyole linaloongozwa na Spika msitaafu, Dk Tulia Ackson (CCM) huku viongozi mbalimbali wakitarajia kushiriki.

Mara ya mwisho Sugu kuhutubia katika mkutano wa hadhara ilikuwa Machi 23, 2025 alipoambatana na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, akiwamo Mwenyekiti Tundu Lisu na Makamu Mwenyekiti, John Heche jijini Mbeya katika kampeni ya ‘No Reforms No Election’.

Hata hivyo, Chadema ilifungiwa kufanya shughuli za kisiasa na Mahakama Kuu Tanzania kufuatia uwapo wa kesi ya mgawanyo wa mali za chama na baadhi ya makada wa chama hicho kabla ya kufunguliwa Aprili 15, 2026 kuendelea na shughuli zao.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 9, 2026, Sugu amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo utakaoanza saa 6 mchana akisisitiza kuwa taratibu zote za mkutano huo zimefanyika na hakutakuwapo changamoto yoyote.

Amesema katika mkutano huo, viongozi mbalimbali wa Kanda na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla watakuwapo huku wakiwasilisha agenda nne zenye uzito kwa mustakabali wa Taifa na kwamba wamejipanga kuendeleza walipoishia.

“Chadema ndio sauti ya wananchi, ndio tunagusa maisha yao na kesho tunatarajia mkutano wetu kufanyika baada ya kuzuiwa kwa muda mrefu, viongozi wa Kanda, majimbo, Wilaya na Mkoa watakuwapo,” amesema na kuongeza:

“Tutazungumzia masuala ya nchi kisiasa, kimaisha, uchumi na usalama wa wananchi, maandalizi yamekamilika na taratibu zote zimefuatwa kwa vyombo vyote husika, niwaombe wananchi waje kwa wingi,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Mbeya mjini.

Naye, mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Masaga Karoli amesema watatumia hadhara hiyo kuzindua rasmi mkutano wa Chama Mkoa akieleza kuwa wanayo mengi ya kuzungumza na wananchi baada ya kuwapoteza muda mrefu.

“Tunatarajia hali ya amani na usalama kwakuwa viongozi wetu wa majimbo wamefanyia kazi, tunayo mambo mengi ya kuzungumza na wananchi kwakuwa ni muda mrefu, tutatumia muda huo kuzindua rasmi mikutano mingine ya Mkoa,” amesema Masaga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha) Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya amesema mkutano huo ni mahsusi kwa vijana katika kudai haki, amani, katiba mpya na kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Lissu.

Amesema mkutano huo utakuwa mwanzo wa kampeni ya kudai mambo hayo na kwamba jambo la Chama ni la vijana na jambo la Vijana ni la chama hivyo watakuwa msitali wa mbele kupambania ili haki ipatikane.

“Ndio maazimio ya Kamati Kuu kwa Chama, sisi vijana tunahitaji mambo mawili makubwa, Katiba mpya na kuachiwa huru kwa kiongozi wetu Lissu, lakini tunataka haki na amani kwa Taifa letu,” amesema Chonya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *