
Dar es Salaam. Wakati Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikiendelea kuandika historia katika huduma za uzazi pandikizi (IVF), madaktari wake wanasema changamoto kubwa walizokutana nazo katika awamu za mwanzo za huduma hiyo, ni ubora hafifu wa mbegu za wanaume na idadi kubwa ya wanawake wanaofika hospitalini wakiwa wamechelewa umri wa uzazi.
Imefafanua kuwa wanaume wawili kati watatu wanaofika na wenza wao kwa ajili ya huduma za IVF, mbegu zao zinakuwa hafifu na mmoja anayesalia tatizo linakuwa kwa mwenza wake.
Huduma ya IVF Muhimbili ilifunguliwa Septemba 2024 na kuanza kupokea wahitaji wa mwanzo Desemba mwaka 2024 baada ya kuanzishwa kwa kituo hicho.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, ambaye pia ni mtaalamu wa uzazi pandikizi MNH, Matilda Ngarina anasema tangu kuanza kwa huduma hiyo, tayari wanawake 26 wamefanyiwa hatua ya kuvunwa mayai kwa ajili ya IVF.
“Tumeshafanya upandikizaji kwa wanawake wanane, kijusi (kiinitete) baada ya kurutubishwa maabara; na upandikizaji wa kijusi kilichogandishwa kwa wanawake 10.
Kwa wale wanane ni pale ambapo mayai yanarutubishwa na kurejeshwa tumboni kwa mama ndani ya mzunguko ule ule, wakati hawa 10 ni pale ambapo viinitete vinawekwa kwenye ubaridi maalumu na kupandikizwa baadaye mwilini kwa mama,” anasema.
Hata hivyo, nyuma ya mafanikio hayo, Dk Ngarina anasema wamekutana na picha halisi ya changamoto za uzazi nchini, hasa kwa wanaume.
“Ukifanya tathmini ya wagonjwa tunaowaona, karibu theluthi mbili ya matatizo yanatoka kwa wanaume. Tunakuta hakuna mbegu kabisa, au zipo lakini ni chache, hazitembei vizuri, zina vichwa vibovu au mikia mibovu,” anasema.
Anaeleza kuwa baadhi ya wanaume wanaonekana wenye afya njema, lakini vipimo vinaonyesha hawana mbegu kabisa katika manii zao.
“Unaweza ukaangalia mbegu leo, ukirudi baada ya muda mfupi unakuta nyingi zimekufa. Ubora wa mbegu za wanaume unapungua sana na bado dunia haijaelewa vizuri chanzo chake,” anasema.
Kwa mujibu wa daktari huyo, mtindo wa maisha ni sehemu ya tatizo hilo.
“Pombe, sigara, matumizi ya dawa za kulevya, msongo wa mawazo, kukosa usingizi na hata mavazi yanayobana sehemu za siri, ni vitu vinavyoathiri ubora wa mbegu,” anasema.
Anasema baadhi ya wanaume hulazimika kufanyiwa upasuaji au matibabu maalumu chini ya wataalamu wa mfumo wa uzazi wa wanaume, huku wengine wakihitaji kubadili kabisa maisha yao ya kila siku kabla ya kufikia hatua ya IVF.
Changamoto kwa wanawake
Kwa upande wa wanawake, Dk Ngarina anasema changamoto kubwa wanayoiona sasa ni wanawake wengi kufika hospitalini wakiwa wamechelewa umri wa uzazi.
“Asilimia kubwa ya wanawake tunaowaona wana miaka zaidi ya 40 au wanakaribia huko. Wengi wamechelewa kupata watoto kwa sababu ya masomo, kazi au maisha kwa ujumla,” anasema.
Anasema baadhi ya wanawake wanafika hospitalini wakiwa tayari wameingia kwenye dalili za ukomo wa hedhi.
“Tunawaona wanawake wa miaka 34, 35 au 36 tayari mayai yao yamepungua sana au yameisha kabisa. Hii ni changamoto kubwa sana siku hizi,” anasema.
Anasema wanawake wengi huchelewa kutafuta msaada wa kitabibu wakiamini bado wana muda wa kupata watoto.
“Wengi wanaamini watazaa wakati wowote, lakini ukweli ni kwamba ubora wa mayai unapungua kadri umri unavyoongezeka,” anasema.
Mbali na umri, Dk Ngarina anataja magonjwa matatu makubwa yanayochangia ugumba kwa wanawake kuwa ni ugonjwa wa vinyama vingi kwenye ovari au ugonjwa wa mayai mengi yasiyopasuka kwenye ovari, ugonjwa wa utando wa kizazi kukua nje ya kizazi na kushindwa kufanya kazi kwa ovari au ovari kupoteza uwezo wa kuzalisha mayai.
Anafafanua kuwa ugonjwa mayai kushindwa kupasuka husababisha yashindwe kutoka kwenye ovari kila mwezi.
“Yanatengenezwa, lakini hayapasuki kutoka nje kwenda kukutana na mbegu za mwanaume. Badala yake yanabaki kujikusanya ndani ya ovari,” anasema.
Wanawake wenye tatizo hilo, anasema wanaweza kuwa na mayai mengi kwenye vipimo vya ultrasound, lakini mengi yakawa hayana uwezo wa kurutubishwa.
“Unaweza kufurahi kuona mayai ni mengi kumbe ukienda kuvuna unakuta ni matupu,” anasema.
Anasema endometriosis (utando kutoka nje ya kizazi) nayo imekuwa tatizo kubwa linalowapa wakati mgumu madaktari wa uzazi nchini.
“Huu ni ugonjwa mgumu sana. Utando wa ndani ya kizazi unatoka nje ya kizazi na kwenda sehemu nyingine tumboni. Kila mwanamke anapopata hedhi, sehemu zote hizo nazo zinavuja damu,” anasema.
Anasema hali hiyo husababisha viungo vya ndani kushikamana na kuathiri ubora wa mayai pamoja na uwezo wa mimba kushika.
“Tumeshawahi kutoa mayai kwa wagonjwa wenye endometriosis lakini hata mayai ya kurutubishwa hayakupatikana,” anasema.
Licha ya changamoto hizo, Muhimbili tayari imefanikisha kuzaliwa watoto watatu kupitia IVF tangu huduma hiyo kuanza.
Dk Ngarina anasema mmoja wa wanawake waliofanikiwa, alipata ujauzito katika jaribio la kwanza baada ya kukaa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka minane bila mtoto.
“Tatizo lake lilikuwa mirija ya uzazi kuziba, lakini mayai yake yalikuwa mazuri na mume wake hakuwa na shida ya mbegu. Tuliporutubisha mayai na kupandikiza, mimba ilishika mara moja,” anasema.
Usiri nao tatizo
Hata hivyo, Dk Ngarina anasema changamoto nyingine kubwa ni wagonjwa wengi kutotaka jamii ijue wamepata watoto kwa njia ya IVF kutokana na unyanyapaa uliopo kuhusu ugumba.
“Wengi hawataki hata ndugu zao wajue wamefanya IVF. Kuna wagonjwa tulihifadhi siri zao mpaka wakati wa kujifungua,” anasema.
Kutokana na hilo, baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakitaka kutibiwa kwa usiri mkubwa, kiasi kwamba hawataki hata wauguzi kuwafahamu historia zao.
“Ugumba una unyanyapaa mkubwa sana katika jamii yetu,” anasema.
Safari ndefu ya IVF
Dk Ngarina wanasema safari ya uzazi pandikizi (IVF) ni ndefu, yenye gharama kubwa na isiyo na uhakika wa mafanikio kwa kila anayeanza matibabu.
Anasema tofauti na watu wengi wanavyodhani, IVF si matibabu ya siku moja bali ni mchakato unaohitaji maandalizi ya muda mrefu kabla ya kupandikiza kijusi tumboni kwa mama.
“Tunamwandaa mama kwa karibu mwezi mzima kwa kutumia dawa maalumu, kisha akipata hedhi tunaanza sindano za siku 14 za kuchochea mayai yakue na kupevuka,” anasema.
Katika kipindi hicho, madaktari hufuatilia ukuaji wa mayai kwa kutumia vipimo vya ultrasound kabla ya kuyavuna kupitia uke kwa kutumia vifaa maalumu katika usingizi.
Hata hivyo, anasema matokeo kwa wanawake kuhusu hatua hiyo hutofautiana.
“Kuna mama anatoa mayai manne, mwingine 30 na mwingine hapati yai lolote,” anasema.
Baada ya mayai kuvunwa, hupelekwa maabara kwa ajili ya kurutubishwa kwa kutumia mbegu za mwanaume. Viinitete vinavyopatikana hufuatiliwa kwa siku tatu ndani ya mashine maalumu za kuhifadhi viinitete (incubator) kabla ya kupandikizwa.
“Siku ya tatu tunaangalia ni mayai mangapi yamekuwa vijusi na tunaviwekea madaraja ya ubora,” anasema.
Anasema si wanawake wote wanaoruhusiwa kupandikizwa mara moja. Wale wanaotoa mayai mengi hulazimika kusubiri kutokana na hatari ya kupata ugonjwa wa kuchochewa kupita kiasi kwa ovari, kunakosababishwa na ongezeko la homoni mwilini.
“Tunafreeze (tunagandisha) vijusi kwanza mpaka mwili urudi kawaida,” anasema.
Dk Ngarina anasema baadhi ya wanawake huanza matibabu lakini mayai yanakuwa matupu, hayarutubishwi au yanageuka kuwa vijusi dhaifu visivyofaa kupandikizwa.
“Hakuna uhakika kwamba ukishatoa mayai lazima upate mtoto,” anasema.
Changamoto nyingine, anasema wagonjwa wengi wanaofika Muhimbili huwa tayari wamezunguka hospitali nyingi bila mafanikio na wengi wao huwa wamechelewa umri wa uzazi.
“Tunapata wanawake wengi wenye zaidi ya miaka 40. Wengine wana miaka 60 na bado wanataka mtoto wao wa kwanza,” anasema.
Anasema ni takribani asilimia 20 tu ya wagonjwa wanaofika wakiwa kwenye umri mzuri wa uzazi.
Anasema baadhi ya wenye matzo ya uzazi hushauriwa kutumia mayai ya wafadhili, jambo linaloongeza gharama za matibabu.
Hadi sasa, Muhimbili imefanikiwa kufanya upandikizaji wa vijusi moja kwa moja na vilivyogandishwa, ambapo wanawake wawili wamepata ujauzito. Mmoja alijifungua mtoto kupitia vijusi visivyogandishwa; mwingine alijifungua watoto pacha kupitia vijusi vilivyogandishwa lakini walifariki dunia na wajawazito wengine wawili wanaendelea vizuri.
Dk Ngarina anasema kiwango cha mafanikio ya IVF duniani ni wastani wa asilimia 40 na hutegemea chanzo cha tatizo la uzazi pamoja na umri wa mgonjwa.
Kuhusu gharama, anasema mzunguko mmoja wa IVF Muhimbili hugharimu takribani Sh14 milioni, ikihusisha kuchochea mayai, kuvuna, kurutubisha, kupandikiza na kuhifadhi viinitete kwa mwaka mmoja.
“Bado ni gharama kubwa kwa Mtanzania wa kawaida kwa sababu dawa nyingi huagizwa kutoka nje na ni ghali,” anasema.
Anasema maandalizi ya kuanzisha huduma hiyo yalianza mwaka 2018 lakini yalicheleweshwa na changamoto mbalimbali ikiwamo janga la Uviko-19.
“Sasa kazi kubwa ni kuhakikisha huduma hizi zinawafikia Watanzania wengi zaidi kwa gharama nafuu,” anasema.
Itaendelea kesho…