Chanzo cha picha, PA Media
Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer amesisitiza kuwa hatajiuzulu na “kuitumbukiza nchi kwenye mgogoro,” wakati chama cha Labour kikikabiliwa na hasara kubwa katika uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi nchini England, Scotland na Wales yameongeza shinikizo kwa Sir Keir, huku baadhi ya wabunge wa Labour wakimtaka kuweka ratiba ya kuondoka kwake madarakani, ingawa kwa sasa washirika wake wa baraza la mawaziri wanaendelea kumuunga mkono.
Labour imepoteza madaraka nchini Wales, na hivyo kumaliza utawala wake wa miaka 27, huku chama cha SNP kikiendelea kuwa chama kikubwa zaidi nchini Scotland.
Chama cha Reform UK ndicho kilichopata mafanikio makubwa zaidi nchini England, kikitwaa zaidi ya viti 1,400 na kuchukua udhibiti katika maeneo ambayo kihistoria yalitawaliwa na Labour na Conservatives.
Chama cha Labour kimepoteza zaidi ya viti 1,100 vya halmashauri nchini England, ikiwemo katika ngome zake za kisiasa kaskazini mwa England na maeneo ya Midlands, na kinatarajiwa kukumbana na matokeo mengine magumu.