
BAADA ya Simba SC kukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Steve Barker, amesema kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinatwaa angalau taji moja kati ya yale yanayowania msimu huu, huku akisisitiza kuwa kufanikiwa kutwaa yote mawili kutakuwa mafanikio makubwa zaidi.
Licha ya kuonyesha matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kwa sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na alama 64, pointi mbili nyuma ya vinara Yanga wenye alama 66.
Yanga inatarajiwa kucheza mechi muhimu dhidi ya Azam FC Juni 27, mchezo ambao unaweza kuwa na athari kubwa katika mbio za ubingwa. Endapo Yanga itapoteza au kutoka sare, Simba itapata nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kupigania taji hilo.
Ugumu wa mechi hiyo unaonekana kutokana na matokeo ya mzunguko wa kwanza na Yanga na Azam FC zilitoka sare ya bila kufungana katika mchezo uliochezwa Mei 15.
Kwa upande wa Simba, timu hiyo inatarajiwa kuvaana na Singida Black Stars Juni 27 katika Uwanja wa KMC Complex. Ingawa Simba ilishinda mabao 3-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Septemba 25, Barker anaifahamu vizuri Singida Black Stars kutokana na ushindani waliowahi kuupata katika mashindano ya ndani.
Akizungumzia malengo ya timu, Barker alisema kufuzu kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kumempa matumaini makubwa ya kumaliza msimu kwa mafanikio.
“Kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho ni jambo kubwa kwetu na linatupa imani ya kupigania taji. Tunatambua kuwa mechi zilizosalia ni ngumu na ushindani ni mkubwa, lakini tupo tayari kupambana,” alisema Barker.
Aliongeza kuwa wachezaji wake wanaendelea kuonyesha kiwango kizuri mazoezini na katika mechi, jambo linalompa matumaini ya kutimiza malengo yaliyowekwa mwanzoni mwa msimu.
“Tuna jukumu la kufanya vizuri katika mechi zote zilizobaki. Kiwango wanachokionyesha wachezaji kila siku kinatupa matumaini ya kumaliza msimu kwa mafanikio. Tunahitaji kushinda kila mchezo uliosalia,” aliongeza.
Simba imebakiza mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara. Itaanza kwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar Juni 24 katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, kabla ya kukutana na Singida Black Stars Juni 27 na baadaye KMC Juni 30, mechi zote zikitarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa KMC Complex.
Hadi sasa Simba imecheza mechi 27 za ligi, ikishinda 19, kutoka sare saba na kupoteza mchezo mmoja. Timu hiyo imefunga mabao 48 na kuruhusu mabao 11, ikikusanya alama 64.
Katika Kombe la Shirikisho la CRDB, Simba imeonyesha ubora mkubwa tangu hatua ya 16 Bora. Iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika hatua hiyo, kabla ya kuifunga TRA United mabao 3-0 katika robo fainali na kuichapa Coastal Union mabao 4-0 katika nusu fainali na kutinga fainali.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara Juni 30, fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB inatarajiwa kuchezwa Julai 4, ingawa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) bado halijatangaza rasmi uwanja utakaotumika kwa mchezo huo.