SIMBA iko kwenye moto sana, inapiga inavyotaka. Ni timu mbili pekee ambazo hazijaonja kipigo kutoka kwa wekundu hao kwenye ligi lakini moja inajua machungu ya kipigo hicho, ikionyesha ubora mkubwa uwanjani lakini nyuma ya mabadiliko hayo kuna huyu Steve Barker.

Kuanzia Simba ilipoanza maisha na Barker ghafla mambo yamebadilika kwenye kikosi hicho, wekundu hao wakianza kurudi kwenye zama za ubora ambao ulizoeleka kabla kwa kuwa tishio uwanjani tofauti na ilivyokuwa kabla ya ujio wa kocha huyo.

MECHI 30 BILA KUFUNGWA

Barker ameiongoza Simba kucheza jumla ya mechi 30 bila kupoteza ambapo kwenye idadi hiyo kuna mechi 15 za Ligi Kuu Bara ambako tangu aanze mchezo wa kwanza Januari 18, 2026 dhidi ya Mtibwa Sugar alipoanza kwa sare ya bao 1-1 tena nyumbani kocha huyo hajapoteza mechi yoyote.

Kwenye ligi pia Simba ikiwa chini ya Barker imetoa sare mechi saba ambazo ndio kama matokeo mabaya kwa wekundu hao, ikionyesha mabadiliko makubwa ya ubora.

Simba pia imecheza mechi tatu za Kombe la Muungano bila kupoteza ikishinda zote mpaka ikachukua ubingwa huo, mashindano yaliyofanyika Kisiwani Zanzibar katika Uwanja wa Amaan.

Ukiondoa hizo za Muungano, pia Simba imecheza mechi tano za Kombe la Shirikisho la CRDB na mchezo wa mwisho ilicheza juzi jijini Arusha ikiifunga Coastal Union kwa mabao 4-0 ikitinga fainali ya mashindano hayo.

MOJA TAYARI

Barker ameshamaliza ukame wa mataji ndani ya Simba katika msimu wake wa kwanza tu, akiipa Simba Kombe la Muungano kwa kuifunga Yanga kwa bao 1-0 na kutatua kitendawili kigumu kwa mashabiki wa klabu hiyo ambao walikuwa na unyonge wa kuona kikosi chao kinamaliza kiu hiyo.

USAJILI FRESH,SIMBA YA KASI

Mabadiliko makubwa ya Simba yalianzia dirisha dogo la usajili baada ya kocha huyo kusimamia kusajiliwa kwa wachezaji nane wakija kukiongezea nguvu kikosi hicho na saba kati yao wakafanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa na kuwapa nguvu wekundu hao.

Simba chini ya Barker ilimsajili kipa Tanji Kassali, mabeki Nickson Kibabage na Ismael Toure, viungo wakiwa Anicet Oura, Lebase Gueye, Clatous Chama na Inno Loemba, pamoja na mshambuliaji Baraka Mwangosi ambaye ndiye mchezaji pekee ambaye amekuwa akikosa mechi za wekundu hao.

Hapo kabla Simba ilikuwa na makosa mengi ya usajili lakini ujio wa Barker akashirikiana vyema na mabosi wa klabu hiyo kusajili wachezaji ambao wameleta tija kubwa kwa kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Simba uwanjani imejitambulisha kwa soka linalotokana na falsafa ya Barker ambaye anataka kuona kikosi hicho kikicheza soka la kasi wakati wote, hatua ambayo imeipa matokeo mazuri ya ushindi kwenye mechi hizo 30.

AGOMEA UNYONGE YANGA

Mashabiki wa Simba kwa sasa hawana wasiwasi na presha inapokuja wanakutana na Yanga, na ujasiri huo umetokana na namna Barker alivyofanikiwa kuwapa wekundu hao ubora katika dabi hizo.

Barker tangu atue Simba amekutana na Yanga kwenye mechi tatu na hajapoteza mchezo wowote akitoa sare mbili za ligi lakini pia akashinda mchezo mmoja. Simba ilirudi kujiamini baada ya kupoteza mechi tano mfululizo dhidi ya mtani wake huyo.

Matokeo mazuri dhidi ya Yanga ni kitu muhimu kwa afya ya ajira ya makocha ambapo hapo kabla mashabiki wa klabu hiyo walianza kuchukizwa na aliyekuwa kocha wao Fadlu Davids ambaye alipoteza mechi tatu dhidi ya mabingwa hao wa soka Tanzania ndani ya msimu mmoja.

CHAMA AMERUDI

Wakati Chama anaondoka Simba alionekana kama mchezaji ambaye umri umekwenda na hana cha kuongeza kwenye kikosi hicho, akaachiwa na kutua Yanga ambako hakufanya makubwa kama ilivyotarajiwa.

Kiungo huyo alipoondoka Yanga alitua Singida Black Stars alikocheza nusu msimu tu kabla ya Simba kumchukua Januari. Baada ya kurejea Simba, Mzambia huyo amekuwa kama amezaliwa upya akiwasha moto mkali, akifunga mabao nane, akitoa pasi za mabao saba na kuhusika kwenye jumla ya mabao 15.

BADO INATAKA MAWILI

Simba chini ya Barker bado ina nafasi ya kuongeza mafanikio zaidi ikiendelea kukimbizana na Yanga kwenye mbio za ubingwa wa ligi, timu hizo zikipishana kwa pointi mbili pekee, wekundu hao wakiwa nafasi ya pili na pointi 64 wakati vinara Yanga wakiwa na pointi 66.

Timu zote zimebakiza mechi tatu kumaliza msimu ambapo kama Yanga ikipoteza pointi tatu na Simba kushinda zote basi wekundu hao wanaweza kuchukua taji la pili msimu huu chini ya Barker.

Ukiacha mbio hizo za ligi, Simba pia inalitafuta taji la Shirikisho baada ya kuingia fainali kwa kuing’oa Coastal Union, ikiwa fainali ya pili kwa Barker akiwa na wekundu hao, ikisubiri kukutana na Azam kwenye mchezo utakaopigwa Julai 4.

MSIKIE BARKER MWENYEWE

Akizungumzia mwanzo huo mzuri ndani ya Simba, Barker alisema mafanikio hayo yanatokana na mahusiano mazuri ndani ya kikosi hicho, ambapo uongozi wa klabu umekuwa ukimpa ushirikiano mzuri pamoja na wasaidizi wake na wachezaji kujituma kwa nguvu.

“Kweli umekuwa mwanzo mzuri wenye changamoto mpya. Hili linatokana na namna ambavyo tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na uongozi wa klabu. Tumekuwa tukifanya kazi kama watu wenye lengo moja la kuitafutia mafanikio Simba,” anasema Barker.

“Ukiacha uongozi, kuna kazi nzuri inayofanywa na wasaidizi wangu kwenye benchi; wamekuwa watu muhimu kwangu. Wachezaji nao wamekuwa wakijituma sana. Ukiangalia, bila kujali changamoto ya ratiba ngumu ya mechi, wameendelea kupambana kutafuta matokeo mazuri.

“Tumekuwa kila mmoja akijituma kwa ajili ya klabu hii bila kuchoka. Mapambano haya ni maalum kwa ajili ya furaha ya mashabiki wetu. Wamekuwa ni watu muhimu sana wanaohamasisha wachezaji kwenye kila mchezo; kila uwanja tunaokwenda tunawakuta wamejaa kama ilivyokuwa mechi iliyopita.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *