
Addis Ababa, Ethiopia ndiko yaliko Makao Makuu ya Muungano wa Afrika ambako leo kumefanyika mkutano wa 10 kati ya AU na UN ukiongozwa na viongozi wawili wa vyombo hivyo Guterres wa UN na Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika.
Baada ya mkutano, wamezungumza na waandishi wa habari na Guterres anayekamilisha n’gwe yake ya uongozi Desemba 31 mwaka huu akasema katika kipindi chake uhusiano kati ya vyombo hivyo viwili umeendelea kuwa imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote na kwamba hana shaka kuwa utaendelea kuimarika siku zijazo.
Amepongeza Muungano wa Afrika kama kinara wa ushirikiano wa kimataifa barani Afrika na sauti ya pamoja ya haki kwa ulimwengu unaoendelea.
Akikumbuka miaka yake ya ushirikiano na AU, Guterres amesema alianza tangu mwanzo wa muhula wake kujenga ushirikiano wa kipekee wa kimkakati na taasisi hiyo ya kikanda.
Guterres amesema, “ushirikiano huo umeleta maendeleo yenye maana kote Afrika katika masuala ya amani na usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu.”
Kuhusu tathmni ya ya mkutano, Katibu Mkuu amesema yeye na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf wametathmini ushirikiano katika maeneo manne makuu na kujadili namna ya kuendeleza ushirikiano wa siku zijazo.
Eneo la kwanza lilijikita katika kuimarisha uhusiano wa kitaasisi kati ya Umoja wa Mataifa na AU. Viongozi hao wawili wametia saini tamko jipya lililothibitisha upya mifumo ya ushirikiano wa pamoja na kurasimisha mifumo ya uratibu yenye lengo la kuboresha ushirikiano katika amani, maendeleo na haki za binadamu.
Eneo la pili lilihusu ufadhili wa maendeleo endelevu barani Afrika. Guterres ametoa wito wa kufanyiwa mageuzi kwa mfumo wa fedha wa kimataifa, akisema kuwa nchi za Afrika zinaendelea kukabiliwa na gharama kubwa zisizo za haki za kukopa pamoja na mizigo mikubwa ya madeni inayodhoofisha uwekezaji katika sekta muhimu kama afya, elimu na huduma za maji. Pia aliunga mkono kuanzishwa kwa Wakala wa Afrika wa Ukadiriaji wa Mikopo na kuongezwa kwa uwakilishi wa Afrika katika taasisi za fedha za kimataifa.
Mabadiliko ya tabianchi na nishati jadidifu ndio nguzo ya tatu ya majadiliano. Guterres ameonya kuwa Afrika bado iko katika hatari kubwa ya ukame, mafuriko na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi licha ya kuchangia kiwango kidogo sana cha hewa chafu duniani.
Amehimiza nchi zilizoendelea kuongeza ufadhili wa kukabiliana na athari mbaya za tabianchi na kusema Afrika inaweza kuwa kinara wa dunia katika nishati jadidifu iwapo vikwazo vya uwekezaji vitaondolewa.
Suala la nne muhimu lilihusu amani na usalama kote barani humo. Guterres amethibitisha tena uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa mpango wa AU wa “Kunyamazisha Bunduki” na kuangazia ushirikiano katika juhudi za upatanishi wa migogoro nchini Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ukanda wa Sahel na Libya.
Halikadhalika amekosoa kutotekelezwa kwa Azimio 2719 la Baraza la Usalama kuhusu Somalia, akisema uamuzi huo “hauwezi kueleweka.”
Amehitimsiha hotuba yake, Guterres akisema imekuwa heshima kubwa kufanya kazi na Afrika katika kipindi cha miaka kumi iliyopita na akasisitiza tena dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za bara hilo katika kutafuta amani, haki na maendeleo.