Dodoma. Shirika la AGRA limeanza kutoa mafunzo maalum ya uchambuzi wa hatari za mabadiliko ya tabianchi kwa wadau wa sekta ya kilimo nchini, katika hatua inayolenga kusaidia Tanzania kujenga mifumo ya kilimo na chakula inayoweza kustahimili athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu Climate Vulnerability Mapping and Risk Analysis yanafanyika jijini Dodoma yakihusisha wataalamu wa kilimo, mazingira, taasisi za maendeleo pamoja na wadau wa sekta ya chakula na kilimo.
Sambamba na mafunzo hayo, AGRA imezindua mwongozo unaojulikana kama A User Guide to AGRA’s Climate Vulnerability Assessment Tool (ClimVAT) unaolenga kuwasaidia wadau kutumia taarifa za tabianchi katika kupanga sera, uwekezaji na afua mbalimbali za maendeleo ya kilimo.
Kupitia mfumo wa ClimVAT, wadau wanaweza kuchambua maeneo yaliyo katika hatari kubwa ya ukame, mvua zisizoeleweka, joto kali pamoja na changamoto nyingine zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula.
Mfumo huo unaunganisha taarifa za hali ya hewa, udongo, uzalishaji wa mazao pamoja na takwimu za kijamii na kiuchumi ili kusaidia kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji na mipango ya kukabiliana na athari za tabianchi.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Ofisa kutoka Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya mazingira, Hassani Issa, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta ya kilimo.
“Serikali ipo karibu na wadau mbalimbali katika kupambana na mabadiliko hatarishi ya tabianchi. AGRA ni miongoni mwa wadau, na tupo hapa kama sehemu ya kufuatilia na kuunga mkono juhudi hizi za kusaidia kilimo Tanzania,” amesema Issa.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo, Profesa John Jeckoniah, amesema matumizi ya taarifa za tabianchi ni muhimu katika kupanga shughuli za kilimo kutokana na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yanayoendelea kujitokeza.
“Leo hatuwezi tena kupanga kilimo kwa mazoea. Lazima tufanye maamuzi kwa kutumia taarifa za tabianchi, data na uchambuzi wa kisayansi ili kujua maeneo yaliyo hatarini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mapema,” amesema Profesa Jeckoniah.
Naye Ofisa Miradi kutoka shirika la RUCODIA, Palesia Waziri, amesema taarifa sahihi za tabianchi zitasaidia kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye changamoto kubwa zaidi.
“Taarifa sahihi za tabianchi zinatusaidia kuelewa wapi pa kupeleka rasilimali na namna ya kubuni afua zinazoweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Waziri.
Ofisa Miradi wa AGRA Tanzania, Japhet Laizer, amesema matumizi ya mifumo ya kidigitali na takwimu ni muhimu katika kujenga ustahimilivu wa mifumo ya chakula dhidi ya athari za tabianchi.
“ClimVAT inasaidia kugeuza data za tabianchi kuwa taarifa zinazoweza kutumika moja kwa moja katika kupanga uwekezaji, sera na hatua za kujenga kilimo himilivu nchini,” amesema Laizer.
Kwa mujibu wa AGRA, matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta ya kilimo yanaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula.