Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndani ya siku 13 kueleza kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kusimamishiwa usajili au kutozwa faini kwa madai ya kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Alipotafutwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kufafanua kuhusu barua hiyo, ameeleza kuwa imetoka ofisini kwake.

Akizungumza leo Mei 13, 2026 nje ya Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, ambapo kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar iliyofunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa  Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema kuwa  wamepata barua hiyo. 

“Hata hivyo, katika hatua hii hatutakuwa tayari kuweka hadharani maudhui ya barua hiyo kwa kuwa tunaendelea kuifanyia kazi,” amesema Mnyika.

Amesema kuwa barua hiyo imetokana na maazimio ya chama hicho baada ya kufanya kikao  Kamati Kuu Aprili 28 na 29, 2026 pamoja na matamko mbalimbali ya Mei 2 na Mei 5 na kauli zilizotolewa katika nyakati tofauti kuhusu mwenendo wa kisiasa nchini.

Barua hiyo, inakuja ikiwa ni takriban mwezi mmoja tangu Chadema, ishinde maombi ya marejeo ya kesi ya mgawanyo wa mali na kuruhusiwa kuendelea kufanya shughuli za kisiasa, zilizokuwa zimesimama kupisha kesi hiyo.

Barua ya Msajili

Katika barua yenye kumbukumbu namba HA.322/362/16A/22 ya Mei 7, 2026, iliyosainiwa kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Kaimu Msajili, Sisty Nyahoza, ofisi hiyo imeeleza kuwa imebaini matukio kadhaa yanayodaiwa kwenda kinyume na sheria katika shughuli za chama hicho.

Barua hiyo, imeeleza kuwa miongoni mwa matukio hayo ni kauli zinazodaiwa kutolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kuhusu mpango wa kuitisha maandamano ya nchi nzima kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na kesi mahakamani.

Kwa mujibu wa Msajili, kauli hizo zinaweza kutafsiriwa kuwa ni shinikizo kwa mhimili wa Mahakama na zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa nchi, jambo ambalo limekatazwa chini ya vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Aidha, ofisi hiyo imenukuu kauli zinazodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Korogwe, Oliver Kisaka, zikielezwa kuwa ni za uchochezi na zinaweza kuhamasisha vurugu za kisiasa, hususan kutokana na rejea zake kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025 na kauli ya No Reform No Election.

“Nyinyi watu wa Kibamba mnaweza kuwa mnajichukulia poa lakini nyinyi kwenye siasa za Tanzania na siasa za Dar es salaam, nyinyi ni watu wa kuigwa na ni watu mfano, wakati machafuko yanatokea tarehe 29 Oktoba mimi ni moja ya watu ambao waliokuwa wamekamatwa na tulikuwa tumewekwa sehemu isiyojulikana, wakati mitandao inarudi inarudishwa mimi nilikuwa nataka kujua watu wameandama au hawajaandamana.

“Wamepiga kura au hawajapiga kura, askari mmoja akaja na simu yake baada ya mitandao kufunguliwa, nikamuuliza bwana vipi, akasema bwana nimekuletea kitu uone jinsi watu walivyosimama, nikasema watu wa wapi, akasema hawa watu ni wa Kibamba na Ubungo, katika sehemu iliyoonesha msimamo wa No reform No election ni Kibamba na Ubungo, maana yake ni kwamba inawezekana mageuzi makubwa ya nchi hii uasisi wake ukatokea katika jimbo hili msishangae,” amenukuliwa Oliver kupitia barua hiyo.

Barua hiyo, imerejea vifungu vilivyokiukwa ambavyo ni kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 (Toleo la Urekebu la Mwaka 2023) kinaeleza kuwa, chama cha siasa kinapaswa kuendeshwa kwa kufuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Zanzibar, Sheria ya Vyama vya Siasa.

Pia, kifungu cha 19(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinaeleza

kuwa, chama cha siasa hakipaswi kuruhusu viongozi au wanachama wake kutamka au kutumia lugha za matusi, kisasi, kashfa au maneno ya uchochezi yanayoweza kusababisha au kupelekea uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa nchi.

“Kesi ya Tundu Lissu ipo mahakamani, kushinikiza au kuhamasisha watu washinikize aachiwe ni kuishinikiza Mahakama itoe uamuzi wa kupendelea upande fulani, suala ambalo ni kinyume cha sheria za nchi yetu,” imeeleza barua hiyo.

Katika hatua nyingine, Msajili pia ameigusia taarifa ya Kamati Kuu ya Chadema iliyotolewa Mei 5, 2026, akisema baadhi ya maneno yaliyotumika yanaashiria kashfa, uchochezi na kudhalilisha taasisi za dola na viongozi wa Serikali.

Barua hiyo, imenukuu sehemu mbalimbali za taarifa hiyo ambazo zinamshutumu Rais Samia Suluhu Hassan, Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama kwa madai ya matumizi ya nguvu, ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhodhi madaraka.

“Kamati Kuu inasema kuwa kuwataka wananchi waheshimu sheria za nchi wakati huku genge la watu wachache kupitia CCM na kiongozi wao Samia Suluhu Hassan wakisigina haki zao ni kuwageuza wao kuwa ni mandondocha…Vijana na wote waliouawa mnamo  Oktoba 29, 2025 na wale waliotekwa, kuteswa, na kuuawa kabla na baada ya tarehe hiyo ni mashujaa wa taifa letu na Chadema inawatangaza hivyo,” imenukuu barua hiyo.

Msajili kupitia barua hiyo, amesema pamoja na Katiba kuruhusu vyama vya siasa kutoa maoni na kufanya shughuli za kisiasa, uhuru huo unapaswa kutekelezwa bila kukiuka sheria za nchi wala kutumia lugha za kashfa, dhihaka au uchochezi.

Kutokana na hali hiyo, Chadema imetakiwa kuwasilisha maelezo yake Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ifikapo Mei 20, 2026 saa 9:30 alasiri kueleza kwa nini hatua za kinidhamu zisichukuliwe dhidi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *