
Dar es Salaam. Wakulima walio katika vyama vya ushirika wako mbioni kuondokana na changamoto ya upotevu wa mazao baada ya mavuno, kufuatiwa kusainiwa kwa mkataba wa ushirikiano kati ya Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) na Agra.
Mkataba huo wa makubaliano wa miaka mitano unalenga la kuchochea matumizi ya zana na teknolojia za kisasa katika kilimo, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuimarisha mifumo ya chakula hapa nchini Tanzania huku wakulima wakipata hadi ruzuku ya asilimia 30 katika mikopo ya zana za uhifadhi mazao.
Programu hiyo iliyopewa jina la Re-Gain imeundwa kushughulikia upotevu wa chakula baada ya mavuno huku ikiimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia uhamasishaji, kujenga uwezo, pamoja na matumizi ya teknolojia bunifu za kupunguza upotevu wa chakula kupitia mikopo.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo jijini Dar es Salaam leo Mei 12, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop benki, Godfrey Ng’urah amesema ushirikiano huo unaendana na dhamira ya muda mrefu ya benki katika kuimarisha usalama wa chakula, ufadhili endelevu pamoja na kuwawezesha wakulima nchini Tanzania.
“Usalama wa chakula na ufadhili endelevu ni sehemu muhimu ya Dira yetu ya 2030, huku sekta ya kilimo ikichangia zaidi ya asilimia 60 ya mikopo yetu. Baada ya miezi kadhaa ya majadiliano yenye tija, tunafurahia kurasimisha ushirikiano huu na Agra,” amesema.
Amesema mkataba huu unaashiria hatua muhimu katika dhamira ya pamoja ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima wa Tanzania.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utachangia kwa kiasi kufanikisha azma ya benki ya kufikia familia milioni 10 ifikapo mwaka 2030, hasa wakati huu ambapo zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanategemea kilimo kama chanzo chao kikuu cha maisha.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Benki ya Ushirika kwa kushirikiana na Agra itawasaidia wakulima wadogo nchini, wakianzia na mikoa 11 ya kimkakati ambayo ni kapu la chakula (food basket) ikiwemo Katavi, Iringa, Morogoro na Mbeya.
Amesema kwa pamoja wamedhamiria kufanya mapinduzi yatakayosaidia kufanikisha Dira ya 2050, kuhakikisha kila Mtanzania anapata mtaji na nchi inakuwa na hifadhi salama ya chakula.
Akielezea namna ya kupata mkopo huo, Ng’urah amesema mkulima anapaswa kuainisha mahitaji yake ya vifaa vya kuhifadhi mazao kama vile magunia maalumu, silos (vihenge vya kisasa au teknolojia za plastiki kwa ajili ya mazao ya nafaka.
Baada ya hapo, mkulima anapaswa kuomba mkopo kwa ajili ya thamani ya vifaa vya kilimo anavyohitaji kwa ajili ya kuhifadhia chakula
“Mikopo hii inatolewa kwa ruzuku ya hadi asilimia 30 ya thamani ya vifaa hivyo ili kupunguza gharama kwa mkulima,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Agra Tanzania, Vianey Rweyendela amesema ushirikiano huo utasaidia kuwahamasisha wauzaji, wazalishaji na wasambazaji kutumia suluhisho bunifu na rafiki kwa mazingira huku ukiimarisha miundombinu ya uhifadhi na ushughulikiaji wa mazao baada ya mavuno.
“Athari za mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania, na kusababisha matukio ya hali mbaya ya hewa kuwa ya mara kwa mara na ya muda mrefu zaidi kama ukame, mafuriko, mawimbi ya joto, uvamizi wa nzige na kuenea kwa jangwa,” amesema Rweyendela.
Aliongeza kuwa ukame unaojirudia mara kwa mara unaendelea kufupisha misimu ya kilimo na kupunguza uzalishaji wa mazao, hasa katika maeneo yenye changamoto za kilimo.
“Programu ya Re-Gain inalenga kuongeza uwezo wa wakulima wadogo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha matumizi mapana ya suluhisho za kupunguza upotevu wa chakula katika nchi saba za Afrika, ikiwemo Tanzania,” ameongeza.