Katika taarifa iliyotolewa kutoka Damascus, Rome na Cairo, shirika hilo limesema limepunguza msaada wa dharura wa chakula kwa asilimia 50 kuanzia mwezi Mei 2026, kutoka watu milioni 1.3 hadi watu laki sita na nusu. Aidha, mpango wa ruzuku ya mkate (bread subsidy programme) uliokuwa ukiwanufaisha mamilioni ya watu kila siku umesitishwa.

Mamilioni ya watu bado wanakabiliwa na njaa

Kwa mujibu wa WFP, zaidi ya watu milioni 7.2 nchini Syria wanaendelea kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku milioni 1.6 wakiwa katika hali mbaya zaidi ya ukosefu wa chakula.

Shirika hilo limeonya kuwa familia nyingi zinashindwa kumudu mahitaji yao ya kila siku ya chakula, hali inayowalazimu kupunguza kiwango cha chakula wanachokula, kutumia vyakula visivyo na lishe ya kutosha au kuruka baadhi ya milo. WFP imeeleza kuwa hali hiyo inaweza kuongeza viwango vya utapiamlo, hasa kwa watoto.

Ruzuku ya mkate ilikuwa msaada muhimu

Kwa mujibu wa shirika hilo, mpango wa ruzuku ya mkate ulikuwa nguzo muhimu katika kusaidia familia zilizo hatarini kwa kuhakikisha bei ya mkate inabaki nafuu.

Kupitia mpango huo, WFP ilisaidia zaidi ya duka 300 ya kuoka mikate kwa unga wa ngano ulioimarishwa, na hivyo kuwezesha mkate wa bei nafuu kufikia hadi watu milioni nne kila siku katika maeneo yenye uhitaji mkubwa. Hata hivyo, kutokana na changamoto za kifedha, shughuli za shirika hilo sasa zitapunguzwa kutoka majimbo yote 14 ya Syria hadi majimbo saba pekee.

WFP yaonya kuhusu athari za kupunguzwa kwa msaada

Marianne Ward, Mkurugenzi wa WFP nchini Syria, amesema kupunguzwa kwa msaada huo hakusababishwi na kupungua kwa mahitaji ya kibinadamu bali ni kutokana na changamoto za ufadhili.Amesema Syria bado ipo katika kipindi kigumu cha kuimarika baada ya miaka ya migogoro, huku mamilioni ya wananchi wakiendelea kutegemea msaada wa chakula ili kuishi.

Wakimbizi wa Syria katika nchi jirani waathirika pia

Athari za uhaba wa fedha zimeathiri pia wakimbizi wa Syria wanaoishi katika nchi jirani kama Lebanon, Jordan na Egypt.

Nchini Jordan, WFP imesitisha msaada wa fedha za chakula kwa wakimbizi 135,000 wanaoishi katika jamii, huku ikiendelea kutoa msaada uliopunguzwa kwa wengine 85,000 walioko kambini. Nchini Egypt, Wasyria 20,000 wameathiriwa na kupunguzwa kwa msaada huo.

Samer Abdeljaber, Mkurugenzi wa Kanda wa WFP kwa Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Ulaya Mashariki, ameonya kuwa bila msaada wa haraka na endelevu wa kifedha, mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi yanaweza kupotea na mamilioni ya watu kuzama zaidi katika njaa.

Wito wa msaada wa haraka wa kifedha

Kwa sasa, WFP inahitaji dola milioni 189 za Marekani katika kipindi cha miezi sita ijayo kuanzia Juni hadi Novemba 2026 ili kuendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha ndani ya Syria.

Kwa mujibu wa shirika hilo, fedha hizo zitasaidia kuwafikia watu milioni 1.6 walio katika mazingira hatarishi zaidi, kuendeleza huduma za lishe na kuhakikisha mamilioni ya wananchi wanaendelea kupata mkate kwa bei nafuu wakati taifa hilo likiendelea na juhudi za kujijenga upya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *