MWANDAAJI wa mashindano ya Swahili Talent Swimming, Nelson Lawrence amesema yanalenga kuwafikia watoto wa kawaida na wenye mahitaji maalumu ili kukuza vipaji vyao mapema.
Swahili Talent Swimming inatarajiwa kufanyika Mei 23 na 24, mwaka huu, katika Klabu ya Gymkhana jijini Dar es Salaam.
Lawrence amesema maandalizi ya msimu wa tatu wa mashindano hayo yamekamilika na usajili umefungwa baada ya kupata washiriki 300 kutoka shule zaidi ya 25.
Ameongeza kuwa idadi kubwa ya washiriki ni watoto wenye umri wa miaka sita kushuka chini, jambo ambalo linaonyesha kuwa vipaji vya kuogelea vinaanza kuonekana tangu utotoni.
“Tumefika mwisho wa usajili na tumepata watoto 300. Wengi wao wana miaka sita kushuka chini, miaka saba, miaka nane na hilo ndilo lengo letu kuu kwa sababu vipaji vinaanzia utotoni na mara nyingi watoto wanakuwa navyo,” amesema Lawrence
Amesisitiza kuwa wamefanikiwa pia kuigusa jamii kwa kuwajumuisha watoto wenye mahitaji maalumu 23 kutoka Dar es Salaam na Arusha ambao tayari wanajua kuogelea.
Wadau mbalimbali wamejitokeza kudhamini mashindano hayo kwa kutoa zawadi na vifaa vitakavyosaidia kuwapa motisha washiriki.
Kwa mujibu wa waandaaji, mshindi wa kwanza hadi wa tatu watapatiwa medali huku washiriki wengine wakikabidhiwa vikombe ikiwa ni sehemu ya kuwapa hamasa ya kuendelea na mchezo huo.
Meneja wa Bidhaa wa kampuni ya Absa, George Kaindoah amesema wameamua kuunga mkono mashindano hayo kutokana na mchango wake katika maendeleo ya watoto na elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa michezo.
“Lengo letu ni kusaidia kukuza vipaji lakini pia kutoa elimu kwa wazazi juu ya umuhimu wa michezo kwa watoto wao,” amesema Kaindoah.
Kwa upande wake Meneja wa Masoko wa Afiya, Mohamed Salim amesema ni mara yao ya kwanza kudhamini mashindano hayo lakini wamevutiwa na namna yanavyowajumuisha watoto wengi pamoja na wenye mahitaji maalumu.
“Haya ni mashindano yenye shule zaidi ya 25 na tumevutiwa sana kuona watoto wenye uhitaji wakipewa nafasi. Sisi ni wadau wakubwa wa michezo na ndio maana tukaona ni muhimu kuwa sehemu ya mashindano haya,” amesema Salim.
Kocha wa Swahili Talent Swimming, Odilo Kamata amesema maandalizi ya kiufundi yamekamilika huku makocha wakijiandaa kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kushindana.
“Tumeifikia namba ambayo ilikuwa lengo letu na sasa tumefunga usajili. Tumejipanga vizuri kwa upande wa makocha na maandalizi yote yanaendelea vizuri,” amesema Kamata.
Ameitaja sababu ya mashindano hayo kuitwa ‘Swahili Talent’ ni kuhakikisha yanafika mpaka kwa watoto wa mitaani ambao mara nyingi hukosa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
“Tunataka kuwafikia wale ambao hawafikiki kirahisi na ndio maana tukaamua kutumia jina la Swahili ili kuibua vipaji hadi vya mtaani,” amesema.
Philip Saliboko, mzazi wa muogeleaji Colins Philip amesema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kukuza vipaji.
“Sisi wazazi tunataka kuona mchezo wa kuogelea unaleta sifa kubwa nchini na watoto wetu wanapata nafasi ya kufikia ndoto zao,” amesema.