Katika ripoti hiyo mpya ya “Takwimu za Afya Duniani 2026 “, shirika hilo limesema dunia bado ipo mbali kufikia malengo yoyote ya afya ya SDGs ifikapo mwaka 2030 licha ya mafanikio yaliyoonekana katika maeneo kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maendeleo makubwa yamepatikana tangu mwaka 2010, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa asilimia 40 ya maambukizi mapya ya VVU, kupungua kwa matumizi ya tumbaku na pombe, pamoja na kushuka kwa asilimia 36 ya idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya magonjwa yaliyopuuzwa ya kitropiki

Upatikanaji wa huduma muhimu pia ripoti inasema umeongezeka kwa kiasi kikubwa, ambapo karibu watu bilioni moja walipata maji safi salama na zaidi ya watu bilioni 1.4 walipata nishati safi ya kupikia kati ya mwaka 2015 na 2024.

© UNAIDS/Daniel Msirikale Mgonjwa nchini Tanzania akipokea dawa za kupunguza makali ya VVU kutibu VVU.

Afrika yapiga hatua kubwa dhidi ya VVU na kifua kikuu

Ripoti imeonesha mafanikio ya kutia moyo katika baadhi ya maeneo, hususan barani Afrika. 

Kanda ya Afrika ya WHO ilirekodi kupungua kwa kasi zaidi kuliko wastani wa dunia katika maambukizi ya VVU kwa asilimia 70, huku visa vya kifua kikuu vikishuka kwa asilimia 28. 

Wakati huo huo, Kwa mujibu wa ripoti Kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia ipo kwenye njia nzuri ya kufikia lengo lake la mwaka 2025 la kupunguza malaria.

Hata hivyo, shirika hilo limeonya kuwa kiwango cha malaria duniani kimeongezeka kwa asilimia 8.5 tangu mwaka 2015, jambo linaloifanya dunia kuwa mbali zaidi na malengo ya kimataifa

Hatari nyingine za kiafya zinaendelea kuwaathiri mamilioni ya watu, ikiwemo upungufu wa damu kwa wanawake wa umri wa kuzaa ambao umeendelea kubaki asilimia 30.7 duniani, pamoja na kuongezeka kwa uzito kupita kiasi au utipwatipwa kwa watoto walio chini ya umri miaka mitano, ambao umefikia asilimia 5.5 mwaka 2024.

“Takwimu hizi zinaeleza simulizi ya mafanikio lakini pia ukosefu mkubwa wa usawa, ambapo watu wengi hasa wanawake, watoto na wale wanaoishi katika jamii zilizotengwa bado wanakosa mazingira ya msingi ya kuwa na maisha yenye afya,” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa WHO. 

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika mifumo imara na yenye usawa ya afya, ikiwemo mifumo madhubuti ya taarifa za afya, ni muhimu ili kuziba mapengo na kuhakikisha uwajibikaji.

Maendeleo ya huduma za afya kwa wote yapungua kasi

Ripoti hiyo pia imeeleza wasiwasi kuhusu kupungua kwa kasi ya maendeleo kuelekea huduma za afya kwa wote. 

WHO imesema kiwango cha huduma za afya kwa wote duniani kiliongezeka kwa kiwango kidogo tu kutoka asilimia 68 hadi asilimia 71 kati ya mwaka 2015 na 2023. Wakati huo huo, robo ya watu duniani walikumbwa na ugumu wa kifedha kutokana na gharama za afya, huku takribani watu bilioni 1.6 wakiingia au kuendelea kuishi katika umaskini kutokana na matumizi ya moja kwa moja ya huduma za afya mwaka 2022.

Licha ya vifo vya wajawazito kupungua kwa asilimia 40 tangu mwaka 2000 na vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kushuka kwa asilimia 51, nchi nyingi bado ziko mbali kufikia malengo ya mwaka 2030

© WHO WHO yaunga mkono kampeni ya dharura ya kutoa chanjo nchini Malawi baada ya kubainika kwa mgonjwa wa polio.

Shirika hilo la WHO pia limesema maendeleo ya kupunguza vifo vya mapema vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza yamepungua kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2015, huku hatari za kimazingira na kitabia zikiendelea kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika.

WHO yaonya kuhusu mgogoro wa ufadhili wa afya

Uchafuzi wa hewa pekee kwa mujibu wa ripoti hiyo uchafuzi wa hewa pekee ulichangia takribani vifo milioni 6.6 duniani mwaka 2021 huku ukosefu wa maji safi, huduma za usafi na mazingira salama ukichangia vifo milioni 1.4 mwaka 2019

Vilevile, ukatili dhidi ya wanawake unaendelea kuwa tatizo kubwa, ambapo mwanamke mmoja kati ya wanne duniani amewahi kukumbwa na ukatili kutoka kwa mwenza wake.

“Mwelekeo huu unaonesha vifo vingi ambavyo vingeweza kuzuilika,” amesema Dkt. Yukiko Nakatani Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu kwa ajili ya mifumo ya afya. Ameongeza kuwa “Kutokana na kuongezeka kwa hatari za kimazingira, dharura za afya na mgogoro unaozidi kuwa mbaya wa ufadhili wa afya, lazima tuchukue hatua za haraka kuimarisha huduma za msingi za afya, kuwekeza katika kinga na kuhakikisha mifumo endelevu ya ufadhili ili kujenga mifumo imara ya afya na kurejesha maendeleo katika mkondo sahihi.”

WHO imesema janga la coronavirus“>COVID-19 lilifichua zaidi udhaifu uliopo katika mifumo ya afya duniani. Kati ya mwaka 2020 na 2023, janga hilo lilihusishwa na takribani vifo vya ziada milioni 22.1 duniani zaidi ya mara tatu ya idadi rasmi ya vifo vya COVID-19 na hivyo kufuta mafanikio ya miaka mingi katika kuongeza matarajio ya maisha.

WHO yataka mifumo imara ya takwimu za afya

Ripoti hiyo pia imebainisha udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa takwimu za afya duniani

Kufikia mwisho wa mwaka 2025, ni asilimia 18 pekee ya nchi zilizokuwa zinawasilisha taarifa za vifo kwa WHO ndani ya mwaka mmoja, huku karibu theluthi moja ya nchi hazijawahi kabisa kutoa taarifa za sababu za vifo imesema ripoti. 

WHO imesema ni karibu theluthi moja tu ya nchi zinazokidhi viwango vya kimataifa vya ubora wa taarifa za vifo.

“Mapengo ya takwimu yanaathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa kufuatilia mwenendo wa afya kwa wakati halisi, kulinganisha matokeo kati ya nchi na kubuni hatua madhubuti za afya ya umma,” amesema Alain Labrique Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Kidijitali na Ubunifu katika shirika la WHO.

Amehimiza uwekezaji zaidi katika mifumo ya kidijitali, viwango vya utoaji taarifa na mifumo madhubuti ya kitaifa ili kuboresha maamuzi ya afya.

WHO imesema matokeo ya ripoti hiyo yanatoa ujumbe wa wazi kuwa maendeleo ya afya duniani bado ni dhaifu na hayatoshi, na imetoa wito kwa nchi na washirika kuongeza kasi ya hatua, kuimarisha mifumo ya afya na kuboresha ukusanyaji wa takwimu ili dunia irejee katika mkondo wa kufikia malengo ya afya ya mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *