“Kutokana na haya mafunzo yamenipa msukumo yaani kupata picha kubwa ya Kwenda kutatua migogoro huko mitaani kwa njia za amani kabisa,” amesema Sada Hamadi, msaidizi wa kisheria, kwa lugha ya kiingereza Paralegal akizungumzia mafunzo hayo ya siku sita yaliyofanyika kuanzia Aprili 13  hadi 18 mwaka huu huko Pemba, visiwani Zanzibar nchini Tanzania.

Mafunzo hayo yametolewa kwa kushirikiana na asasi za kiraia na Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Zanzibar kupitia mradi wa uwezeshaji wa kisheria na upatikanaji wa haki (LEAP II), unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.

Meneja wa mradi, Gamaliel Sunu amesema lengo kuu la mafunzo ni kuwapa wasaidizi hao mbinu za kisasa za upatanishi na majadiliano ya amani, ili waweze kumaliza migogoro hiyo mapema bila kuhitaji kwenda mahakamani.

“Tumewalenga wasaidizi wa kisheria kwasababu hao ndio wanaofanya katika jamii, kwahiyo ni rahisi kwao Kwenda kuwasaidia wale watu ambao hawajiwezi katika jamii kwamfano haya makundi maalum; wanawake, Watoto, watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine katika jamii.” 

Aidha, Bw. Gamaliel ameeleza kuwa kisiwa cha Pemba kina familia duni na maeneo mengi ambayo hayana huduma za kutosha za kisheria, hali inayowafanya wananchi kuwategemea zaidi wasaidizi wa kisheria kutatua migogoro ya kifamilia, ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia.

“Kupitia haya mafunzo tumewapatia ujuzi wasaidizi wa kisheria ambao moja kwa moja utaenda kuhakikisha kwamba hawa wananchi wa chini wanaenda kupata haki bila malipo kabisa.”

Bi. Sada anarejea kufafanua majukumu yao katika jamii.

“Kwa huku Pemba ninaweza kusema kwamba ofisi za wasaidizi wa kisheria zipo kila wilaya, kazi zetu tumejikita zaidi kutoa msaada wa kisheria na pia kutoa elimu ya kisheria, kwenye jamii huko kuna watu ambao hawajui kuhusiana na mambo ya sheria, tupo sisi tunawasaidia jinsi ya kutatua migogoro yao, na kama mgogoro unakuwa ni mkubwa hatuwezi kuutatua basi tunamwelekeza wapi aende, na wakati mwingine tunamwongoza kwa hatua moja hadi nyingine hadi apate haki yake.”

Baada ya Pemba, UNDP inajipanga kufanya mafunzo hayo kisiwani Unguja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *