
Mwanza. Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Barnabas Mtokambali, amewataka watoa huduma za afya kuzingatia maadili ya taaluma yao, kutoa huduma bora na kutumia ipasavyo vifaa vya kisasa ili kutoa huduma kwa ubora unaohitajika.
Askofu Mtokambali amesema hayo Mei 10, 2026, wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Royal Zonal Referral Hospital, uliofanyika eneo la Ghana, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Amesema watoe huduma kwa kuzingatia ubora, utu na huruma wanapowahudumia wagonjwa ili kutimiza maneno ya Mwenyezi Mungu.
“Ningependa kusisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma, ubora wa huduma, matumizi sahihi ya vifaa vya kisasa pamoja na kuwahudumia wagonjwa kwa utu, huruma na uadilifu kama neno la Mungu linavyotutaka,” amesema.
Ameyataja mambo matano ya kuzingatiwa na watoa huduma za afya, moja likiwa ni kufanya kazi kwa bidii na uaminifu; pili, kuwa na moyo wa huduma; na tatu, kutafuta ubora katika kila jambo.
Jambo jingine amesema kazi ya hospitali ni utumishi mbele za Mungu na kwamba lolote wafanyalo watawajibika mbele za Mungu. Ameongeza kuwa afya ya mwanadamu ni jambo nyeti linalohitaji moyo wa kujituma na weledi.
Askofu Mtokambali amesema pia wananchi watumie hospitali vizuri kwa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara, ili kuzuia magonjwa kabla hayajatokea au kabla hayajawa makubwa.
Royal Hospital ilisajiliwa Machi 9, 2020 kama hospitali ya wilaya, na Machi 16, 2026 ilipewa kibali cha kufanya kazi kama hospitali ya kanda ikiwa na huduma za kisasa na vifaa vya teknolojia ya juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Glory Joseph, amesema hospitali hiyo inatoa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi kwa kutumia vifaa vya kiteknolojia, ikiwemo X-Ray na CT Scan inayotumika kugundua magonjwa ya saratani, uvimbe na damu kuvuja ndani ya mwili.
“Huduma nyingine ni chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), chumba cha watoto wachanga mahututi (NICU), huduma ya mochwari, huduma za dharura na ajali pamoja na huduma za VIP,” amesema.
Dk Glory akisoma hotuba kwa mgeni rasmi amesema hospitali hiyo imekuwa na maendeleo makubwa, na kwa sasa ina jengo la ghorofa 10, likiwa na vitanda 80, vyumba vya upasuaji vitano, na wafanyakazi zaidi ya 300.
Baadhi ya wadau wamesema hospitali hiyo itawapunguzia gharama za kusafiri kwenda nje ya nchi kwa matibabu, hasa wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
Tuse Mwaikasu, dada wa familia, amesema: “Wananchi wa Mwanza sasa wataenda kupata huduma nyingi tofauti na awali, na hawatohangaika kwenda Muhimbili au Ocean Road, bali watatibiwa hapa hapa, na itapunguza mzigo kwa Hospitali ya Bugando kama itatokea imezidiwa na idadi ya wagonjwa.”
Mchungaji Martina Kabisama amesema: “Mgonjwa anapotibiwa na kupona, kunywa dawa pekee haitoshi, bali mazingira na huduma inayotolewa na watoa huduma inachangia.”
Moses Muhumuza, mhasibu wa kujitegemea mkoani Mwanza, amesema: “Wataalamu watakuwepo na kila kitu kitapatikana hapa, na gharama za matibabu kweli zitakuwa chini na nafuu kwa wananchi.”