Wakati dunia ikiadhimisha siku ya mama leo, mijadala ya upendo, heshima na shukrani kwa kinamama imeshika kasi katika familia, taasisi na mitandao ya kijamii.

Kusherehekea siku hii baadhi ya watu walijandaa kwa maua, zawadi, kadi za pongezi na jumbe za upendo kwa mama zao huku mitandao ya kijamii ikiwa imesheheni picha za kinamama walio hai au hata wale waliokwisha kuaga dunia.

Hata hivyo, nyuma ya mandhari hiyo ya sherehe kuna picha nyingine ya maisha ya kila siku ya mama wa kisasa picha ya uchovu, majukumu yasiyoisha na mzigo wa kihisia unaobebwa kimya kimya.

Katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, mama wa sasa ameendelea kuwa nguzo ya familia nyingi licha ya changamoto zinazoongezeka kila siku. Lakini nyuma ya nguvu hiyo, kuna simulizi ya uchovu wa kimya unaohitaji kusikilizwa na kushughulikiwa kwa dhati.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya kijamii na afya ya akili, mama wa sasa amebeba majukumu mengi zaidi kuliko vizazi vilivyopita, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, ongezeko la gharama za maisha na mabadiliko ya mfumo wa familia.

Maisha ya haraka, majukumu yasiyoisha

Kwa kina mama wengi mijini, siku huanza mapema na kuisha usiku wa manane.

Ni safari ya kuandaa watoto kwenda shule, kwenda kazini, kurudi nyumbani, kupika, kusimamia masomo ya watoto na wakati mwingine kuendelea na shughuli za ziada za kujiongezea kipato.

“Ninapoamka saa kumi na moja alfajiri, tayari kichwani nina orodha ya mambo zaidi ya kumi ya kufanya siku hiyo. Tatizo si kazi moja, ni mkusanyiko wa kila kitu,” anasema Halima Juma, mama wa watoto watatu mkazi wa Temeke, Dar es Salaam.

Anasema licha ya kufanya kazi rasmi, bado anabeba jukumu kubwa la nyumbani ambalo mara nyingi halina mapumziko.

“Kuna wakati najiuliza, mama anapata lini muda wake binafsi? Lakini ukweli ni kwamba mara nyingi hatupati,” anasema Halima.

Kwa upande wake, Rehema Mally, mkazi wa Mbagala na mama wa watoto wawili, anasema changamoto kubwa kwa mama wengi wa sasa ni kubeba mzigo wa kihisia huku wakijitahidi kuonekana wenye nguvu muda wote.

“Unakuta mtoto ana matatizo shuleni, mume ana changamoto zake, gharama za maisha zimepanda lakini bado jamii inatarajia mama awe mtulivu kila wakati. Kuna siku unachoka kiakili lakini huna nafasi hata ya kusema umechoka,” anasema.

Mzigo usioonekana wa mama

Mwanasaikolojia Neema Mwakalukwa anasema changamoto kubwa inayowakumba wanawake wengi si kazi wanazofanya tu, bali ni kile kinachoitwa “mental load” mzigo wa kufikiria na kupanga kila kitu kinachohusu familia.

“Mama ndiye anayekumbuka kila kitu ratiba za watoto, mahitaji ya nyumbani, afya ya familia na hata mahusiano ya kifamilia. Hii ni kazi ya akili ambayo haipati mapumziko,” anasema Neema.

Anasema hali hiyo huweza kusababisha uchovu wa muda mrefu, msongo wa mawazo na wakati mwingine kupoteza furaha ya maisha bila mtu mwenyewe kutambua haraka.

Naye Neema Charles, mama anayejishughulisha na biashara ndogo Kariakoo, anasema mara nyingi mchango wa mama ndani ya familia hauonekani kwa sababu umezoeleka.

“Mama akifanya kila kitu nyumbani inaonekana ni kawaida. Lakini siku akiumwa au akishindwa kufanya majukumu ndipo watu wanaona umuhimu wake. Tunahitaji kuthaminiwa kila siku, si siku moja tu kwa mwaka,” anasema.

Shinikizo la kuwa mama mkamilifu

Katika miaka ya hivi karibuni, mitandao ya kijamii imeongeza changamoto mpya kwa kinamama wengi. Picha za maisha “kamili” mtandaoni zimeweka kiwango kipya cha matarajio ya jamii.

Mama anatarajiwa kuwa na nyumba safi kila wakati, watoto wenye nidhamu, kazi inayoendelea vizuri na ndoa yenye furaha, huku yeye mwenyewe akionekana akiwa na tabasamu muda wote.

Mshauri wa masuala ya familia, Happiness Mrema, anasema hali hiyo imeongeza presha kwa wanawake wengi wanaojilinganisha na maisha wanayoona mtandaoni.

Anasema shinikizo hilo limechangia ongezeko la msongo wa mawazo kwa baadhi ya wanawake, hasa vijana wanaoanza maisha ya ndoa na malezi.

“Wengi hawaoni uhalisia wa nyuma ya picha. Matokeo yake wanajiona kama hawatoshi au hawafanyi vya kutosha,” anasema Hapiness.

Kauli hiyo inaungwa mkono na baadhi ya kinamama waliozungumza na gazeti hili kuhusu changamoto wanazopitia katika maisha ya kila siku.

Mariam Abdallah, mama wa mtoto mmoja na mkazi wa Kigamboni, anasema mara nyingi hujikuta akijilaumu anapoona maisha ya wengine mtandaoni yakionekana kuwa bora zaidi kuliko yake.

“Unaingia Instagram unaona mama mwenzako ameandaa kila kitu vizuri, watoto wanang’aa, nyumba safi. Ukirudi kwenye maisha yako ya kawaida unajisikia kama wewe hupambanii familia yako vya kutosha, kumbe kila mtu ana changamoto zake,” anasema Mariam.

Kwa upande wake, Esther Mushi, mama wa watoto wawili kutoka Ubungo, anasema presha ya kutaka kuonekana mwenye furaha kila wakati imekuwa changamoto kubwa kwa kinamama wengi.

“Kuna siku umechoka, una mawazo, lakini bado unaona lazima uweke picha ukionekana sawa kwa sababu jamii imezoea kuona mama akiwa imara muda wote,” anasema Esther.

Naye Janeth Kweka, mfanyabiashara mdogo wa Kariakoo, anasema mara nyingi mitandao ya kijamii huwafanya wanawake kusahau kuwa maisha ya mtandaoni si halisi kwa asilimia zote.

“Tunajilinganisha sana na watu tusiojua maisha yao ya kweli. Wengine wana msaada mkubwa nyuma yao lakini sisi tunaangalia tu picha nzuri na kujiona tumeshindwa,” anasema Janeth.

Familia na mgawanyo wa majukumu

Katika baadhi ya familia, bado kuna changamoto ya mgawanyo wa majukumu ya nyumbani, ambapo wanawake hubeba sehemu kubwa ya kazi za malezi hata pale wanapokuwa wanafanya kazi nje ya nyumba.

Mchambuzi wa masuala ya jamii, Bakari Mfaume, anasema hili ni tatizo la mtazamo ambalo linahitaji kubadilika.

“Malezi ya watoto na uendeshaji wa nyumba si jukumu la mama pekee. Ni jukumu la wazazi wote wawili.Watoto wanafaidika pia wanapoona ushirikiano wa wazazi wao,” anasema.

Mfaume anabainisha kuwa familia zinazoshirikiana hupunguza mzigo kwa mama na kuongeza mshikamano wa kifamilia.

 Afya ya akili ya mama

Wataalamu wa afya wanasema kuna ongezeko la changamoto za afya ya akili miongoni mwa kinamama, ikiwemo msongo wa mawazo, uchovu wa kudumu na wakati mwingine dalili za huzuni ya muda mrefu.

Neema anasema baadhi ya wanawake hupitia hali hizi kimya kimya bila kupata msaada wa kitaalamu.

“Jamii bado haijaweka kipaumbele cha kutosha kwenye afya ya akili ya mama. Wengi huambiwa tu wavumilie,” anasema.

Anasisitiza kuwa msaada wa kihisia, mapumziko na ushirikiano wa familia, ni muhimu katika kulinda afya ya mama.

Mama wasioonekana

Katika simulizi nyingi za mafanikio ya familia, mama huonekana kama nguzo kuu, lakini mara nyingi mchango wake wa kila siku hauzungumzwi kwa kina.

Wataalamu wanasema hii ni moja ya sababu zinazofanya mzigo wa mama uendelee kuwa wa kimya, kwa sababu jamii imezoea kuuchukulia kama jambo la kawaida.

“Mara nyingi tunasherehekea matokeo ya kazi ya mama lakini hatuulizi alilipa gharama gani kufikia hapo,” anasema Mfaume.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *