
Katika tamko lake liliotolewa leo mjini Geneva, nchini Uswisi, Türk pia amesema amesikitishwa na ripoti za kuuawa kwa makumi ya wavuvi kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya jeshi la nchi ya Chad kaskazini-magharibi mwa Nigeria.
“Nimeshtushwa na ripoti kwamba mashambulizi ya anga ya jeshi la Nigeria kwenye soko kaskazini-mashariki mwa jimbo la Zamfara yameua takriban raia 100 na kujeruhi wengine wengi. Pia nimeingiwa na hofu na kuhuzunishwa na ripoti kwamba makumi ya wavuvi wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya jeshi la Chad kaskazini-magharibi mwa Nigeria,” ameeleza Türk.
Amesisitiza umuhimu kwa nchi zote mbili kuchunguza matukio hayo yanayovuruga amani.
“Ni muhimu sana kwa mamlaka za Nigeria na Chad kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina, huru, na usio na upendeleo kuhusu matukio haya yanayoumiza na kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wowote wanawajibishwa, kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.”
Wito wa kufuata sheria za kimataifa katika operesheni za kijeshi
Türk ametoa wito wa dharura kwa majeshi yote mawili kuchukua kila tahadhari inayowezekana ili kuepuka madhara kwa wananchi wa kawaida wakati wa mapigano yao akisema “Natoa wito wa dharura kwa majeshi yote mawili kuchukua tahadhari zote zinazowezekana ili kuepuka madhara kwa raia.”
Türk. ameonya kuwa “Operesheni zao za kijeshi, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Boko Haram na kundi linaloitwa ‘Islamic State West Africa Province’ lazima zifanyike kwa kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu. Raia na mali zao hawapaswi kamwe kuwa shabaha ya mashambulizi.”